Top Leaderboard Advert

Patreon

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, November 15, 2016

Rais ZLS amtaka Shein asisaini muswada wa mafuta na gesi!


Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein 

Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Omar Said Shaaban amemshauri Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kutokuusaini muswada wa sheria ya mafuta na gesi uliopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hivi karibuni kwa madai kuwa unavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Omari ameeleza msimamo huo katika barua yake ya maneno 1,293 aliyomwandikia Dk Shein akifafanua jinsi gani muswada huo unavunja sheria na rais huyo anavyoingizwa kwenye mtego wa kuvunja Katiba.

Katika barua hiyo iliyochapishwa kwa ukamilifu katika ukurasa wa 34 wa gazeti mwananchi, mwanasheria hiyo anasema:

“Mheshimiwa Rais, zipo taarifa kuwa unajiandaa kuweka saini kwenye muswada huo uliopitishwa na Baraza la Wawakilishi ili hatimaye iwe sheria. Naomba nikunasihi uachane na mpango huo ili kujiepusha na mtego wa jaribio la kuvunja Katiba.”
Anasisitiza: “Kwa heshima naomba nikueleze kuwa jaribio la Serikali yako na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na hatua yako ya kuweka saini muswada huo ili uwe sheria, ni uvunjaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo wewe umeapa kuilinda, lakini pia ni kinyume na maelekezo ya sheria inayorejewa kama ndiyo chanzo cha mamlaka ya Zanzibar kutunga sheria yake.”

Mwanasheria huyo anabainisha kuwa kama kweli nia ya dhati ipo ya kuondoa mafuta na gesi kwenye Muungano, hatua pekee na salama kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kusukuma kumalizika kwa mchakato wa Katiba Mpya au kupelekwa mabadiliko ya Katiba Bungeni kuliondoa jambo hilo kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba.

Omari alisema ameamua kutumia barua kwenye gazeti kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kufikisha ujumbe kwa Rais kwa kuwa kuna wakati wananchi wanapata tabu ya kujua ni njia gani sahihi ya kuwasiliana naye na kuhakikisha ujumbe wanaokusudia unamfikia.

Alisema akiwa mwanasheria tena kiongozi kwenye kada hiyo, ana wajibu wa kikatiba, kimamlaka na kitaaluma kusimamia ulindwaji na usimamizi wa Katiba na sheria za nchi na akiwa mwenye uchungu na Zanzibar, anapenda kuona ikisimamia rasilimali zake yenyewe bila ya kukiuka masharti ya Katiba.

Alibainisha kuwa katika Katiba ya Muungano kwenye nyongeza ya kwanza, suala la mafuta na gesi ni jambo la Muungano hivyo usimamizi wake na utungiwaji sheria kwa mujibu wa katiba zote mbili upo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hakuna mahali duniani kote ambapo suala lenye misingi yake kikatiba linaondolewa kwa “makubaliano ya viongozi wa wakuu wa Serikali,” anasema.

Wakati huo huo; Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein leo saa nne asubuhi atasaini Muswada wa Sheria ya uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ya mwaka 2016.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Dk Juma Mohammed Salum kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, ni kwamba Rais Shein atasaini muswada huo baada ya Baraza la Wawakilishi kuupitisha kwenye mkutano wa tatu wa baraza hilo lililofanyika Septemba.

Imeelezwa kwenye taarifa hiyo kuwa, kusainiwa kwa sheria hiyo kutawezesha kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar, kuanza kwenye visiwa vya Unguja na Pemba.

/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment