Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa kwenye Viwanja vya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
`Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Taasisi zote zenye usimamizi kuhakikisha zinasimamia vyema jukumu lao la kutumia nafasi zao kuongeza juhudi katika kuimarisha misingi ya Utawala Bora, Uwazi, Uadilifu na Uwajibikaji.
Makamu wa Rais aliyasema hayo leo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliofanyika kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Dodoma.
Makamu wa Rais alisema Vita dhidi ya ukiukwaji wa Maadili haiwezi kupiganwa na Serikali peke yake, “Ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu na maovu mengine vinatokomezwa”
Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kisera na kisheria ambayo itahakikisha vijana wanakuzwa kimaadili kwani hakuna Taifa Duniani linaweza kupata maendeleo bila kuwa na utamaduni unaozingatia maadili alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa ili kujenga Utawala Bora ni lazima kuweka uwiano wa yanayofanyika na serikali kuu hadi serikali ya mitaa nchi nzima.Serikali ilizindua Rasmi mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Tatu (NACSAP III) Desemba 2016.
Makamu wa Rais alisema kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa baadhi ya Ofisi za Serikali, Serikali imeamua kufuatilia uhalali wa vyeti vya Watumishi, Idadi halali ya Watumishi wa Umma na ulipaji wa Mishahara Hewa na kusisitiza zoezi ili litakuwa endelevu.
Mwisho, Makamu wa Rais aliwaeleza wananchi na Watumishi wa Umma kwa ujumla kuwa Maadili ni nguzo muhimu katika maendeleo ya nchi yetu. “Ni imani yangu kuwa Wakuu wa Taasisi hizi kuwa mtahakikisha misingi ya haki za binadamu, utawala bora na viwango vya Maadili ya Viongozi wa Umma vinasimamiwa ipasavyo ili kuimarisha nidhamu ya Maafisa na Watumishi wa Umma”.
Kuimarishwa na kudumishwa kwa nidhamu ya utendaji, huduma zitolewazo Serikalini, Ukusanyaji wa mapato na matumizi bora ya fedha za Serikali kutaleta mafanikio katika kuelekea uchumi wa kati.
No comments :
Post a Comment