Said Ali Mbarouk
Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kinaamini kuwa kiliporwa ushindi wake kwenye uchaguzi wa Oktoba 2015 visiwani Zanzibar, kimeilaani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kile kinachosema ni ubaguzi wenye misingi ya Uunguja na Upemba na kuwakomoa wale waliokikosesha ushindi Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi huo, ambao baadaye ulifutwa kinyume cha sheria na taratibu.
Akizungumzia kupitishwa kwa bajeti ya shilingi bilioni 26 kwa ajili ya wizara inayohusika na vikosi vya SMZ na tawala za mikoa na Baraza la Wawakilishi, msemaji wa CUF kwa wizara hiyo, Said Ali Mbarouk, amesema kisiwa cha Pemba kimetengewa shilingi bilioni 1.068 tu, ambayo ni sawa na asilimia 4.1 ya fedha zote zilizoidhinishwa kwa wizara hiyo, jambo ambalo ameliita ni “upitishwaji wa bajeti yenye misingi ya kibaguzi na upendeleo baina ya Unguja na Pemba kwa kutumia muhuri wa Baraza la Wawakillishi.”
Baraza la Wawakilishi linajumuisha wajumbe wa kuchaguliwa kutoka CCM pekee na wajumbe wengine watatu wa kuteuliwa kutoka vyama vya ADC, TADEA na Chama cha Wakulima na ambao wote ni sehemu ya baraza la mawaziri la Dk. Shein.
“Ni wazi kuwa ubaguzi huu unaofanywa na watawala wa CCM waliojiweka madarakani kwa mtutu wa bunduki umelenga kuendeleza mpango mkakati wa kuwakomoa wazanzibari kufuatia uamuzi wao wa kukikataa chama hicho katika uchaguzi Mkuu halali wa 25 Oktoba, 2015 na kuamua kuichagua CUF kwa kumpa ridhaa Maalim Seif Sharif Hamad.” Inasema sehemu ya taarifa ya msemaji huyo iliyosambazwa leo kwa vyombo vya habari.
Tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuchukuwa hatua ya peke yake ya kuufuta uchaguzi huo hapo tarehe 28 Oktoba 2015, siku tatu baada ya wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi vituoni kuamua juu ya uongozi wa nchi yao, CUF imekuwa kwenye mgogoro mkubwa na CCM na serikali zake kwa kukataa kuutambua uamuzi huo, na hivyo kutokuitambua serikali inayoongozwa sasa na Dk. Shein.
/Zanzibar Daima
No comments :
Post a Comment