dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, April 9, 2016

‘Ushauri kuhusu BoT ulipuuzwa’



“Skendo ya Epa haikuwa jukumu la BoT, hata Escrow, nilisikitika baada ya Epa, BoT kuingizwa tena kwenye Escrow, kama nchi hatukujifunza kuhusu kuzitenga kazi za BoT na mambo mengine.” Ludovick Utouh
By Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema akiwa katika ofisi hiyo alishauri Benki Kuu ya Tanzania kufanya kazi peke yake bila kushirikisha taasisi tanzu nyingine za kifedha, lakini ushauri wake haukufanyiwa kazi.
Utouh ambaye alifanya mahojiano maalumu na Mwananchi juzi alisema baada ya ukaguzi aliofanya kuhusu Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ambapo Sh 133 bilioni ziliibwa, alitoa mapendekezo ya moja kwa moja kuiacha BoT ifanye kazi zake peke yake, lakini hilo halikufanyiwa kazi na hicho ndicho chanzo cha benki hiyo kuhusishwa kwenye sakata la Escrow.
 “BoT ni chombo kitakatifu, kinapokuwa na skendo si nzuri kwa benki na kwa nchi,” alisema.
Kufichwa kwa ripoti
Katika mahojiano hayo, ambayo sehemu ya kwanza ilichapishwa kwenye gazeti hili jana, Utouh alizungumzia suala la baadhi ya ripoti alizofanya kutochapishwa na kuwekwa bayana.
Utouh alisema miongoni mwa ripoti hizo ni ile ya sakata la Epa ndani ya BoT.
 Alisema chanzo cha ripoti hiyo kutotolewa bayana ni ukaguzi wake kushindwa kukamilika kwa asilimia 100.
Utouh alisema ukaguzi huo ulibaini kuwa Sh90 bilioni za Epa ziliibwa, lakini ofisi yake ikashindwa kuthibitisha wizi wa Sh43 bilioni zilizosalia kati ya Sh133 bilioni zilizopotea.
Alisema ili ripoti ikamilike ulitakiwa kufanyika ukaguzi mwingine, lakini haukufanyika na sababu zake hazijui.
Utouh alisema ukaguzi wao licha ya kutokamilika lakini ulifichua mambo mengi na kusababisha baadhi ya wahusika kukamatwa, kufungwa na wengine kulipa fedha walizokuwa wameiba.
“Ripoti yetu haikutolewa kwa sababu haikukamilika, hii ni kawaida duniani kote, ripoti inayotolewa ni ile ambayo uchunguzi wake umekamilika kwa asilimia 100,” alisema.
Uchunguzi wa Escrow/Epa
Pamoja na mambo mengine, Utouh aligusia sakata la Escrow na kufafanua kitendo cha kukosa baadhi ya mafaili katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Leseni (Brela) ambayo yangesaidia katika uchunguzi, kuwa hilo ni kawaida kwa kuwa taasisi nyingine kama Takukuru huyachukua na kuyafanyia kazi.
Alipotakiwa kuzungumzia kwa undani kuhusu uchunguzi wa Escrow, Utouh alisema si sahihi kwake kuzungumza kwa kuwa hakukamilisha ripoti hiyo bali aliifanya kwa asilimia 90 tu.
Ukaguzi wa akaunti ya Tegeta Escrow uliombwa na Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini. Ukaguzi huu ulilenga kufanya uchunguzi wa kina na kutoa taarifa kamili yenye kuonyesha hali halisi kuhusu miamala (transactions) kwenye akaunti maalumu ya Tegeta Escrow kisha kutoa taarifa kuhusiana na ukaguzi huo.
Kashfa hiyo ilihusisha zaidi ya vigogo 50 wa Serikali katika uchotaji wa zaidi ya Sh306 bilioni katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Kasi ya Magufuli
Utouh alizungumzia kasi ya Rais John Magufuli  kuwa inaendana na ile ya CAG wa sasa, Profesa Mussa Juma Assad.
“CAG wa sasa anatakiwa afurahi kwa kuwa ana Serikali ambayo inatekeleza na inasikiliza yale ambayo anayaibua,” alisema.
Hata hivyo, aliisifu Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa kumpa ushirikiano na kuyafanyia kazi baadhi ya mapendekezo yake.
Utouh aliwataka Watanzania kuielewa na kuifuatilia ripoti ya CAG itakayopelekwa bungeni hivi karibuni ili kujifunza na kuwajibika.
Taasisi ya Wajibu
Utouh alizungumzia taasisi yake ya Wajibu ambayo alisema itajikita katika kubadili mtazamo wa Watanzania kuijua dhana ya uwajibikaji.
“Nilipokuwa CAG niliona kuwa watu wengi wanadhani uwajibikaji ni wa CAG au ni wa kamati ya Zitto au Dk Slaa, lakini Watanzania wote wana wajibu na kufahamu kuwa sisi ndiyo wadau wa maendeleo,” alisema. Alisema hata ripoti za CAG hazifanyiwi kazi ipasavyo na husahauliwa baada ya muda mfupi kwa sababu ya kukosekana dhana ya uwajibikaji. “Kila mtu awajibike, sisi wazazi tuwajibike na hata hii ya kutumbua majipu haitafika mbali  iwapo Watanzania hawatabadilika,” alisema.

No comments :

Post a Comment