Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Wednesday, August 17, 2016

Maalim Seif ‘afutuka’ kusalimiana na Dk Shein!

Viongozi wa kitaifa waliyoshiriki katika sala ya maiti ya aliyekuwa rais wa awamu ya pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe iliosaliwa katika Msikiti wa Muembeshauri, Zanzibar, jana.

Mwinyi Sadallah – Nipashe
16 August 2016


MAZIKO ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi yaliwakutanisha takriban viongozi wote wa siasa wa Zanzibar na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Muungano.

Shughuli hiyo ya maziko ilikumbwa na taswira, iliyotoa hisia tofauti kwa watu waliyohudhuria kufuatia kitendo cha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ‘kufutuka’ kusalimiana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Maalim Seif na Dk Shein, walifanyakazi pamoja kwa muda wa miaka mitano katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), iliyoundwa mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.

Baada ya Sheikh Noiman Jongo, kutangaza kumalizika kwa shughuli ya maziko, viongozi wa kitaifa waliingia ndani ya nyumba ya marehemu wakiongozwa na Dk. Shein.

Hata hivyo, Maalim Seif alizunguka nyuma ya nyumba na kuanza kuondoka na walinzi wake wawili na kuelekea katika gari yake iliyokuwa imeegeshwa pembezoni nje ya nyumba ya marehemu Jumbe.Sala hiyo ya maiti ya kumsalia marehemu Jumbe ilifanyika katika Msikiti wa Mwembeshauri, Kariakoo, mjini Zanzibar, jana saa 7:00 adhuhuri.

Viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo ni marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume.

Wengine aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Omar Mahita.

Baada ya kukamilizika kwa sala ya maiti, jeneza la Jumbe, lilibebwa na mamia ya wananchi waliokuwa wamejitokeza na kupitia katika barabara za Kariokoo, Miembeni, Kilimani mpaka Migombani, takriban kilomita mbili kutoka Msikiti wa Muembeshauri, alikosaliwa maiti.

Akitoa shukrani kwa niaba ya familia yake, Mustafa Aboud Jumbe ambaye ni mtoto wa marehemu alisema, wanashukuru serikali kwa kuheshimu wasia wa baba yake wa kutaka azikwe kama muislamu wa kawaida.

“Tunashukuru serikali kwa kutukubalia ombi letu la kumzika bila ya kuhusisha taratibu za kiserikali kama alivyokuwa ameandika katika wasia wake,” alisema Mustafa.

Akisoma wasifu wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud alisema kuwa, Jumbe atakumbukwa kwa kufungua mlango wa demokrasia na misingi ya utawala bora kwa kuanzisha Baraza la Wawakilishi na kuandikwa kwa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Aboud alisema kuwa Jumbe alishiriki harakati za kutafuta uhuru wa Zanzibar akifanya kazi kwa karibu na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Alisema Jumbe aliacha kazi katika Serikali ya Kikoloni ya Kiingereza na kukitumikia chama cha Afro Shiraz kuelekea kupigania uhuru wa Zanzibar, hadi yalipofanyika Mapinduzi mwaka 1964.

Baada ya mauaji ya Karume mwaka 1972, aliteuliwa na Baraza la Mapinduzi kurithi kiti cha Karume hadi alipojiuzulu mwaka 1984 kwa kile kilichodaiwa kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa ya Zanzibar mwaka 1984.

Alisema mbali ya kufanya kazi ya ualimu, Jumbe alishika nafasi mbalimbali za uongozi kama Katibu Mipango wa ASP, Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kupitia jimbo la Fuoni kabla ya Mapinduzi na mnadhimu wa wenzake kupitia chama hicho.

Waziri Aboud alisema Jumbe alikuwa kiongozi jasiri na mtu mwenye kushirikiana na viongozi wenzake na alifanya kazi kwa karibu na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Alisema alishika nyadhifa za Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na pia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano kabla ya kuwa Rais wa Zanzibar, Aprli 11, 1972.

No comments :

Post a Comment