
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof Joyce Ndalichako akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Joseph Dar es Salaam, jana. Picha na Beatrice Moses
Dar es Salaam. Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tawi la Dar es Salaam wamemchongea Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Yunus Mgaya kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kwa kumwita ‘jipu’ na kumuomba amtumbue.
Profesa Mgaya alichongewa jana baada ya kufanya ziara ya kushtukia kwenye chuo hicho kilichopo eneo la Luguruni wilayani Kinondoni. Awali, wanafunzi hao waligoma kufanya mitihani kwa madai mbalimbali ikiwamo ya kufundishwa walimu wasio na sifa ya kuwa wahadhiri.
Akiwa mbele ya wanafunzi hao kwenye mkutano uliofanyika katika uwanja wa chuo hicho, Profesa Ndalichako ambaye wanachuo walimpokea kwa vifijo, aliwahakikishia kwamba matatizo yanayowakabili yanatatuliwa chini ya TCU.
Kutokana na kauli hiyo, ndipo zikazuka kelele zikimtaja Profesa Mgaya aliyekuwapo hapo kuwa ni jipu.
“Hawezi huyo ni jipu, hatutaki mtumbue huyo,” zilisikika sauti za wanafunzi na kuzua mshangao kwa Waziri Ndalichako na viongozi wengine walioandamana naye akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Profesa Simon Msangila.
Profesa Ndalichako alisema chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kila mtumishi anapaswa kuwajibika, hivyo kama kuna matatizo TCU yatashughulikiwa.
“Nyie wenyewe hapa ni majipu mbona wengine mmekosa nidhamu mnazomea, nimewaheshimu wanangu, nimekuja kuzungumza nanyi badala tusikilizane vyema wengine wanaishia kuzomea kwenye matatizo yenu sioni ambalo linashindikana kupata ufumbuzi,” alisema Ndalichako.
Aliwaonya wanafunzi kufuata mkumbo kwa kuwa hali hiyo inaweza kuwasababishia wafukuzwe vyuo na kujikuta wakidaiwa fedha walizokopeshwa na Serikali.
“Ninawasihi mrejee kwenye masomo yenu tazama mmeshindwa kufanya mtihani tangu Jumatatu, Serikali ipo makini na nyie ndiyo maana mnapata mikopo mna sifa za kuajiriwa popote hata serikalini, baada ya hapo tutataka mlipe mikopo yenu ili wengine nao waitumie,” alisema Ndalichako.
Akizungumza mara baada ya mkutano huo, Profesa Mgaya alisema wanafunzi hao hasa wanaosomea uhandisi wanamuita jipu kwa sababu hakuwatimizia walichohitaji.
“TCU ilituma wataalam wake kufanya uchunguzi wa mazingira kulingana na malalamiko ya wanafunzi, kweli tumekuta maabara ipo moja, lakini uongozi wa chuo umetuhakikishia vifaa vyao vipo bandarini kwa ajili ya maabara nyingine, kifupi matatizo yaliyopo hapa yanarekebishika,” alisema Profesa Mgaya.
Madai mengine ya wanafunzi hao yaliwasilishwa na Rais wa Serikali ya wanafunzi, Celestine Makota ambaye alisema hofu imewatawala baada ya kufungwa kwa matawi ya vyuo hivyo Arusha na Songea.
No comments :
Post a Comment