zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, March 6, 2016

Tunawekeza asilimia kubwa ya muda wetu katika uendawazimu!

Makala
Jenerali Ulimwengu
Toleo la 447KATIKA nchi karibu zote barani Afrika, kipindi cha uchaguzi ni msimu wa shaka. Ni wakati wa makundi ya watu kufanya kila aina ya njama ili wapate ushindi, uwe ni ushindi halali au haramu.

Kipindi cha uchaguzi ndio muda wa watu kujiingiza katika matendo ya udanganyifu, ulaghai, wizi, rushwa, fitna, uongo, ubazazi, uzabizabina, chuki, uchawi, na mambo yote unayoweza kuyafikiria kama maovu. Ni kipindi kinachotufanya, sisi Waafrika, tushushe kabisa thamani ya utu wetu, tuuze nyoyo zetu na tujisabili kwenye nguvu za kiza za kila aina.


Ni kipindi cha hovyo kinachotufanya tupoteze akili na mantiki, tusiweze kutumia hata akili za kawaida. Tunakuwa punguwani, wendawazimu na misukule wa kutumikia mradi wa msimu. Nilikwisha kuandika kwamba hiki ni kipindi ambamo akili zetu huwa tunaziweka katika akaunti isiyotumika ili tushiriki katika uchaguzi, tukiahidi kurudi kuzikomboa pindi uchaguzi utakapomalizika.


Kwa jinsi ambavyo sote huwa tunakumbwa na kiwewe, ni bahati njema kwamba vipindi vya uchaguzi huwa havipo kila mwaka, kwa kuwa kama ingekuwa kila mwaka tunaingia katika aina hii ya kiwewe, baada ya miaka ishirini tungekuwa sote tunastahili kupelekwa Mirembe kama vichaa.
Hata hivyo hatujapona kabisa. Katikati ya vipindi vya miaka mitano kuelekea Uchaguzi Mkuu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakuwa na uchaguzi wake wa ndani ya chama. Sasa, hata vyama vingine navyo vimeweka utaratibu wa kufanya uchaguzi wa ndani.

Hadi hivi karibuni, vyama vya upinzani havikushuhudia hamasa kubwa katika chaguzi za ndani. Lakini kadri vinavyozidi kupata nguvu na kujiimarisha, ndivyo navyo vitaanza kuwa na mihemko hiyo inayokikumba chama-tawala leo.

Mihemko hii inatokana na nini? Sababu kubwa ni kwamba katika bara la Afrika, siasa ndiyo biashara kubwa kuliko zote. Hii ndiyo biashara ambayo inaweza kufanywa na mtu yeyote bila kujali uwezo wake, haiba ya mtu mwenyewe, wala elimu aliyo nayo, alimradi aweze kupepesa mdomo wake huku akisambaza kila aina ya uozo.


Lengo kuu linakuwa ni “kushinda” uchaguzi kwa njia yoyote ile inayowezekana bila kujali haki za wale tunaoshindana nao. Katika nchi nyingi, kipindi cha uchaguzi ndio wakati wa watu kuchinjana kwa sababu ya kubaguana na kutengana kwa misingi ya makabila yao na dini zao.


Kwa hiyo, tukitaka kukadiria ni kiasi gani cha uendawazimu tunauwekeza katika akili zetu, tunaweza kuanza kwa kujiuliza maswali yafuatayo na majibu yake ni kama haya ninayoyaelezea hapa. Kwanza, katika kipindi cha miaka mitano tuna miezi mingapi? Jibu ni kwamba tuna miezi 60. Miezi sitini ni siku ngapi? Jibu ni siku 4,800.


Swali linalofuata litakuwa, katika kipindi cha miezi 60 ni miezi mingapi inatumika katika uchaguzi? Jibu litakuwa kwamba katika mwaka ambamo uchaguzi hufanyika miezi 12 yote hutumika kwa shughuli zinazohusiana na uchaguzi, ndiyo kusema tangu watu “wanachukua fomu”; wanazitembeza; zinajazwa; wanazirejesha; wanaunda timu za kampeni; wanaanza kampeni; wanakusanya fedha; wanauza nyumba za familia zao; wanawapinga wapinzani wao na kuwaua ikibidi; kura zinapigwa na kuhesabiwa; kura zinaibwa na walioshindwa wanatangazwa kuwa washindi; walioshinda wanalalamika na kuandamana; polisi wanapiga mabomu ya machozi na baadhi yao wanakufa; hatimaye hali ya “utulivu” inarejea lakini wananchi wengi wanatembea na kinyongo moyoni. Yote hii inachukua takriban siku 360 za uendawazimu.
Tukiongeza miaka ya uchaguzi wa ndani ya vyama vikubwa, hizo ni siku nyingine 360 za uendawazimu. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba, kwa wale wanaohusika moja kwa moja na uchaguzi mkuu na uchaguzi wa ndani ya vyama, jumla ya siku 720 kati ya siku 1,800 (miaka mitano) zinatumika katika uendawazimu. Ndiyo kusema tunatumia takriban asilimia arobaini (40%) ya muda wetu katika uendawazimu.


Katika asilimia 60 za muda zinazobakia, inabidi tuondoe asilimia kadhaa inayochukuliwa na mambo mengine ya kipuuzi yasiyohusika na uchaguzi. Asilimia kadhaa inachukuliwa na mifumo mibovu katika elimu yetu, kwa maana ya watoto kwenda shule bila kujifunza lolote la maana. Asilimia nyingine inachukuliwa na ufisadi uliotanda katika kila sekta ya shughuli za nchi. Nyingine itapotelea katika shughuli zisizokuwa na tija, na zenye madhara makubwa, kama matumizi ya mihadarati, ulevi wa kupindukia, na ufisadi wa kawaida. Inawezekana tukijumlisha asilimia zote hizo, tutajikuta na asilimia isiyozidi 10 tunayoiwekeza katika shughuli za maana.


Kama hiyo ni kweli, hata kama ingekuwa ni nusu ya hesabu zangu, ni nani anashangaa kwamba hatupigi hatua za maendeleo? Iwapo asilimia hiyo ya muda wako unaitumia katika uzuzu na uzezeta, ni muda gani unasalia ambao unaweza kuutumia ukifanya mambo ya akili?
Tuangalie uchaguzi uliopita mwaka jana. Hadi sasa uchaguzi huo haujakamilika. Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, alifuta uchaguzi wa Visiwa hivyo. Sasa ametangaza tarehe ya uchaguzi mpya. Wapinzani wamesema hawatashiriki katika uchaguzi mpya, wakisisitiza kwamba tume hiyo inajua aliyeshinda uchaguzi wa Oktoba na wakiitaka tume imtangaze.


Kwa hiyo tumeingia kipindi kingine cha “vuta-nikuvute” visiwani Zanzibar, na kwa maana hiyo ile asilimia ya uendawazimu inazidi kuongezeka. Hakuna ajuaye ni nini hasa kitatokea visiwani humo, lakini tunatakiwa tujifunze kutokana na historia kwamba maafa yanaweza kabisa kutokea kutokana na awamu hii ya uendawazimu.


Jijini Dar es Salaam bado madiwani wanavutana kuhusu nani awe meya wa jiji. Kila aina ya uhuni inafanywa na wahusika ili upande wanaoupendelea ushinde. Kinachotumika hapa ni uhuni na ujanja, na wala si akili, mantiki wala hekima. Tangu matangazo ya biashara yalipoanza kutuambia, “Kuwa mjanja!” tumeachana na akili tukakumbatia uhuni.


Dalili kwamba hata katika chaguzi nyingine chama-tawala kililazimisha ushindi zi wazi kabisa. Iwapo chama hicho kinaonekana waziwazi kikitaka kubatilisha matokeo ya uchaguzi katika ngazi ya serikali za mitaa wakati sote tukiangalia, kuna sababu gani itakayotufanya tusadiki kwamba na kwingineko hakikulazimisha matokeo vivyo hivyo?


Tayari tunayo mifano kadhaa ya wananchi katika baadhi ya maeneo waliowalazimisha wasimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo waliyokuwa wameyahatamia. Pamoja na kwamba matokeo yalikuwa yamekwisha kupatikana, wasimamizi hao walikuwa wamegoma kuyatoa wakisubiri maelekezo “kutoka ngazi za juu.’’


Chaguzi za aina hii haziwezi kuzaa utawala wenye maana, kwa sababu utawala huo utakuwa umetokana na michakato ya kijanja na kihuni, michakato haramu. Isitoshe, chaguzi za aina hii zinazidi kueneza tabia za ubabe, wizi, uongo na uozo wote nilioutaja hapo juu na kuzidi kupunguza kiasi cha amani kilichopo miongoni mwetu.


Pia ni ishara ya kutisha ya jinsi tunavyoshindwa kutendeana haki. Tunakubali mjanja na mbabe ndiye apewe anachotaka bila kujali kama anayo haki ya kukipata au la. Uchaguzi wa aina hii si uchaguzi bali ni zoezi la wahuni linalotupeleka pabaya, kwa sababu linazidi kutufundisha sote kuwa wahuni.


Tumeiona hali ya Zanzibar, ambako maneno ya kibaguzi yanavumiliwa na wakuu wa dola; tumeshuhudia jinsi watu walivyouwawa mwaka 2001 na nchi yetu ikatengeneza wakimbizi kwa mara ya kwanza kabisa. Tunajua, au tunapaswa kujua, kwamba hali ya sasa hivi inaweza kabisa kuturejesha huko, lakini tunajifanya hamnazo.


Tutakuja kujuta. 

- See more at: http://raiamwema.co.tz/tunawekeza-asilimia-kubwa-ya-muda-wetu-katika-uendawazimu#sthash.hwrI6pwD.dpuf

No comments :

Post a Comment