Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Tuesday, November 22, 2016

Mikutano ya Prof Lipumba na Maalim Seif yawaweka polisi matatani!


Wakati Jeshi la Polisi likizuia mikutano ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, hali ni tofauti kwa Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye ziara zake zinaendelea mikoani bila ya bughudha ya Jeshi la Polisi.

Uenyekiti wa Profesa Lipumba uliingia dosari baada ya kujiuzulu mwaka jana na baadaye kuandika barua ya kufuta uamuzi wake, jambo ambalo linapingwa na baadhi ya wanachama, wakiongozwa na Maalim Seif.

Nafasi hiyo ya Maalim Seif haijakumbwa na utata wa kisheria, lakini uendeshaji wa shughuli zake hasa Tanzania Bara umekumbwa na vikwazo, huku Profesa Lipumba akiendelea bila ya matatizo.Jeshi la Polisi mkoani Mtwara lilizuia mikutano ya Maalim Seif kwa maelezo kuwa mpaka pande mbili zinazosuguana ndani ya chama hicho zitakapokaa na kukubaliana.

Maelezo ya kuzuia mikutano hiyo yalitolewa na kamanda wa polisi wa mkoa huo, Thobias Sedoyeka, jambo lililomkera Maalim Seif ambaye alisema anajua kinachoendelea.

Juzi, Maalim Seif aliingia mkoani Lindi ambako pia alizuiwa kufanya mikutano, wakati Profesa Lipumba alifanya mkutano wa ndani Ijumaa iliyopita mkoani Morogoro.

Kamanda wa polisi wa Lindi, Renata Mzinga alisema wamezuia kwa sababu za kiusalama jambo lililomfanya Maalim Seif, aelekee Dar es Salaam kuendelea na shughuli nyingine.

Katibu wa CUF mkoani Morogoro, Shomvi Rajab alisema ziara ya Profesa Lipumba ilikuwa ya kawaida yenye lengo la kuimarisha chama.

“Ni kawaida kwa Profesa Lipumba kufanya ziara mikoani mara baada ya uchaguzi ili kufanya tathmini ya uchaguzi uliopita na kujipanga kwa uchaguzi ujao,” alisema Shomvi.

Alisema kabla ya kukutana na wanachama wilayani Morogoro, Profesa Lipumba amefanya ziara mkoani Tabora, Singida na Dodoma.

Katibu huyo alisema mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni hali mbaya ya uchumi ambayo wanachama waliilalamikia na Profesa Lipumba aliahidi kulifuatilia.

Kuhusu uhalali wa mkutano wa Morogoro, Kamanda Ulrich Matei alisema mikutano ya ndani ya kisiasa imesharuhusiwa na Serikali hivyo wao hawawajibiki kutoa masharti yoyote.

Wasomi wakerwa na hali hiyo

Wasomi walioulizwa na Mwananchi kuhusu hali hiyo, walikosoa vitendo vya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya Maalim Seif na kuruhusu ya Profesa Lipumba.

Walisema ili kuwapo uwanja sawa, Jeshi la Polisi lilipaswa lizuie mikutano viongozi wote wawili (Lipumba na Seif), badala ya kumuacha Profesa Lipumba kufanya mikutano huku, wakimzuia Maalim Seif.

Wakili wa kujitegemea wa mjini Dar es Salaam, Frank Mushi alisema kinachofanywa na polisi kinalitia doa jeshi hilo kwa vile kinaonyesha upendeleo wa dhahiri ambao haukustahili.

“Kinachofanywa na polisi ni double standard (kuwa na uamuzi tofauti kuhusu jambo moja). Haieleweki ni kwa kigezo gani?…Lipumba aliruhusiwa kufanya mikutano yake ya ndani, lakini Seif anazuiwa katika mikoa hiyo hiyo,” Wakili Mushi alisema na kufafanua:

“Polisi wameteleza katika hili na ukifuatilia sana mtu namba moja anayekiuka Katiba ni polisi. Jeshi letu linapaswa kufanya maamuzi kwa weledi ili lisitafsiriwe kuwa nalo linajiingiza kwenye siasa.”

Wakili huyo alisema kwa kuliangalia suala hilo kwa undani, mtu wa kawaida anapata picha kwamba kuna mmoja kati ya Profesa Lipumba na Maalim Seif anayependelewa na mwingine anaonewa.

“Kwanini wote wawili wafanye jambo sahihi kisheria ila mmoja kwake iwe shida. Tunaita double standard na hii isipoangaliwa itaendelea kupalilia chuki baina ya wafuasi wa CUF,” alisisitiza.

Jaji mstaafu ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema kwa vile tayari kuna kesi kuhusu uhalali wa uenyekiti wa Profesa Lipumba, walitakiwa wote wazuiwe.

“Nafahamu kuna kesi nisingependa sana kutoa maoni yangu, lakini ninachokiona kulitakiwa kuwe na zuio la mahakama kwa wote vinginevyo wanawachanganya wanachama wao,” alisema.

Wakili Peter Shayo wa mjini Arusha, alisema bodi ya wadhamini ya CUF ilipaswa kuomba amri ya muda ya kumzuia Lipumba kufanya mikutano hiyo ya ndani.

“Kulipaswa kuwe na zuio la muda la hicho kinachoendelea hadi mahakama itakapotoa uamuzi wake, lakini polisi kumzuia Seif na kumruhusu Lipumba kunaleta picha mbaya,” alisema wakili Shayo.

Profesa Efraim Senkondo wa mjini Dar es Salaam alisema kinachoendelea, kinaifanya jamii ipate picha kuwa huenda Profesa Lipumba anatumika kuidhoofisha CUF.

“Huenda Profesa anakuwa supported na authority (kusaidiwa na mamlaka) ili kuidhoofisha CUF na Maalim Seif,” alisema Profesa Senkondo.
/MWANANCHI.

No comments :

Post a Comment