dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, April 7, 2016

Dakika 30 za Rais Magufuli mkahawani Mwanza


By Ngollo John, Mwananchi 
Mwanza. Machi 29, ni siku itakayosalia kwenye kumbukumbu za Meneja na Wafanyakazi wa Mghahawa wa Victoria Catering, uliopo eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Ni siku ambayo Rais John Magufuli aliweka historia kwa kuingia, kukaa na kula chakula na kunywa kwenye mkahawa huo wa kawaida akiongozana na mkewe, Janeth na viongozi wengine wa Serikali mkoani Mwanza.
Kama ilivyo mighahawa mingine ya kawaida nchini, Victoria Catering unaouza vyakula kwa bei za kawaida, chai ya rangi huuzwa kwa Sh200 huku chai ya maziwa ikiuzwa Sh300. Chakula cha bei ya juu ambacho ni wali, ugali, chips kwa kuku au samaki huuzwa kwa Sh4,500 kwa wanaokula papohapo, wakati anayehitaji kubeba hulazimika kuongeza Sh500 kwa ajili ya vifungashio kwa kila sahani.
Kwa anayehitaji kula wali maharage hutozwa Sh1,500 kwa sahani, huku soda zikiuzwa kwa Sh500 kwa chupa.
Meneja wa mgahawa
“Ilikuwa ni dakika 30 za hofu na woga ambayo mwishowe iligeuka furaha baada ya mauzo yetu kupanda kutoka kati ya Sh80,000 na Sh90,000 kwa siku hadi zaidi ya Sh200, 000,” anasema Meneja wa mghahawa huo, Elizabeth Maneno na kuongeza:
“Haikuwa jambo la kawaida, kumuona Rais akiingia kwenye mghahawa wetu wa kawaida wa chai ya Sh200.”
Akizungumza wakati wa mahojiano eneo la mghahawa wake, Elizabeth anasema siku hiyo waliuza na kumaliza vyakula, maji na soda zote.
“Tulipika kilo saba za mchele, ugali kilo nne, kilo mbili za nyama, kilo moja ya maharage na vyote vilikwisha hata watu wengine wakakosa chakula,” anasema Elizabeth na kuongeza:
“Hata sanduku nne za soda na katoni sita za maji ya kunywa ambazo huwa tunauza kwa siku tatu hadi nne, vyote viliisha siku moja na havikutosha. Yaani siku ile ilikuwa ya neema kubwa kwetu kwa mauzo.” 
Anasema maishani mwake hakuwahi kupata wazo kuwa kwa ipo siku angemhudumia kiongozi wa nchi katika mghahawa huo, ambao wateja wake wengi ni wafanyakazi wa uwanja wa ndege, madereva taksi, bodaboda na wageni au ndugu wa wasafari.
Ujio wa Magufuli
Kuhusu taarifa za ujio wa kiongozi huyo kwenye mgahawa wake, Elizabeth anasema: “Hatukujua wala kupata fununu kuwa Rais Magufuli angekuja kula kwenye mghahawa wetu; tungejua angalau tungefanya maandalizi hata kwa kuweka mandhari na mazingira inayolingana na hadhi yake tofauti na alivyotushtukiza.”
Hata hivyo, anasema: “Isipokuwa asubuhi ya siku ya tukio, kuna mtu tusiyemfahamu alifika na kuweka oda ya sahani 28 za chakula alizotaka ziwekwe kwenye vifungashio, ambazo sisi huuza kwa Sh5,000 kila shahani.”
Anasema baada ya kutoa taarifa kwa mhusika kuwa chakula alichoagiza kipo tayari, mtu huyo alibadilisha kauli na kumtaka kuandaa eneo kwa ajili ya wageni wake aliosema wameamua kula hapo mghahawani.
“Cha ajabu ni pale mtu yule alipokuja na kutuagiza kugawa chakula alichokiagiza awali kwa Rais Magufuli na ujumbe wake; hapo ndipo tuliposhtuka kuwa kumbe oda ile ilikuwa ya Rais Magufuli, mkewe Janeth na viongozi alioandamana nao,” anasimulia Elizabeth.
Alichokula Dk Magufuli, mkewe
Meneja wa mgahawa huo anasema, anachokumbuka chakula kilichopelekwa kwa Rais Magufuli na mkewe vikiwa kwenye vifungashio ni chipsi na kuku wa kukaanga, ambavyo thamani yake kwa kila sahani yenye kuku robo ni Sh5,000.
Aliyemhudumia Rais Magufuli
Hamida Miraji ni mmoja wa wafanyakazi katika mgahawa huo, ambaye ndiye alipata mshtuko anaoita bahati asiyoitarajia tena maishani mwake, kwa kumhudumia Rais Magufuli, mkewe Janeth na viongozi wa Mkoa wa Mwanza.
“Mwanzoni nilisita hata kuisogelea ile meza nilipotakiwa kuwahudumia; nilipatwa na hofu iliyochanganyika na woga lakini pia furaha ya kumuona rais uso kwa uso, tena akiwa ameketi mbele ya macho yangu nikitakiwa kumhudumia,” anasema Hamida na kuongeza:
“Nilipiga moyo konde na kuisogelea meza yao, nikiwa na chupa ya maji aina ya Kilimajaro kwenye sinia na kuwahudumia.”
Hata hivyo, Hamida anasema: “Nakumbuka niliwahi kumuona Dk Magufuli siku za nyuma, lakini kabla hajawa Rais wa nchi. Kipindi hicho alikuwa mbunge na waziri tu.”
Hamida anasema ingawa hatarajii kupata fursa adimu tena kama iliyomtokea Machi 25, kwa kumhudumia rais wa nchi aliye madarakani, anamuomba Mungu tukio hilo lijirudie siku nyingine, akiahidi kufanya vyema zaidi kuliko siku ile kwa sababu atakuwa amepata uzoefu.
“Ilikuwa mara yangu ya kwanza kumhudumia kiongozi wa nchi, pengine inaweza kuwa ndiyo ya mwisho, inagawa siombei iwe hivyo,” anasema Hamida.
Mghahawa, kiti cha Magufuli kugeuka lulu
Kwa mujibu wa Elizabeth, tangu siku hiyo kiti kilichokaliwa na Dk Magufuli kimekuwa kama lulu, kwani kila mteja anatamani akae hapo lakini wateja wameongezeka.
“Tangu siku ile, mauzo yetu yameongezeka kwa kupata wateja wengi zaidi huku kila mmoja akiulizia na kutaka kukikalia kiti na meza alivyotumia Rais Magufuli siku ile,” anasema Elizabeth na kuongeza:
“Baadhi hufika na kuagiza chakula kwa sharti la kukalia kiti hicho na pale wanapokuta mwingine kakikalia, wapo radhi kusubiri hadi aliyekikalia anyanyuke ndipo naye aagize chakula; yaani wakati mwingine inatubidi kucheka watu wanavyokigombania kiti hicho,”
Anasema imebidi kuongeza wingi wa chakula wanachopika, kutokana na wateja wanaomiminika kwenye mghahawa wao ambao hivi sasa umebatizwa jina la ‘Mghahawa wa Magufuli.’
“Ingawa uongozi haujafikiria kubadilisha jina la mghahawa, lakini tangu Machi 25 watu wameubatiza mghahawa wetu kutoka Victoria na kuuita ‘Mghahawa wa Magufuli’,” anasema Elizabeth ambaye ni meneja wa mgahawa huo.
Majirani, bodaboda walonga
“Nimefanya biashara eneo hii kwa muda mrefu, lakini hatujawahi siyo tu kuona kiongozi wa hadhi ya rais au Waziri Mkuu akiingia na kununua kitu hapa. Hata mawaziri wakisimama na kununua bidhaa, husalia ndani ya magari na kutuma wasaidizi wao,” anasema Joyce John, mmiliki wa mgahawa jirani na alipokula Rais Magufuli.
Mwendesha bodaboda nje ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Juma Abdallah anasema siyo tu kwa kula mghahawani kumemuongezea Rais Magufuli mvuto mbele ya umma, bali pia kitendo cha kufungua Barabara ya Igombe-Mwanza iliyofungwa kwa miaka miwili, kimefurahisha umma uliokuwa ukilazimika kuzungukia Nyakato kwenda na kurudi katikati ya Jiji la Mwanza.
“Kutoka Igombe hadi katikati ya jiji ni kilomita tano na nauli ni Sh700, lakini wananchi walikuwa wakilazimika kuzungukia Nyakato, umbali wa zaidi ya kilomita 18 kwa nauli ya Sh1, 500 kwa safari moja; ujio wa Rais umeleta faraja,” anasema Abdallah.
Rais alipowachomoka walinzi
Siku hiyo haikuwa ya kipekee kwa wafanyakazi wa Mghahawa wa Victoria pekee, bali hata kwa waimbaji wa Kwaya ya Kanisa la African Inland Churh (AIC) ya jijini Mwanza, ambao walifanya usajili wa muda wa mwimbaji mpya.
Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza pale Rais Magufuli alipoanza kunogewa na wimbo maalumu wa kwaya hiyo uliokuwa ukisisitiza amani Tanzania, alianza kuchezesha kichwa na mikono kabla ya kuchomoka ghafla katikati ya walinzi wake na viongozi wengine wa mkoa kisha kujichanganya na waimbaji.
Walinzi wakalazimika kujipanga kwa baadhi kujichanganya na rais katikati ya waimbaji, huku wengine wakizunguka nyuma na pembeni mwa waimbaji kuimarisha ulinzi wa kiongozi huyo ambaye tayari alianza kuimba kwa ufasaha na ‘wana kwaya wenzake’.
Wimbo uliomkuna Rais Magufuli na kufanikisha usajili wa muda katika kwaya ya AIC. ulisisitiza amani kwa wote bila kujali tofauti za kisiasa, kidini, kikabila wala maeneo.
Abiria wapata fursa kumsabahi Rais
Alipotoka kuimba na kucheza na wana kwaya, Rais Magufuli alipitia sehemu ya abiria wanaosubiria kusafiri na kupeana nao mikono.
Mara ya kwanza kurejea Chato
Tangu alipochaguliwa kuwa Rais na kuapishwa Novemba 5, mwaka jana, Machi 25 ilikuwa siku ya kwanza kwa Rais Magufuli kurejea nyumbani kwake Chato, ambako ametangaza kufyeka mishahara ya vigogo kutoka Sh40 milioni hadi Sh15 milioni na kuwataka wasiokuwa tayari kupokea kiwango hicho kuanza kutafuta kazi nyingine.
Akiwa Chato, Rais Magufuli akapata ugeni wa rafiki yake, Raila Oginga Odinga aliyeambata na mkewe Ida na binti yao, Winnie wakiwa wageni wa familia ya Rais Jumapili iliyopita wakasali pamoja katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikra Maria, ambako Raila akamuasa kuendelea kutumbua majipu huku akitenda haki kwa wote na kumtanguliza Mungu.     

No comments :

Post a Comment