Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, February 4, 2017

MHE RAIS, TUNAKUOMBA UTUMBUE USAA HUU. AG NA DPP HAWAWEZI TENA KUFANYA KAZI PAMOJA. TUMBUA WOTE WAWILI. JIPU DAWA YAKE NI KULITUMBUA TU NA SIO KULIPAKA MAFUTA. VYENGINEVYO NI KUPOTEZA MUDA TU!!!

Siri gomvi la DPP, AG sasa hadharani

DPP Bwana Biswalo Muganga

Image result for AG WA TANZANIA
AG BWANA GEORGE MASAJU


HATIMAYE siri kuhusiana na mvutano baina ya Mwansheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Mkurugenzu wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, zimeanza kufichuka ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais John Magufuli kuwataka vigogo hao kutafuta suluhu baina yao kwa nia ya kufanikisha vyema shughuli za Serikali.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia vyanzo mbalimbali vilivyo karibu na wawili hao na pia kwa baadhi ya wabunge wa kamati inayoshughulikia sheria na katiba, umebaini kuwa mvutano uliopo kati yao ni wa masuala mazito yanayohusiana zaidi na majukumu yao.


Chanzo kimoja cha uhakika kiliiambia Nipashe jana kuwa mgogoro wa wawili hao ulianza kitambo na kwamba, chanzo kimojawapo kikubwa ni mamlaka aliyo nayo kikazi kila mmoja wao na pia, lipo pia suala la safari za kikazi.

Juzi, akizungumza katika sherehe za Siku ya Sheria jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwataka wawili hao kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo baina yao huku akiwakumbusha kuwa wote wana nguvu kubwa kwa sababu wameteuliwa naye. Rais alielezea pia kushangazwa kwake na kutokuelewana kwa DPP na AG ambao wanatoka ‘kumoja’.

“Nani asiyejua ofisi hizi za AG na DPP zinagombana wenyewe? Na Waziri (Dk. Harrison Mwakyembe) anafahamu mgogoro huu…na mbaya zaidi wote wanatoka sehemu moja. Kama ni suala la madaraka, wote ni wateuliwa wa Rais. Nitoe wito kwa ofisi hizi mbili mtafute solution(suluhisho) ,” alisema Rais Magufuli, ambaye pia aligusia mgogoro kuwapo kwa mgogoro kati ya Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi.

Chanzo kiliiambia Nipashe kuwa licha ya ukweli aliouelezea Rais kuhusu uteuzi wa DPP na AG, lakini kiutawala ofisi ya DPP huwa chini ya AG na huo ndiyo mzizi wa mvutano ulipo baina ya wawili hao.

Hata hivyo, chanzo kimongeza kuwa katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama, inaonyesha kuwa DPP anawajibika kwa Rais na siyo kwa AG.

“Mvutano uliopo baina ya wawili hao ni wa muda mrefu na kiukweli, pamoja na mengi yanayoweza kuelezwa, uzito wa madaraka waliyo nayo kila mmoja ndiyo mzizi wa yote haya yaliyowekwa hadharani na Rais Magufuli.

Ni kwamba kila mmoja anajiona ni mkubwa kwa mwenzake na hapo ndiyo penye shida," chanzo kilieleza kwa sharti la kutotajwa jina.

Aidha, chanzo kingine kilidai kuwa licha ya msuguano utokanao na uzito wa cheo cha kila mmoja, sababu nyingine ni masuala ya safari za kikazi, ikidaiwa kuwa wakati mwingine DPP na AG hulazimika kushirikiana katika kufanikisha suala hilo lakini mmoja wao humlalamikia mwenzake kwa kuona kuwa hujaribu kumzibia mwingine.

“Ingawa inafahamika kuwa kila mmoja baina yao huteuliwa na Rais, lakini kuna mambo mengi ya kiutendaji hulazimika kupata Baraka za kila upande na mojawapo ni masuala ya baadhi ya safari za kikazi…hii pia ni sababu kubwa kwa sababu kuna tuhuma za kubaniana (kuzuia) fursa za baadhi ya safari hizo muhimu kwa kila mmoja,” chanzo kilidai.

“Lakini wawili hao (AG na DPP) sasa hawana namna nyingine isipokuwa kujirudi na kupata suluhu baina yao. Vinginevyo, kama wasipojirekebisha, ni wazi kwamba Rais Magufuli atakosa namna ya kuwavumilia na badala yake atawatumbua ili kuondoa mvutano usiokuwa na faida kwa taifa,” chanzo kingine kutoka ndani ya Wizara ya Sheria na Katiba kiliiambia Nipashe.

Hadi kufikia jana jioni, Nipashe haikuweza kuthibitisha kutoka kwenye vyanzo vingine huru kuhusiana na madai kuwa ubishani wa vyeo na ‘kubaniana’ safari ni miongoni mwa sababu za kuibuka kwa mvutano mkali uliomlazimu Rais kuuzungumzia katika hotuba yake ‘Siku ya Sheria’ juzi.

AG Masaju hakupatikana jana baada ya simu yake ya mkononi kuita mara kadhaa bila kupokewa, sawa na DPP ambaye pia hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

WABUNGE WANENA

Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na suala la mvutano baina ya DPP na AG lililowekwa wazi na Rais Magufuli juzi, Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria, Tundu Lissu, alisema kuna uwezekano mkubwa kuwa mgogoro huo unatokana na muingiliano wa majukumu kati yao.

Lissu ambaye pia ndiye Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, alisema kuwa katika katiba ya nchi, imeelezwa wazi kwamba DPP atatekeleza majukumu yake bila kuingiliwa na mamlaka yoyote na pia AG ni mshauri mkuu wa serikali kwenye mambo ya sheria.

Kwa sababu hiyo, Lissu alisema ni kuwa yeyote akiingilia majukumu ya mwenzake ndipo mgogoro huweza kutokea.

Alisema kwa anavyoona, kam Rais ambaye ndiye mteule wa wawili hao ataona kuwa wanagombana, ni vyema akachukua hatua kwa kumuondoa mmojawapo katika nafasi yake au wote wawili ili ateue watu watakaofanya kazi bila kuvutana.

Kwa upande wake, Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Katiba, alisema yeye hakuwahi kusikia kuwa AG na DPP wana mgogoro baina yao hadi juzi Rais alipoamua kuwapasha wawili hao kwa maslahi ya taifa.

Hata hivyo, Mchengerwa alisema DPP na AG hawapaswi kuwa na mvutano wowote kati yao kwa sababu madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwa Tanzania na Watanzania.

Alisema kadri anavyofahamu, AG ndiyo kiongozi wa Serikali katika masuala ya kisheria na DPP amepewa madaraka yake kwa mujibu wa sheria pia na hata katiba ya nchi inamtambua.

Mchengerwa alisema kwa kutambua umuhimu wa majukumu ya kila mmoja kati ya AG na DPP, anaona Rais Magufuli alifanya jambo sahihi la kuwataka wawili hao wamalize tofauti zao kwa sababu kinyume chake ni tatizo kwa taifa.

Akitolea mfano, Mchengerwa alisema mgogoro wa wawili hao unaweza kuathiri mfumo wa sheria kwa sababu kwa sababu DPP kazi yake ni kusimamia makosa yote ya jinai na katika usimamizi wa makosa hayo, yapo mambo mengi yanaweza kujitokeza katika masuala ya mashahidi na bajeti.

“Sasa tunapoona kuna mgongano kati yao, maana yake kuna uwezekano ukaja kwenye masuala ya kibajeti au masuala ya kimamlaka… labda huyu anajiona yupo juu ya huyu, kwa hiyo inawezekana mgongano kati yao ukasababisha madhara makubwa ya sheria,” alisema Mchengerwa na kuongeza:

“Ofisi hizi lazima zifanye kazi kwa pamoja kwa mustakabali wa utoaji haki. Si jukumu tu la DPP kumfikisha mtu mahakamani bali ni kuhakikisha vilevile kuwa haki inatendeka kwa sababu yeye anafikisha mahakamani, lakini kipo chombo kinachosimamia haki,” alisema Mbunge huyo.

Aidha, Mchengerwa alisema hatari nyingine pale AG na DPP wasipoelewana ni pamoja na uwezekano wa AG kuathiri mwenendo wa kesi akiamua kwa sababu ana uwezo wa kumuondoa mwendesha mashtaka yeyote anayewakilisha kesi ya Jamhuri ambaye kimsingi hutoka kwa DPP kwa sababu naye (DPP) yupo chini ya ofisi ya AG.

“Hata fungu la bajeti la DPP lipo chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Msaidizi (Naibu AG). Kwa hiyo inamaanisha kuwa fungu lipo katika Ofisi ya AG na hivyo ni rahisi kukwamisha kesi ikiwa ugomvi wao utakuwa mkubwa na kukosa suluhu,” alisema mwenyekiti huyo wa Kamati ya Katiba na Sheria.

No comments :

Post a Comment