Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Thursday, April 7, 2016

Wasomi, wachumi waipongeza bajeti, lakini waweka angalizo

WAKATI Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, jana akiwasilisha mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17 na kutaja kuwa ni Sh. trilioni 29.5, wasomi na wachumi mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu bajeti hiyo.

Wakizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, baadhi ya wanazuoni, walisema serikali ya awamu ya tano, inahitaji kujikita zaidi katika ukusanyaji kodi na kuwekeza zaidi katika viwanda.
Aidha, wamesema kuondolewa uanachama katika Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) na baaadhi ya wahisani kujiondoa kuchangia bajeti, hakutaifanya Tanzania kushindwa kutekeleza shughuli za maendeleo, kwani sekta ya viwanda, miundombinu, umeme na rasilimali za nchi, zitaongeza mapato ya ndani.
Dk. Joel Silas, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema serikali ni lazima iweke mikakati ya ukusanyaji kodi ikiwamo kodi ya majengo pamoja na serikali kuuza hati fungani kwa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Alisema serikali itaimarisha uchumi kupitia viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuvifufua na kuvijenga viwanda nchini.
Mbali na hayo, Dk. Silas alisema kuongezeka kwa bajeti elekezi ya mwaka fedha 2016/17 na kufikia shilingi trilioni 29.53 kutoka Sh. trilioni 22.4 ya mwaka wa fedha uliopita, kunaifanya serikali ijipange zaidi kwa kuweka miundombinu rafiki itakayowezesha waliojiajiri katika sekta binafsi kufanya shughuli zao kirahisi.
“Kuna umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu, umeme ufike hadi vijijini, ijengwe reli na barabara zitakazoziunganisha wilaya zote na kupitika kwa mwaka mzima, ili kufanikisha usafirishaji kutoka eneo moja hadi lingine, ingawaje tumeshaona kupungua kwa bei ya umeme ni mkakati mmojawapo,” alisema Dk. Silas.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Wilhelm Ngasamiaku, alisema kuongezeka kwa fedha kutoka katika vyanzo vya ndani ,kutategemea zaidi rasilimali za nchi hususan katika sekta ya utalii na madini.
Alisema bado serikali haijakusanya kodi ya kutosha kutoka katika sekta hiyo, ikiwamo ukusanyaji wa kodi ya majengo.
“Kuna sekta binafsi zina majengo mengi na kodi haikusanywi ipasavyo, hata sekta ya utalii na madini ukusanyaji si wa kuridhisha, serikali ikikusanya ipasavyo itapunguza ‘gap’ lililopo katika bajeti yetu kulingana na fedha za ndani na za wahisani tunazozitarajia,” alisema Dk. Ngasamiaku.
Naye Mshauri wa masuala ya uchumi Dk. Donath Olomi, alisema serikali imeendelea kuwa na bajeti kubwa ya matumizi ya kawaida, licha ya bajeti ya nchi kutegemea zaidi mikopo kutoka kwa wafadhili hali inayosababisha kutumia fedha nyingi kulipia deni.
Dk. Olomi alisema serikali inapaswa kupunguza bajeti ya misaada ya wafadhili kutoka nje ya nchi kwani mara nyingi wamekuwa hawaitoi fedha hizo kwa wakati.
“Uzoefu unaonyesha kuwa fedha za wafadhili hazitoki kwa wakati hivyo tunatakiwa tusitegemee sana misaada hiyo, kwani inachelewesha fedha za bajeti kufika kwenye miradi iliyoelekezewa,” alisema.
Kuhusu deni la Taifa, alisema kuna haja ya tahadhari kubwa kuchukuliwa juu ya madeni ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa ili zitumike vyema.
Alisema kuwapo kwa chombo cha kusimamia na kulipa madeni yote, kutasaidia serikali kulipa madeni.
Dk. Olomi alisema ili uchumi ukue kupitia viwanda na kupunguza umaskini, iwekwe mikakati ambayo inaonekana na serikali iboreshe viwanda vilivyopo vya watu binafsi na kufufua vile vilivyokufa badala ya kujenga viwanda vipya.
Naye Mhadhiri na Mtafiti wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja, alisema bajeti ipo katika muelekeo mzuri changamoto iliyopo Tanzania haina viwanda vya kuvisaidia.
Alisema viwanda vingi vilivyopo vinamilikiwa na watu kutoka nje ya nchi na siyo vya wazawa, hali ambayo inatakiwa serikali kuliangalia suala hilo kwa umakini.
“Mikakati inayowekwa kwa ajili ya kusaida viwanda haitekelezeke kwa kuwa sera imepitwa na wakati hapa inatakiwa kujenga taasisi ambazo zitasaidia Watanzania,” alisema Profesa Semboja.
Alisema serikali inatakiwa kuangalia katika vipaumbele vyake kama itatengeneza kilimo ambacho kitazalisha mazao kuingia kwenye viwanda.
Alisema kutengwe kwa mashamba makubwa yatakayosaidia kukua kwa viwanda ili kuongeza uchumi wa nchi na siyo kuwaachia wawekezaji kuwekeza wenyewe huku wazawa wakinyimwa.
Aidha, alisema bajeti ya mwaka huu ni kubwa na imeonyesha matumizi ya fedha kwenye upatikanaji wa mapato.
“Siku zote hatuwezi kuendelea katika bajeti kabla ya kupanga matumizi, unatakiwa kueleza jinsi ya kupata mapato na tunataka kusikia hawa wa ngazi za chini wanapataje ajira na siyo kusikia watu wanajilipa mishahara mikubwa,” alisema.
Aidha, alisema matumizi mabaya ya fedha, yamechangia kwa kiwango kikubwa kwa wahisani kukataa kutoa fedha zao.
Mchambuzi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda, alisema bajeti hiyo imeleta matumani katika kufanya mabadiliko.
Alisema trilioni 11.8 zilizosemwa kwa ajili ya maendeleo, zinatakiwa kutumika kama ilivyopangwa ili zionekane zinafanya mageuzi makubwa ya maendeleo.
“Mara nyingi zinapotengwa fedha za maendeleo, zilikuwa hazifiki katika miradi iliyokusudiwa, hivyo tunatakiwa kuhakikisha fedha hizo zinakwenda kwenye maendeleo,” alisisitiza Mbunda.
Alisema bajeti imeonyesha kiwango kidogo cha fedha kwa wafadhili, jambo ambalo ni nzuri kuondokana na utegemezi.
Imeandaliwa na Beatrice Shayo, Christina Mwakangale na Mary Geofrey

No comments :

Post a Comment