zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, March 10, 2016

Rais Magufuli ataka Watanzania kuiga ubunifu wa Wavietnam


By Julius Mathias, Mwananchi 
Dar es Salaam. Baada ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam kunufaika na mbegu ya samaki iliyochukua Ziwa Victoria, Rais John Magufuli amewataka Watanzania kujikita kwenye kilimo na ufugaji ili kukuza uchumi wa nchi na kuondokana na umasikini.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana baada ya mazungumzo yake na mwenzake wa Vietnam, Truong Tang Sang ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku nne, akiwa Rais wa kwanza kutembelea nchini tangu Serikali ya Awamu ya Tano (SA5) iingie madarakani.
“Mwaka 1976, Vietnam walikuja kuomba mbegu ya samaki kutoka Ziwa Victoria, leo hii wao ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa samaki duniani. Waliomba pia mbegu za korosho na sasa wapo mbele yetu kwenye kilimo hicho,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Kutokana na mazao hayo wamefanikiwa kupunguza umasikini nchini mwao, ilhali sisi tungali ni nchi maskini.”
Alieleza kuwa nchi hiyo imefanikiwa kuongeza kipato cha mwananchi kutoka Dola 100 za Marekani kwa mwaka hadi 2,000, huku ikipunguza umasikini kwa asilimia 50 hivyo kufanikiwa kujiondoa miongoni mwa nchi masikini duniani.
Pia, Vietnam inaongoza kwa kilimo cha mpunga na Rais Magufuli alisema taifa hilo linalima mara tatu kwa mwaka mmoja, hivyo kuwa na ziada kubwa ya chakula licha ya kuwa na eneo dogo la ardhi ukilinganisha na Tanzania.
“Ziara hii ni mahsusi kwetu kujifunza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, uchumi na biashara. Ni wakati wa kujifunza kutoka kwao imekuaje wameweza kukuza uchumi wao ndani ya muda mfupi na kutuacha tukiendelea kuwa masikini tangu tupate uhuru?” alihoji Rais Magufuli.
Alibainisha kuwa sasa thamani ya biashara kati ya nchi hizi ni Dola 300 milioni za Marekani (zaidi ya Sh600 bilioni) kwa mwaka, mpango uliopo ni kuimarisha miamala husika ili kuanzia mwakani kiwango hicho kianzie Dola bilioni moja (zaidi ya Sh20 trilioni).
“Katika mazungumzo yangu na Rais Magufuli msisitizo mkubwa tumeuweka kwenye uhusiano ya biashara na uchumi. Sekta za kilimo, ufugaji na mawasiliano ndizo zenye kipaumbele cha awali, sambaba na viwanda vya uchakataji na usindikaji samaki,” alisema Rais Troung.
CCM Lumumba
Baadaye Rais Troung alitembelea Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba kuzungumza na Mwenyekiti wake, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kabla hajamalizia siku yake kwa kukutana na jumuiya ya wafanyabiashara nchini.
Akieleza juu ya ugeni huo, Kikwete alisema vyama vilivyounda CCM; ASP na TANU, vilikuwa na uhusiano mzuri na chama cha Kikomunisti cha Vietnam, hivyo Rais huyo aliona ni busara kutembelea makao makuu ya chama hicho kilichoisaidia.
“TANU imekuwa na urafiki wa muda mrefu na Vietnam. Umoja wa Vijana umewahi kuchanga na kumtuma Rais Mstaafu, (Benjamin) Mkapa kuwasilisha kiwango kilichopatikana kwa ajili ya ukombozi wa taifa hilo, hata wakati inapambana na Marekani bado TANU iliendelea kuiunga mkono,” alisema Kikwete.
Biashara
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Chama Wafanyabiashara cha Wenye Viwanda cha Vietnam (VCCI), walikubaliana kutumia fursa za biashara zilizopo baina ya nchi hizi mbili ili kuimarisha uhusiano ambao wakuu wa nchi wameridhia. Mwenyekiti wa TPSF, Reginald Mengi alisema: “Tunaamini kuna mengi ya kujifunza kutoka Vietnam hasa kwenye kilimo. Kwa ushirikiano na wenzetu, ni imani yangu tutazitumia vyema fursa zilizopo.”
Kampuni ya Simu ya Halotel ni moja ya miradi inayoendeshwa kwa ubia kati Kampuni ya Simu Vietnam (Vietel) na Tanzania.  

No comments :

Post a Comment