dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, April 14, 2016

SAKATA LA MKATABA LUGUMI: Bunge mtegoni


  • *Utata waibuka, Naibu Katibu wa Bunge, PAC watoa kauli tofauti
  • *Katibu Mkuu Mambo ya Nadani adai amepewa maagizo maalum
  • *IGP amshushia mzigo Waziri kupeleka mkataba bungeni...
WAKATI mengi yakiendelea kuibuka katika sakata la ufisadi wa Sh. bilioni 37 kati ya kampuni ya Lugumi Enterprises Limited na Jeshi la Polisi, wengi wamekuwa wakihoji kama Bunge limezidiwa nguvu na jeshi hilo.

Hilo ni swali wanalojiuliza watu wengi baada ya kukiukwa kwa amri ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo Aprili 5, mwaka huu, ilitoa siku sita ipewe mkataba wa wabia hao wa kufunga mitambo ya kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi nchi nzima.

Baadhi ya wabunge wa CCM na wa upinzani waliopo kwenye kamati hiyo, wamedokeza kuwa, kinachofanya jambo hilo lionekane kuzidi nguvu muhimili huo ni kitendo cha PAC kukosa mwenyekiti ambaye kikanuni anapaswa kutoka upinzani.

“Kungekuwa na mwenyekiti ingesaidia sana, sasa hivi huku mara kuwe na shinikizo la viongozi wa chama, sijui serikali, kwa hiyo kidogo inakuwa ni shida,” alisema mmoja wa wabunge.Upinzani umesusia Kamati ya PAC na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kwa kile unachodai licha ya kamati hizo kuwa zao, CCM imekuwa ikiwachagulia ni nani anatakiwa kuwa mwenyekiti.

MAPYA YAIBUKA

Jana Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, aliliambia Nipasha kuwa, kilichoombwa na kamati hiyo siyo mkataba kati ya Lugumi Enterprises Limited na Jeshi la Polisi, bali ni taarifa tu za mkataba huo.

Wakati Joel akisema hivyo, Aprili 5, mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilary, alisema: “Tumewaomba (polisi) waje Aprili 11, watuletee mkataba huo tuuone kwa sababu haiwezekani tangu mwaka 2011 hadi leo kampuni hiyo iwe imefunga mashine katika vituo 14 tu, wakati fedha wameshalipwa.”

Hata hivyo, jana baada ya gazeti hili kutaka kujua endapo ofisi ya Bunge imeandika barua kwenda kwa jeshi hilo kama ambavyo PAC iliagiza, Joel alisema: “Barua imeshandikwa.”

Alipoulizwa kuhusu mamlaka ya kamati inapoomba taarifa kutoka kwenye taasisi yoyote ile na ikagomewa kama ambayo PAC imenyimwa mkataba huo, Joel alisema: “Ninachojua hawakuomba mkataba, wameomba taarifa, barua ambayo imekuja kwetu ni kuomba maelezo ya mkataba, wao wameomba maelezo na siyo mkataba, nadhani mtakuwa mmewanukuu vibaya”.

Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyekuwa kwenye mkutano siku PAC inatoa agizo hilo, aliliambia Nipashe kuwa katika hali ya kawaida haiwezekani kupeleka taarifa ya utekelezaji wa mkataba bila mkataba wenyewe, hivyo ni lazima mkataba upelekwe na kwamba katika hilo wamejipanga hawatakubali kuyumbishwa.

Jana Aeshi alitafutwa na Nipashe ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

KAULI YA IGP

Juzi, Nipashe lilizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, ambaye alisema jeshi hilo haliwajibiki kwa wabunge moja kwa moja.

Alisema Jeshi la Polisi linawajibika kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye yeye (waziri) ndiye anayewajibika katika Bunge.

IGP Mangu alisema Jeshi la Polisi halijapewa maagizo yoyote na PAC, ila maagizo hayo amepewa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye atawasiliana na jeshi hilo kwa ajili ya kupatiwa nyaraka yoyote inayohitajika na wabunge kisha yeye ataiwasilisha.

Alisema PAC haikuhitaji mkataba huo wa Lugumi kutoka Jeshi la Polisi, bali walihitaji vitu vingine na kuda kuwa waandishi wa habari wanaeleza jambo ambalo hawalifahamu kwa sababu siku ya mahojiano na PAC hawakuwamo ndani.

KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, alisema mkataba huo haujapelekwa katika kamati yoyote kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari (si Nipashe), vilivyoeleza kuwa umepelekwa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Alisema yeye ana maagizo maalum aliyopewa na PAC ambayo waandishi wa habari hawayafahamu kwa kuwa hawakuingia katika kikao cha kwanza kilichowajumuisha wabunge wa PAC na Jeshi la Polisi.

Alipoulizwa ni maagizo gani aliyopewa na kamati hiyo, Meja Jenerali Rwegasira alisema hawezi kuwaeleza waandishi wa habari bali mwenyekiti wa PAC peke yake ndiye mwenye mamlaka hiyo.

MKURUGENZI WA UPELELEZI

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani, alisema suala hilo wameanza kulifanyia kazi, lakini wanalishughulikia kwa sehemu ndogo kwa sababu linahusu Jeshi la Polisi.

Alisema sehemu kubwa inashughulikiwa na Takukuru, ambao wameshaanza kulifanyia kazi.

TAKUKURU WAZUNGUMZA

Ofisa Habari wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Tunu Mleli, alisema suala hilo limeshafika ofisini kwao na limeshaanza kufanyiwa kazi.

IGP MSTAAFU

Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, IGP Said Mwema, alipoulizwa kuhusu kuhusishwa kwake na suala hilo, alisema hawezi kuzungumza kwa sasa, bali anukuliwe alivyozungumza na baadhi ya vyombo vya habari mwishoni mwa wiki.
Katika mazungumzo hayo, Mwema alisema IGP ni ofisi, siyo mtu binafsi na jukumu hilo la u-IGP alikwishalikabidhi kwa mtu mwingine.

“Kama nitatakiwa mimi binafsi kutoa ufafanuzi nitatoa majibu na kama majibu au maswali yatahusu ofisi, basi ninaomba muwasiliane na waliopo ofisini, kwani IGP ni ofisi,” alisema Mwema.

WATAALAM WA SHERIA WANASEMAJE

Mwanasheria Bagiliye Bahati, alisema Kamati ya Bunge ama Bunge lina mamlaka ya kuomba nyaraka yoyote pindi inapohitaji.

Alisema Bunge ama Kamati ya Bunge itafanya uamuzi wa kuomba nyaraka hiyo kupitia Ofisi ya Spika hata kama nyaraka hiyo ni siri lazima kuwapo na maelezo ya kina, lakini mwisho wa siku endapo kutakuwa na ulazima wa Bunge kuona nyaraka hiyo, lazima itaiona.

Alisema hakuna siri ambayo Bunge halipaswi kufahamu, hivyo nyaraka yoyote ya siri ni lazima Bunge litafahamishwa na kwamba hata mahakama ikiomba nyaraka yoyote ni lazima ipelekewe.

“Kamati ya Bunge ama Bunge lenyewe lina meno, lakini tatizo linakuja wanayatumiaje hayo meno, kama kamati imeomba nyaraka ya mkataba na haijapewa, itakuwa ni udhaifu wa Bunge,” alisema Bahati.

Alisema kuna sheria ya kukaidi amri halali ya Bunge ambayo inampa uwezo Spika au mwenyekiti wa kamati kuamuru mtu kukamatwa au taasisi kukamatwa.

Naye Mwanasheria wa kujitegemea, John Mallya, alisema Kamati ya Bunge inaweza kumwita mtu yeyote au kudai nyaraka yoyote na ikapatiwa.

Alisema endapo mtu au taasisi ikikaidi amri ya Bunge, Spika wa Bunge ana mamlaka ya kumwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) kuomba mhusika huyo akamatwe.

“Hata Ester Bulaya (Mbunge wa Bunda Mjini) alitakiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge kuhojiwa lakini alipokaidi agizo hilo, Spika wa Bunge aliliandikia Jeshi la Polisi kumkamata na kweli alikamatwa na alifikishwa mahakamani,” alisema Mallya.

Wakati mkataba huo wa Lugumi ukionekana kuhenyesha muhimili huo wa dola, Bunge la 10 lilijiwekea historia ya aina yake baada ya PAC ya wakati huo, chini ya mwenyekiti wake Zitto Kabwe, kuwaweka ndani vigogo wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), baada ya kukaidi kutoa mikataba ya gesi.

Vigogo hao ni Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Michael Mwande na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa wake, James Andilile.

PAC ilikuwa imeomba kupatiwa mikataba 26 ya gesi kwa takribani miaka mitatu bila mafanikio.

Bunge hilo pia lilishupalia kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akauti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hali iliyofanya mawaziri, wenyeviti wa Bunge na mwanasheria mkuu wa serikali kuachia ngazi.

/Nipashe

No comments :

Post a Comment