Top Leaderboard Advert

Patreon

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, February 15, 2018

Mchongo e-passport!


*JAMHURI lataja vigogo walioshiriki' kufanikisha' dili
*Wengi ni maofisa waandamizi Ofisi ya Rais Zanzibar
*Kampuni iliyoharibu vitambulisho vya taifa yapewa 'shavu'
*Kenya waliokoa mabilioni, Tanzania kutumbukia shimoni.

Na Mwandishi Wetu.
Siri nzito zimezidi kuanikwa jinsi wakubwa walivyoshiriki katika kuhamisha zabuni ya e-passport kutoka kwa kampuni iliyokuwa na teknolojia, uzoefu na bei nafuu kwenda kwa kampuni inayonyofoa mabilioni kutoka kwa walipakodi, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Wakubwa wametumia ujanja wa hali ya juu kupenyeza bei wanayoitaka wao kwa kutumia mfumo sawa na kununua baiskeli mpya, lakini baadaye ukamwambia mtoa fedha kuwa unahitaji kununua usukani, mnyororo, matairi, kiti na vitu vingine kama uchunguzi huu uliofanywa na JAMHURI unavyobainisha kwa uwazi katika habari ya leo jinsi taifa linavyopigwa fedha ndefu kupitia mradi huu wa e-passport.

Wiki iliyopita gazeti la JAMHURI lilichapisha habari za uchunguzi kuhusu nchi kuelekea kupoteza wastani wa Sh bilioni 90 kutokana na ujanja uliofanywa na wakubwa wachache katika mkataba wa kuchapisha hati za kusafiria za kielektroniki (e-passport), na leo JAMHURI linakuletea sehemu ya pili ya habari hii ya uchunguzi inayotisha.

Baada ya kuchapisha habari hiyo, kumekuwepo jitihada za Idara ya Uhamiaji kujaribu ‘kuweka’ mambo sawa. Pamoja na jitihada hizo zinazofanywa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, bado ufafanuzi wake unaacha maswali mengi zaidi kuliko majibu. Wapo wanaosema utetezi uliotolewa na Dk. Makakala ulilenga kuwaokoa walioiingiza nchi katika hatari ya kupoteza zaidi ya Sh bilioni 90 kiujanja.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba, mchongo huu unahusisha Idara ya Uhamiaji na wakubwa wachache kutoka Ofisi ya Rais na Zanzibar, waliomtafuta mzabuni wa e-passportkwa siri kubwa.

JAMHURI limebaini kuwa watendaji hao kutoka ofisi ya Rais waliopewa dhamana ya kusimamia suala la e-passport, bila kumwogopa hata Rais John Magufuli wamefanya uamuzi mgumu unaoitia nchi hasara. Watu hawa wamekuwa na mawasiliano ya karibu na Mkurugenzi wa Mauzo wa HID Global, Joby Mathews, ambaye kampuni anayoiwakilisha ndiyo ilipata zabuni ya kutengeneza hati hizo.

Dili ilivyopigwa

JAMHURI limefahamishwa kwamba kumekuwepo na mawasiliano ya karibu kati ya viungo muhimu waliofanikisha kuiumiza nchi kwa kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 90. Mawasiliano hayo yamekuwa yakifanywa na mtu mahsusi ambaye anafanya kazi katika Ofisi ya Rais, huku kituo chake cha kazi kikiwa Zanzibar.

Mtu huyo ambaye amefahamika kwa majina matatu, Mohammed Khamis Abdallah, amekuwa akiwasiliana na mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya mifumo ya kompyuta (SoftNet), Nuru Othman. Othman, taarifa zinaonesha ni ndugu wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Rashid Othman.

Kampuni ya Softnet ndiye mzabuni wa ndani anayeshirikiana na HID Global iliyopewa zabuni hii ya e-passport na wakubwa kwa sasa.

Nuru Othman, pia alikuwa mkandarasi wa ndani katika mradi wa vitambulisho vya taifa uliokuwa unatekelezwa na kampuni ya IRIS kutoka nchini Malaysia, kampuni ambayo hata hivyo haikumaliza kazi hiyo kwa wakati, hata kabla ya Rais John Magufuli kuingilia kati na kuhoji ubora wa vitambulisho vya Taifa, akijaribu kuvilinganisha na kadi ya kupigia kura.

Uchunguzi wa JAMHURI, umebaini kwamba kumekuwepo pia na mawasiliano baina ya Nuru na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Yahya Simba, huku mawasiliano hayo yakitamalaki kwa wafanyakazi kadhaa wenye vyeo vya juu katika Idara ya Uhamiaji.

JAMHURI, limebaini kati ya Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu, kuhusu suala la e-passport, Nuru amewasiliana na Mohamed Awesu, Mahfoudh Nassoro na Bashir Mang’enya, wote wakiwa ni wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji.

Sehemu kubwa ya maofisa waliokuwa wakiwasiliana na Nuru Othman, ni wafanyakazi katika kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika Idara ya Uhamiaji. Mradi wa e-passport kwa kiwango kikubwa ulikuwa unawahitaji watalaam wa Tehama kuweka ‘mambo sawa’.

Septemba mwaka jana, kumekuwa na mawasiliano makubwa baina ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na wafuatao, Mohamed Khamis Abdallah, ambaye anafanya kazi Zanzibar, huku taarifa nyingine zikionesha anafanya kazi Ofisi ya Rais. Taarifa hiyo inaonesha katika mwezi huo huo kumekuwepo na mawasiliano ya karibu mno na mtu anayeitwa Joachim Nyingo, anayetajwa kufanya kazi Ofisi ya Rais pia.

Gharama za Mradi

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, mradi huo wa kutengeneza e-passport umeligharimu taifa dola za Marekani milioni 57.8 (zaidi ya Sh bilioni 127.68) huku kukiwa na mtazamo kwamba gharama hizo zinahusisha mifumo mingine ya kimtandao, kama pasipoti za kielektroniki (e-passport), viza za kielektroniki (e-visa), vibali vya ukaazi vya kielektroniki (e-permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektroniki (e-border management).

Akizungumza na JAMHURI mtaalam wa mifumo ya kompyuta, Michael Doyo, amesema ni dhahiri kwamba mfumo huo wa e-passport ndio wenye kubeba dhima nzima ya mifumo yote kwenda kielektroniki, huku akifananisha mfumo huo na ule wa baiskeli.

“Unajua baiskeli ili iitwe baiskeli inahitaji kuwa na muunganiko wa vifaa kadhaa, kama vile magurudumu, mnyororo, usukani, pedeli, spoko, mipira, kiti, nanga,‘fluwelo’ na vingine. Hivyo ndivyo ulivyo mradi huo wa e-passport, kuna vifaa vinategemeana katika kutengeneza mfumo mzima wa kielektroniki na kuukamilisha.

“Hivyo hata mradi huu unaotekelezwa na idara ya uhamiaji unahitaji kuwa na ‘component’ zote hizo. Uwekezaji wa hiyo e-passport ndio huo utatumika hata kuwezesha hayo mengine yote, maana kinachohitajika hapo ni mfumo madhubuti wa kuhakikisha mengine yanafanyika,” amesema Doyo.

Mtalaam huyo wa masuala ya mifumo ya kompyuta, ameliambia JAMHURI, ni rahisi zaidi kwa mtu asiyekuwa na ufahamu wa masuala la Tehama kudanganywa katika mambo ‘technical’, huku akisisitiza kwamba ni rahisi sana kuwezesha mambo yote kufanyika baada ya kuweka mifumo ya kompyuta itakayowezesha e-passport.

“Ni rahisi sana watu kusema kwamba wamegharimia mabilioni ya shilingi katika kuweka mfumo ambao utawezesha kufanyika kwa masuala yote yanayotajwa na watu wa idara ya uhamiaji, lakini ukweli unabaki kuwa unapopatana kuweka mfumo kama huo utahusisha ‘component’ zote ndio maana hutasikia tena e-visa na e-border management vikishughulikiwa na kampuni nyingine,” amesema Doyo.

Kwa mantiki hiyo, mzabuni yeyote anayesaini mkataba wa kuchapisha e-passport anakuwa moja kwa moja ameingia mkataba wa kubadili mfumo wote wa uhamiaji kuwa wa kielektroniki. “Sasa nchi hii watu wanadanganywa kama nini. Hivi wewe unaniambia leo unakuwa na hati ya kielektroniki alafu unasema huna mfumo wa e-visa au e-boarder si ni sawa na kuwa na baiskeli isiyo na usukani?

“Wapigaji wanaweka mbwembwe kutenga maneno haya, lakini uhalisia ukiingia e-passport ndo umemaliza mambo yote hakuna tena kununua hivyo vingine maana na ni software moja tu unayofunga ikafanya mambo yote hayo,” amesema mtaalam mwingine.

Gharama ya e-passport nchi jirani

Uchunguzi wa gazeti la JAMHURI, katika nchi nyingine zilizomo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), pamoja na zile zilizoko ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), umebaini kwamba mataifa hayo yalipatana vizuri kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi zao. Uchunguzi huo umezihusisha nchi za Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Msumbiji pamoja na Malawi kwa uchache.

Taarifa ambazo tumezipata kutoka nchini Kenya, ambao wametekeleza mradi kama huu wa e-passport, walimpata mzabuni kwa gharama ya dola za Marekani milioni 21, ambazo ni sawa na Sh bilioni 47.04. Pasipoti ya Kenya yenye kurasa 32, inauzwa kwa Ksh 4550 (sawa na Sh 81,900 za Tanzania).

Serikali ya Kenya, imesaini mkataba wa kutengeneza pasipoti 600,00, ambazo zikiuzwa zote kwa wananchi wake, Serikali hiyo itakusanya kiasi cha Ksh bilioni 27.3, (ambazo ni sawa na fedha za Tanzania Sh bilioni 49.14). Serikali ya Kenya ikiuzwa pasipoti zake kwa wananchi itarudisha gharama zilizotumika kwenye mradi huo.

Hapa Tanzania, ambako mamlaka zimeingia mkataba wa kuchapa pasipoti 400,000 na kutangaza kwamba pasipoti hizo zitapatikana kwa Sh 150,000 kwa kila kitabu, endapo zitauzwa zote kwa mkupuo, Serikali itaweza kukusanya kiasi cha Sh bilioni 60, huku ikipoteza kiasi cha Sh bilioni 67.68.

Ikiwa nchi inataka kurejesha fedha zitakazotumika kumlipa mzabuni wa kuchapa hati hizi, kama walivyofanya Kenya, japo bila faida pasipoti moja ya kusafiria ya Tanzania, inapaswa kuuzwa kwa Sh 319,200. Vinginevyo nchi itapata hasara iliyotajwa hapo juu.

Hasara hii inaweza kuwa kubwa zaidi, kwani Kenya kwa kuitoa hati yao kwa Sh 81,900 za Tanzania, zikiuzwa hati zote 600,000 walizochapisha, watapata salio (faida) ya Sh bilioni 2.1 ambazo ni sawa na Ksh milioni 116.66. Fedha hizi zinagharimia posho, mishahara na huduma nyingine kwa maofisa wanaotoa huduma za hati ya kusafiria nchini humo. Kwa Tanzania itabidi litengwe fungu la ziada kutoka hazina litakaloongeza kiwango cha hasara.

Mfano huu wa Kenya unafanana moja kwa moja na nchi nyingine zilizotajwa hapo juu. Gharama za utengenezaji wa passport zao kwa kutumia kampuni waliyoinyima dhamana hapa nchini ya DeLaRue ya Uingereza ziko chini ikilinganishwa na dola milioni 57 za hapa kwetu. Kampuni ya DeLaRue ilikuwa tayari kuchapa e-passport za Tanzania kwa gharama ya dola milioni 16.

Wakati anazindua hati hizo wiki mbili zilizopita, Rais John Magufuli alisema nchi imefanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambayo yangefunjwa na ‘wajanja’ wachache kupitia mkataba wa awali ambao uchapishaji wa e-passport walitaka uligharimu taifa Sh bilioni 400.

Rais Magufuli amevisifia vyombo nyeti vya dola kuwa vimeweza kushusha gharama za mkataba huo kufikia dola milioni 57. Dola milioni 57 za Marekani ni sawa na Sh bilioni 127.68 kwa bei ya kubadili dola moja Sh 2,240 hadi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa mantiki hiyo, kauli ya Rais Magufuli inamaanisha kuwa nchi kwa mkataba huu imeokoa Sh bilioni 272.32, kumbe bado imepigwa zaidi ya Sh bilioni 90.

Sifa za kuchapa e-passport

Masharti ya kampuni kupewa zabuni ya kuchapa hati za kusafiria za kielektroniki duniani, ambayo Tanzania imeyachukua yote kama sehemu ya zabuni hii, yanaitaka kampuni kuwa imewahi kufanya kazi hii ya kuchapisha hati za kielektorini kwa mikataba isiyopungua mitano.

Kwa ajili ya usalama, kampuni ya kuchapisha hati za kusafiria za kielektroniki inapaswa kuwa na mitambo yake, majengo yake, teknolojia ya kuchapa hati hizo na kitengo cha usalama bila kuhusisha mtu wa kati (third part), lakini kampuni ya HID Global iliyopewa zabuni inashirikiana na kampuni ya Ireland kwani haina uzoefu unaotakiwa kimkataba.

Kuna vigezo tisa vya kupata zabuni ya aina hii kokote duniani, ambavyo ni:-

Mshindi wa zabuni anapaswa kuwa amewahi kuchapisha au yuko katika mchakato wa kuchapisha kama mkandarasi mkuu katika miradi mitano ya hati za kielektroniki. Katika miradi hiyo, anapaswa kuwa aliwahi kuchapisha hati za kusafiria milioni 1 au zaidi kwa kila mkataba kwa mwaka, ambayo mzabuni amekuwa mkandarasi mkuu.
Kipaumbele kinatolewa kwa mkandarasi anayeonyesha katika zabuni yake kuwa ataweka masuala mengi ya kiusalama katika hati ya kusafiria husika kuliko makandarasi wenzake.
Mkandarasi anapaswa kuthibitisha kwa kutoa rejea angalau 10 za kazi za hati za kusafiria alizowahi kuzifanya, zikiwa na mfumo wa taarifa za siri katika ukurasa wa taarifa. Kati ya hati hizo 10, tano ya hati hizo [za nchi mbalimbali] zinapaswa kuwa za kielektroniki.
Mkandarasi anapaswa kuthibitisha kwa kutoa rejea inayoonyesha uwezo wake kuwa alipata kuyatengenezea mataifa yapatayo matano hati za kieleketroniki na kuyahamisha kutoka mfumo wa hati tulionao sasa.
Mkandarasi anapaswa kuonyesha uzoefu wa kurithi mkataba wa kuchapisha hati za kielektroniki katikati ya mradi unaoendelea na akaumalizia kwa ufanisi mkubwa.
Mkandarasi anapaswa kuthibitisha kuwa amewahi kutoa suluhisho la hati za kielektroniki zinazojumuisha kutia saini ya kieleketroniki.
Mkandarasi anapaswa kuwa na rejea tatu za nchi alikochapisha hati za kielektroniki zenye viwango na ubora wa kimataifa.
Mkandarasi anapaswa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa za miaka mitano zenye kuonyesha kuwa mzunguko wa biashara yake unafikia dola milioni 100 za Marekani kwa mwaka, na;
Mkandarasi anapaswa kuonyesha ufahamu juu ya mfumo wa hati za kusafiria za kielektroniki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kampuni ya HID Global iliyopewa kazi hii haijawahi yenyewe kama kampuni kuchapisha hati hata moja ya kielektroniki peke yake kwani kazi yake ya msingi ni kuuza plastic na polycarbonate cards (vitambulisho na kadi za kufungulia milango).

Kutokana na kampuni hii kutokuwa na ujuzi na vifaa vya kutengeneza hati za kusafiria za kielektroniki, imewahi mara moja kwa ubia na kampuni ya DLRS ya nchini Ireland kutengeneza hati ya kielektroniki ya Ireland na sasa wameshirikiana nayo tena kuomba kutengeneza hati ya Tanzania. Hata kwenye mtandao wao imeutangazia ulimwengu ukweli huu.

JAMHURI limebaini kuwa kuna kampuni tatu kubwa na zenye kuaminika duniani zinazofanya kazi ya kuchapisha hati za kielektroniki ambazo ni DeLaRue ya Uingereza, Muhlbaur ya Ujerumani na Gemalto ya Uholanzi.

Kampuni iliyonyimwa kazi inazofanya

Kampuni ya DeLaRue iliyonyimwa zabuni ya kuchapisha hati za kielektroniki kwa gharama ya dola milioni 16 za Marekani kwa miaka minane, inachapisha hati za kielektroniki.

Kwa Bara la Afrika wanachapisha hati za kusafiria za nchi za Angola (e-passport na mifumo), Ghana, Mali (e-passport na mifumo), Swaziland, Lesotho, Botswana (Vitambulisho vya Taifa), Rwanda (Fedha, e-passport na mifumo, vitambulisho vya taifa na huduma za fedha).

Nchi nyingine ni Somalia (fedha na huduma za fedha), Kenya (fedha, e-passport na huduma za fedha), Sudan (stempu za ushuru), Mauritania (e-passport), Cameroon (vitambulisho vya taifa na vya mpigakura) na Guinea Bissau (passport na fedha).

Mchezo ulivyochezwa

Uchunguzi uliofanyika tangu Mei, mwaka jana, umebaini kwamba gharama halisi za mradi ambao umezinduliwa na Rais Magufuli wiki iliyopita hazikutakiwa kuzidi dola milioni 16 za Marekani, karibu Sh bilioni 35.84. Bei ya soko ya kubadili pesa Jumamosi iliyopita ilikuwa Sh 2,240 kwa dola moja ya Marekani.

JAMHURI, limebaini kuwa mchakato wa kumpata mzabuni wa kufanya mradi huo wa Uhamiaji Mtandao, ambao baadaye ungeelekea kwenye kutoa hati ya kusafiria ya kielektroniki (e-passport) ulianza kugubikwa na ‘ushawishi’ wenye harufu ya rushwa ukiwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, na ndipo mabosi wa wizara hiyo walimwomba Rais Magufuli kuingilia kati.

Vyanzo vyetu vimesema miongoni mwa mambo yaliyochangia kuhamishwa kwa zabuni ya kuchapa e-passport kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ni pamoja na Rais Magufuli, kutoridhishwa na mchakato wa zabuni pale wizarani. Sababu nyingine ilikuwa ni kutotaka kufanya zabuni ya wazi maana jambo lenyewe limebeba maslahi mapana ya taifa.

Chanzo chetu cha habari kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kimeliambia JAMHURI kwamba kumekuwepo usiri mkubwa katika mchakato wa kupatikana mzabuni wa kufanya kazi hiyo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa kampuni iliyopewa kazi ya kuchapa e-passport haikuwa miongoni mwa kampuni zilizoomba kazi hiyo awali kupitia wizarani hapo, kabla ya kazi hii kuhamishwa Ofisi ya Rais ilikoaminika kuwa wakubwa wataisimamia kwa uadilifu wa hali ya juu.

“Kiutaratibu hapa tulikuwa tumeshafanya [kazi] mpaka kwenye ‘pre-qualification’ lakini utashangaa kwamba makampuni yote ‘reputable’ yameachwa na wamekwenda kumchukua ‘component supplier’. Kuna baadhi ya masharti tuliyaweka kwa wazabuni, lakini nadhani yamekiukwa ama yalikuwa ya hovyo ndiyo maana hayakuzingatiwa kabisa katika kumpata mzabuni.

“Nadhani ni suala la muda tu, kila kitu kitakuwa wazi na wananchi watafahamu namna kodi zao zinavyochezewa… mpaka napata hisia kwamba labda lingeshughulikiwa hapa wizarani kwetu labda mambo yangekuwa tofauti sana,” kimesema chanzo chetu.

Nyendo zinazotiliwa shaka

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba kumekuwepo na nyendo zinazotiliwa shaka, ambazo zimekuwa zikiwahusisha baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali kutoka ndani ya Idara ya Uhamiaji na Ofisi ya Rais.

JAMHURI limebaini kuwa Novemba 27, mwaka jana viongozi watano kutoka Uhamiaji, walifanya mkutano wa siri katika chumba binafsi Na. 303 cha Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kati ya saa 08:30 alasiri hadi 11:00 jioni, wakiwa na mmoja wa mawakala wa kampuni ya HID Global iliyoshinda zabuni na kupewa kazi ya kuchapisha e-passport kwa kasi ya kutisha.

Kitendo hicho cha kujifungia chumbani watu zaidi ya watano, kinaleta maswali mengi, pengine hata kuikumbusha nchi machungu ya mmoja wa waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kwenda kusaini mkataba wa kuchimba dhahabu ya Buzwagi katika chumba cha Hotel ya Churchill nchini Uingereza mwaka 2007.

Desturi za taifa zinaliona jambo hilo lina ukakasi, hasa ikizingatiwa kwamba kama ni mkutano halali usiokuwa na hila wala mawaa ndani yake, kwanini ukafanyike chumbani wakati kumbi za mikutano kwenye hoteli na ofisi za Serikali zipo.

Taarifa zinaonesha chumba hicho kilikuwa kimekodiwa na raia wa Kenya, Henry Mkuzi, ambaye naye alishiriki kikao hicho kwa muda wa saa tatu.

“Ndugu mwandishi nadhani hapo hata kama ni mtoto mdogo mwenye ufahamu mdogo anaweza kunusa harufu isiyopendeza,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limezungumza na Mkuzi akiwa nchini Kenya, ambaye ameng’aka kwa nini aulizwe swali hilo, akihoji kuna kosa gani yeye kufanya mkutano na watu alioingia nao mkataba, na akataka asipigiwe simu tena.

“Kwani kuna shida gani mimi kukutana na watu ambao tuna mkataba nao hotelini? Mimi sitakiwi kuzungumza na wewe hilo, tafadhali fuata utaratibu sahihi wa kuzungumza na HID,” amesema na ameongeza kuwa JAMHURI likipenda likawaulize watu wa Uhamiaji juu ya suala hili.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (CHADEMA), wiki iliyopita alimtaja aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), Dk. Modestus Kipilimba kuwa alisaini mkataba wa hovyo ulioongeza gharama ya kupata hati za kielektroniki.

Amesema Mkurugenzi huyo amekiuka maelekezo ya Rais Magufuli ya kupata mzabuni mwenye bei nafuu na hivyo amelitia taifa hasara ya mabilioni ya fedha.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, amejibu hoja hiyo bungeni kwa kusema: “Naomba niwaambie kwamba mwanzoni upembuzi uliokuwa unafanyika kabla Serikali haijaingia kati, ukubwa wa mradi ni uleule na fedha zilizotakiwa kutumika ni takribani dola za Marekani milioni 192.

“Kwa maana hiyo kama ambavyo nimesema tangu mwanzo, na ninamjua babu yangu [mtani wake] Mheshimiwa Heche, tangu akiwa kule Bavicha [Baraza la Vijana Chadema] haka ka wimbo ka ufisadi kalikuwa kananoga sana. Kama kuna mtu anadhani nasema uongo atasubiri sana,” amesema Dk. Nchemba.

Jitihada za kumpata Dk. Kipilimba, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, hazikuzaa matunda, ila Gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 4718 la Februari 3, 2018, Jumamosi, limemkariri akisema:

“Nilipelekwa NIDA Februari 25, nikaondoka pale Agosti 24. Kwa miezi sita niliyokuwa pale kwanza ofisi haikuwa na fedha. Sikuwahi kununua wala kuagiza chochote…sijasaini mkataba wowote ndani ya NIDA. Lakini nimenyamaza. Nimeshangaa sana, vitu vingi wamepindua.

“I said nothing (sikusema chochote), wakati mwingine nilikuwa natoa hela yangu mfukoni kununua stationeries. Siku niliyoondoka mimi, kesho yake hela zikaingia kutoka kwa donors [wafadhili] na Serikali Kuu.

“Mimi nimerekebisha tu, hasa tatizo la ikama. Kama mtakumbuka kulikuwa na mashine 150 lakini watu wa kufanya kazi walikuwa 840. Nikaona hata tukifanya shift tatu wanaohitajika ni watu 450 tu, nikapunguza.

“Kingine nilichofanya ni ku-introduce [kuanzisha], kitambulisho chenye signature (saini). To be honest (kuwa mkweli) ofisi haikuwa na fedha. Sikununua chochote, maana sikuwa na hela,” amesisitiza Dk. Kipilimba.

Kuhusu e-passport, Dk. Kipilimba amesema madai ya mbunge Heche yamelenga eneo moja, hakubainisha kwamba kilichozinduliwa ni e-immigration.

“Eti kile kitabu peke yake ndiyo ameona azungumzie. Kuna e-boarder, e permit, e-passport, e-visa, yaani ndugu zangu hao bwana, nyie ndio mnaojuana nao vizuri,” amesema.

Rais Magufuli anena

Wiki iliyopita, Rais Magufuli alizindua mfumo wa Uhamiaji Mtandao (e-Immigration) ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.

Uzinduzi wa mfumo huo ulifanyika katika Ofisi Kuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.

Wengine ni Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid; Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson; Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Dk. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Kabla ya kuzindua mfumo wa Uhamiaji Mtandao, Rais Magufuli alikagua teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielektronikia (e-Passport) ambayo pia ilianza kutolewa siku hiyo hiyo.

Pasipoti mpya za kielektroniki pia zimetolewa kwa viongozi wengine wakuu wa Serikali, Bunge na Mahakama waliohudhuria uzinduzi huo.

Rais Magufuli akampongeza Dk. Nchemba na Idara ya Uhamiaji kwa kufanikisha mradi wa kuweka mfumo wa Uhamiaji Mtandao na kuanza kutoa hati mpya ya kielektroniki kwa gharama nafuu ya ya dola milioni 57 (Sh bilioni 127.2) ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Sh bilioni 400.

“Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Sh bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli akaahidi kutoa Sh bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya Idara ya Uhamiaji mjini Dodoma.

“Kamishna Jenerali Dk. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi kule Dodoma na leo nitawapa fedha nyingine Sh bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu. Nyinyi endeleeni kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Mapema, akitoa taarifa ya mfumo wa Uhamiaji Mtandao, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Makakala alisema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji.

Alisema kupitia mfumo huo Idara ya Uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektroniki (e-passport), viza za kielektroniki (e-visa), vibali vya ukaazi vya kielektroniki (e-permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektroniki (e-border management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu; pamoja na kutoa pasipoti ya kielektroniki ya Afrika Mashariki ya Tanzania.2 comments :

 1. Pole Rais wangu Magufuli!

  ReplyDelete
  Replies
  1. Nampokelea Rais wetu hizo pole.
   Nchi nzima ilikuwa imeoza sasa yeye kwa miaka miwili atamaliza kila kitu?

   Delete