
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2011 na 2015, watu waliofariki dunia kutokana na ajali za barabarani ni 19,180, wanaume wakiwa 15,169 na wanawake 4,011.
Aidha, waliojeruhiwa kutokana na ajali hizo ni 85,515 wanaume wakiwa 63,895 na wanawake 21,620.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga, alipoulizwa sababu ya vifo vingi kuwa vya wanaume kulinganisha na wanawake, alitoa sababu sita ikiwa pamoja na wanaume wengi kuwa wazembe wanapotumia vyombo vya moto au barabara.Sababu zingine zilizotolewa na Kamanda Mpinga ni wanaume wengi kutumia kilevi zaidi ikilinganishwa na wanawake.
Pia Kamanda Mpinga alisema wanawake ni waangalifu wanapotumia vyombo vya moto au kutumia barabara, ingawa idadi ya wanaume wanaotumia vyombo vya moto ni wengi zaidi huku sababu nyingine ikiwa ni idadi kubwa ya wanaume kuwa ndio madereva ilikinganishwa na wanawake.
Sababu nyingine iliyotolewa na Kamanda Mpinga ni ile ya kuwa wanaume ndio wanaotafuta riziki ya familia ndio wengi, hivyo hujikuta wanatumia barabara au vyombo vya moto.
Hali katika miaka mitano
Mwaka 2011, waliofariki dunia kwenye ajali walikuwa 3,981, wanaume wakiwa 3,125 na wanawake 856 huku majeruhi wakiwa 20,802 kati yao wanaume ni 15,750 na wanawake 5,052.
Mwaka uliofuata, vifo vilivyotokana na ajali vilikuwa 3,969 kati yake wanaume wakiwa 3,129 na wanawake 840, huku majeruhi wakiwa 20,111 idadi ya wanaume ikiwa 15,088 na wanawake 5,023.
Kwa mwaka 2013, waliofariki dunia kutokana na ajali ni 4,002 wanaume wakiwa 3,197 na wanawake 805. Majeruhi walikuwa 20,689, kati yao wanaume 15,488 na wanawake 5,201.
Katika mwaka 2014, waliofariki dunia kwa ajali walikuwa 3,760, wanaume 2,965 na wanawake 795 na majeruhi 14,530 wanaume 10,686 na wanawake 3,844.
Mwaka jana, watu waliofariki dunia kutokana na ajali walikuwa 3,468 wanaume wakiwa 2,753 na wanawake 715 huku majeruhi wakiwa 9,383 kati yao wanaume 6,883 na wanawake 2,500.
Ajali za pikipiki pekee
Mwaka 2010, ajali za pikipiki zilikuwa 4,363 ambazo zilisababisha vifo 683 na majeruhi 4,471 na mwaka uliofuata ajali zilikuwa 5,384 na zilisababisha vifo 945 na majeruhi 5,506 huku mwaka 2012 zikiwa 5,763 na vifo 930 na waliojeruhiwa walikuwa 5,532.
Mwaka 2013, zilitokea ajali 6,831 ambazo zikisababisha vifo 1,098 na majeruhi 6,578 wakati mwaka 2014 ajali zilikuwa 4,169 zilizosababisha vifo 928 na majeruhi 3,884. Mwaka jana, ajali za pikipiki zilikuwa 2,626 zilizosababisha vifo 934 na majeruhi 2,370.
Sababu za ajali nyingi.
Kamanda Mpinga akifafanua sababu za ajali nyingi ambazo zimekuwa zikitokea, pamoja na mambo mengine, alisema makosa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na mwendo kasi, uendeshaji wa hatari, ulevi, kuyapita magari mengine na kujaza abiria na mizigo kupita kiasi kuwa ni miongoni mwa vitu vinavyochangia ajali nyingi.
Mbali na sababu za kibinadamu, alisema ubovu wa vyombo vya moto ikiwamo mifumo ya magari kwenye usukani, breki, taa na matairi kupasuka ni sababu zingine za ajali hizo.
“Katika makosa ya kibinadamu uzembe na hasa mwendo kasi ndio unaochangia sana katika kundi hili. Pia matairi ni moja ya vyanzo vya ajali kutokana na kwisha kwa matairi yenyewe, matumizi mabaya ya matairi kama upepo usio sawa, mzigo mkubwa, mwendo kasi zaidi ya unaoruhusiwa na tairi lenyewe na matairi yaliyokwisha muda wake.
“TBS wanapaswa kusimamia uingizaji wa matairi nchini kwani mengine yanaingia yakiwa yamekwisha muda wake. Wanatakiwa kupiga marufuku uuzaji wa matairi yaliyotumika, utoaji wa elimu ya matumizi ya matairi kwa madereva na wamiliki,” alisema Kamanda Mpinga.
TBS yajikanyaga
Kutokana na kuwapo tuhuma za uzembe katika kukagua ubora wa magari na matairi yanayoingia nchini, ambayo ni chanzo cha ajali nyingi, gazeti hili liliwasiliana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kupata ufafanuzi. Ofisa Uhusiano Mkuu wa TBS, Roida Andusamile, alitaka atumiwe maswali kwa barua pepe.
Baada ya kutumwa kwa maswali hayo, gazeti hili lilifuatilia majibu kwa zaidi ya wiki moja bila mafanikio kufanikiwa huku maofisa wa shirika hilo wakirushiana mpira.
Mara kadhaa, Roida alipokuwa akipigiwa simu yake ya kiganjani, ilikuwa ikikatwa na kisha kutumwa ujumbe kwamba yuko kwenye kikao.
Alipotafutwa tena Februari 29, Roida alimwahidi mwandishi kuwa akitoka kikaoni atayafuatilia maswali aliyokuwa ametumiwa.
Baada ya muda, alipopigiwa alisema hajaenda ofisini na kumtaka mwandishi awasiliane na msaidizi wake aliyemtaja kuwa ni Neema Mtemvu.
Gazeti hili lilipomtafuta Neema siku hiyo, alisema maswali ameyaona na kwamba yanashughulikiwa na Mkurugenzi Mkuu, Joseph Masikitiko.
Machi 3, mwaka huu, alipotafutwa alisema kati ya maswali hayo moja ambalo linahitaji takwimu halijashughulikiwa kwa sababu hazipo.
Siku hiyo pia Neema alihoji kuhusu maswali hayo huku akiweka shaka kuwa yataiharibia TBS.
“Mimi naogopa naona kama yatatuharibia, yatatupa sifa mbaya. Unajua tuna kampeni tumeianza ya kukamata magari, kwani polisi wanasemaje kuhusu TBS,” alihoji.
Hata hivyo, mwandishi alipomweleza kuwa polisi imetaja moja ya chanzo cha ajali ni ubovu wa matairi na mengine kuingizwa nchini yakiwa chini ya kiwango ndiyo maana inataka maelezo kwa upande wao, ndipo alipoahidi kutuma majibu siku inayofuata.
Siku iliyofuata alipotafutwa, alidai hayuko ofisini na kwamba majibu ameyaacha kwa Roida ili ayapitie kwa mara ya mwisho na kumtaka mwandishi amtafute (Roida).
Roida alipotafutwa alisema, “Sijapewa majibu. Maswali yako bado yapo kwa mkurugenzi ofisini kwangu hayajafika,” aliongeza.
Baada ya majibu hayo, gazeti lilimpigia simu Masikitiko, ambaye baada ya kuulizwa kama ofisi yake imepokea maswali hayo, alisema hajayaona na kuahidi kuyafuatilia kisha kumpigia mwandishi baada ya muda.
Baada ya muda kupitia bila mwandishi kupigiwa, alipomtafuta simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment