dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, April 7, 2016

CUF isikate tamaa bado ipo nafasi ya kusonga mbele



By Masoud Sanani,Mwananchi
Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ndicho kikuu cha upinzani Zanzibar kinapita katika kipindi kigumu na kinatakiwa kupigana kufa au kupona ili kuhakikisha kinaendelea kuwa hai na imara zaidi.
CUF kwa upande wa Zanzibar ipo kwenye mtihani mgumu kutokana na hali ya kisiasa ilivyo Zanzibar kwa sasa na inahitaji uongozi makini na madhubuti ambao utaiwezesha kuvusha salama jahazi la chama hicho chenye wafuasi wengi zaidi visiwani humo ili lisizame.
Kama ni jahazi, basi CUF ipo katikati ya bahari kubwa yenye mawimbi mazito na isipokuwa na nahodha shujaa na hodari itaweza kwenda mrama na kuzama kuwa mwisho wa safari.
Kutoshiriki uchaguzi wa marudio
Pamoja na wadau kadhaa kuishauri CUF kwamba isisusie uchaguzi wa marudio, lakini chama hicho kimekataa ushauri huo na kususia uchaguzi huo ambao iliupa CCM ushindi mkubwa licha ya kwamba wagombea wa CUF nao walipigiwa kura.
Inawezekana kura hizo ni za wafanya kazi wa Serikali ambao walilazimika kupiga kura kwa kuhofia kufukuzwa kazi endapo wasingeshiriki.
CUF ilifanya uamuzi wa busara wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio kwani kama chama hicho kingeamua kushiriki na kutolea macho uchaguzi huo hali ya hatari ingeweza kuzuka Zanzibar na hata umwagaji damu ungeweza kutokea.
Kwa CUF kususia uchaguzi huo kuliepusha shari kwani vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) visingekuwa tayari kuona chama hicho cha upinzani kinashinda kiti cha Urais wa Zanzibar na kushika madaraka jambo ambalo siku zote hawalitaki.
Katika mazingira ya aina hiyo viongozi wa CUF walifanya uamuzi wa busara kwa kutoshiriki uchaguzi huo kwani yalisaidia kuwaokoa wafuasi wake katika dhahma ambayo wangeipata kama wangeshiriki uchaguzi huo.
Mtihani mgumu
CUF ipo kwenye mtihani mgumu wa kurudisha imani ya wafuasi wake na kuwaweka sawa kwani wamejenga imani kwamba hata wakifanya nini na wakiipigia kura nyingi kiasi gani haiwezi kupata madaraka kutoka na rekodi ya kushindwa mara nyingi waliyonayo.
Wafuasi wa chama wakijenga imani hiyo unakuwa na kazi kubwa ya ziada ya kuifuta na kuwaweka tena kwenye mstari ili ukitokea uchaguzi mwingine waweze kushiriki kupiga kura kwani watakuwa wamekata tamaa.
Viongozi wa CUF ni lazima wapange mikakati ya kurudisha imani ya wafuasi wao ambao kwa kipindi kirefu cha uhai wa chama hicho wamekuwa wakipigana vita ya kutaka kutwaa madaraka ya Zanzibar bila ya mafanikio.
Ni dhahiri kwamba wafuasi wa CUF mara zote wamekuwa wasikivu kwa viongozi wao kila wanapopewa amri ya kufuata, lakini jambo hili litawafanya viongozi hao watumie akili na nguvu za ziada kuwashawishi na wafuasi hao kukubali.
Mikakati ya kujiendesha
Chama cha Wananchi kitakuwa na kazi ya ziada ya kutafuta fedha za kujiendesha kwa vile ruzuku yao wanayoipata kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itapungua kwa vile hakina wajumbe wa Baraza la Wawakilishi safari hii.
Chama hicho kinategemea ruzuku itakayotokana na wabunge wake tu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa vyovyote vile haitakidhi matakwa yao hasa katika kipindi kigumu ambacho watakuwa wanapigania chama chao kisife.
Kwa hiyo, ni lazima wawe na mikakati madhubuti ya kutafuta fedha za ziada ikiwa ni pamoja na kutafuta misaada kutoka nje na michango kutoka kwa wafuasi wao ili kuweza kukiimarisha chama chao na kuweza kuhimili vishindo vya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Maandamano, mikutano ya hadhara
Katika mazingira ya sasa CUF haina budi kufanya maandamano na mikutano ya hadhara na kupata fursa kubwa ya kuzungumza na wananchi moja kwa moja badala ya mtindo wa kuzungumza nao kupitia vyombo vya habari.
Maandamano na mikutano hiyo ya hadhara itasaidia kuongeza hamasa ya wafuasi wa CUF na utii wa wafuasi hao kwa chama chao jambo ambalo litazidi kukiimarisha chama hicho.
Pia, maandamano na mikutano ya hadhara itawasaidia wafuasi wa chama hicho kupunguza joto la kisiasa linalowakabili katika mioyo yao na pia kupata nafasi ya kupunguza jazba kutokana na matukio yaliyo wasononesha yaliyowakabili katika kipindi cha karibuni.
Kwa mfano, wafuasi hao wa CUF wakifanya maandamano ya kutokukubaliana na uchaguzi wa marudio na ushindi uliopatikana kupitia CCM watakuwa wamejiliwaza kwani jambo linalochukiza unatakiwa kuliondoa kwa mikono yako au kwa maneno yako na kama umeshindwa yote hayo basi angalau kuonyesha umelichukia ingawa huu ni udhaifu.
Kuomba msaada kimataifa
Njia nyingine ambayo inaweza kutumiwa na CUF katika kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar ni kwa chama hicho kupiga hodi katika ofisi za jumuiya ya kimataifa kuomba msaada ili waingilie kati.
Pamoja na ukweli kwamba jumuiya hiyo haikutoa msaada unaohitajika katika suala la Zanzibar licha ya kutoa matamko ya kulaani mambo yanayotokea visiwani humo, lakini bado CUF ina nafasi ya kuomba tena msaada huo.
Pia, CUF inaweza kulipeleka suala la mgogoro wa kisiasa Zanzibar katika Mahakama ya Makosa ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi ili kushtaki na kuomba iamue suala hilo.
Pamoja na mambo yote hayo CUF ni lazima itafute haki yake kwa njia ya kidiplomasia na siyo ya kutumia nguvu na siku zote iwashawishi wafuasi wake wadumishe amani ili Zanzibar iendelee kuwa na utulivu na amani.
Mwandishi ni mwandishihabari mwandamizi amefanya kazi kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini. Anapatikana kwa email sanani07@yahoo.com na maoni@mwananchi.co.tz     

No comments :

Post a Comment