
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
Kampala, Uganda. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema hawezi kugawana madaraka na kambi ya upinzani kwani alishinda kihalali kwenye Uchaguzi Mkuu wa Februari 18.
Akizungumza na kiongozi wa chama cha upinzani cha Farmers Party of Uganda (FPU), Meja Jenerali Benon Biraaro, Rais Museveni amesema anakaribisha pendekezo la kufanya mazungumzo na wapinzani kwa ajili ya kujadili mustakabali wa kisiasa wa taifa.
Alisisitiza kuwa yupo tayari kufanya hilo, lakini akasema hayuko tayari kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa itakayowashirikisha wanasiasa wa upinzani.
Alisema uchaguzi ulikuwa fursa nzuri kwa wanasiasa kujitafutia vyeo na kama wapinzani walishindwa kuwashawishi wapiga kura, wanapaswa kusubiri hadi uchaguzi.
Alisema wanasiasa hao hawapaswi kutumia njia za mkato kuingia serikalini.
“Kuhusu hilo la kuwa na mjadala wa pamoja kuhusu ustawi wa taifa letu niko tayari lakini siyo kusema tuunde Serikali ya umoja wa kitaifa.
Siko tayari kufanya hivyo kwani nilishinda kihahali na tume ya uchaguzi imeshatoa matokeo yake,” alisema Museveni.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Museveni kukutana na kiongozi huyo wa upinzani baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
Baadhi ya waangalizi wa kimataifa waliukosoa uchaguzi huo wakisema kuwa vyombo vya dola vilitumika kuwakandamiza wapinzani.
Katika hatua nyingine, kumekuwa na tetesi kwamba kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye ametoweka na hajulikani alipo.
Taarifa zinasema Besigye ambaye alikuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu kufanyika kwa uchaguzi, hayupo nyumbani kwake.
Polisi nchini hapa imekataa kuthibitisha au kukanusha kuhusu taarifa hizo.
Besigye amekuwa akisisitiza kuwa ndiye aliyepaswa kuwa mshindi kwenye uchaguzi huo akidai kuwa kuibiwa kwa kura zake.
Alikamatwa zaidi ya mara nane na baadaye kuwekwa katika kifungo cha nyumbani katika muda usiojulikana.
No comments :
Post a Comment