dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, April 15, 2016

Takukuru yabeba faili la Lugumi


By Fidelis Butahe, Mwananchi 

Dar es Salaam. Sakata la kampuni ya Lugumi iliyoingia mkataba na Sh37 bilioni na Jeshi la Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima, sasa limetua Takukuru baada ya taasisi ya kupambana na rushwa kuchukua faili lake la usajili, Mwananchi limeleezwa.

Kampuni hiyo ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 106 ilizotakiwa kufunga, licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.

Wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikitaka nguvu itumike ili Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo, utata umeibuka katika umiliki wa kampuni hiyo kutokana na kuwepo tuhuma kuwa baadhi ya vigogo wa Polisi na wanasiasa ni wanahisa wa Lugumi Enterprises.

Jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi aliliambia gazeti hili kuwa Takukuru inashughulikia suala hilo, huku akibainisha kuwa kwa sasa Brela hawana takwimu za kina za kampuni hiyo.

“Kampuni hii ilisajiliwa kihalali na kupewa cheti cha usajili. Ila ninachoweza kukueleza kwa sasa ni kwamba jalada la usajili la Lugumi lipo Takukuru kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kinyusi jana wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake.

Kanyusi, ambaye hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu usajili wa kampuni hiyo, alisema: “Waandishi wa habari wamekuwa wakiniuliza maswali mengi kuhusu suala hili ila kwa sasa hali ndiyo hiyo. Jambo hili lipo Takukuru.”

Alisema kwa sasa kampuni zilizosajiliwa na Brela zipo 120,000 na zinakaribia kufika 130,000 na kwamba kampuni lazima zitoe taarifa zake kila mwaka, kinyume na hapo zinaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutwa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Brela zililieleza gazeti hili kuwa taarifa za usajili wa kampuni hiyo zilitoweka takribani miezi miwili iliyopita.

Mwandishi wetu alipofika katika ofisi za wakala huyo kwa ajili ya kupata ukweli wa usajili, alielezwa na mmoja wa watumishi ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi kwamba ni vigumu kupata hilo jalada kwa sababu ya mvutano ulioibuka.

Hata baada ya kufuata taratibu za kupewa jalada hilo kwa ajili ya kupitia masuala mbalimbali, alijibiwa kuwa jalada hilo halionekani ingawa baadaye Kanyusi alisema limechukuliwa na Takukuru.

Ufafanuzi wa Kanyusi umekuja wakati Mwananchi ikifuatilia utata wa wamiliki wa kampuni hiyo, usajili wake na taarifa zake za kila mwaka tangu iliposajiliwa.

Sakata la Lugumi liliibuka wiki iliyopita wakati PAC ilipokutana na Jeshi la Polisi kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na CAG.

Katika hesabu hizo ilibainika kuwa mwaka 2011, Polisi iliingia mkataba na Lugumi kwa ajili ya kufunga mashine hizo katika vituo 118 vya polisi kwa gharama ya Sh 37 bilioni.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kampuni hiyo imefunga mitambo hiyo kwenye vituo 14 tu, huku ikilipwa asilimia 99 ya fedha hizo.

Kutokana na ukakasi huo, PAC ambayo ilibaini viashiria vya ufisadi katika mkataba huo, iliagiza watendaji wa Polisi kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili kamati hiyo iweze kuupitia na kujiridhisha.

Lakini hadi sasa Jeshi la Polisi halijawasilisha mkataba huo, jambo ambalo huenda likazua mjadala mkali katika mkutano wa Bunge unaoanza Jumanne ijayo.

Usajili wa Lugumi

Hata hivyo, kupitia vyanzo mbalimbali ndani ya Brela, Mwananchi lilifanikiwa kuona sehemu ndogo ya taarifa za kampuni hiyo wakati ikisajiliwa.

Jalada la taarifa hiyo linaonyesha kuwa kampuni hiyo ilisajiliwa Julai 25, mwaka 2008 kwa namba 66716 kwa jina la Lugumi Enterprises Limited.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa wamiliki wa kampuni hiyo ni Said Hamad Lugumi mwenye hisa asilimia 40 na Juma Mosi Saburi mwenye hisa asilimia 10.

Zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ilianza na mtaji wa Sh50 milioni ambao uligawanywa katika hisa 1,000 na kila hisa ilikuwa na thamani ya Sh 50,000.

Katika hisa hizo 1,000, Lugumi alichukua hisa 40 na Saburi hisa 10 huku hisa 950 zikibaki katika kampuni hiyo.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kabla ya kusajiliwa kuwa kampuni, Lugumi ilikuwa imesajiliwa kama jina la biashara.

Katika eneo la shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo inaonyesha kuwa Lugumi inajishughulisha na masuala mbalimbali.

Taarifa hizo zinaonyesha kuwa Lugumi iliwasilisha taarifa zake za mwaka Brela kwa miaka mitatu ambayo ni 2015, 2011 na 2013.

No comments :

Post a Comment