DOTTO BULENDU UMENIKOSEA: SIJALILIA FADHILA, NADAI HAKI!!!!
THE FLAMBOYANT TUNDU LISSU DURING HIS HEYDAY BEFORE
BEING GUNNED DOWN BY THE EVIL FORCES OF DARKNESS IN TANZANIA!
BEING GUNNED DOWN BY THE EVIL FORCES OF DARKNESS IN TANZANIA!
Kaka Dotto Bulendu salaam.
Nimesoma makala 'Kosa la Tundu Lissu ni nini?' mara mbili. Baada ya kuisoma mara ya pili, nimelazimika kurejea tena mahojiano yetu ya Nairobi Hospital ya mwaka jana. Nilitaka kujiridhisha kama ulichokiandika kinaendana na makala yako hii.
Ninasikitika kusema kwamba hujanitendea haki mimi mwenyewe, na hujawatendea haki wasomaji wako. Na nina wasi wasi kama umeitendea haki taaluma yako ya uandishi habari. Naomba kufafanua.
TUNDU LISSU AKIWA HOSPITALINI KENYA BAADA YA KUPIGWA RISASI MJINI DODOMA, TANZANIA, TAREHE 7 SEPTEMBER, 2017!
Umetumia maneno ambayo nguzo yake ni neno 'msaada' mara 12 katika makala yako yenye aya 18. Yaani, kwa kila aya tatu umetumia neno hilo kwenye aya mbili.
Hoja yako kubwa ni kwa nini 'sijasaidiwa' kwenye matibabu yangu na Serikali na/au Bunge.
Umeonyesha kupata fadhaa na masikitiko makubwa kwamba Serikali na/au Bunge wamekataa kutoa 'msaada' huo kwangu.
Ombi lako kuu kwa Serikali na/au Bunge ni kwamba 'nisaidiwe' gharama za matibabu hayo.
Aidha, unaona uchungu kwamba mimi, ndugu zangu na familia yangu tunalia ili Bunge na Serikali 'zirejeshe moyo nyuma' na 'zinisaidie' katika matibabu yangu, lakini kilio hicho hakijasikilizwa.
Kaka Dotto mimi sina shaka na wema wa nia yako. Ungependa nipate matibabu ya majeraha na maumivu makubwa niliyosababishiwa na wauaji wa kutumwa walionishambulia na kunijeruhi vibaya siku ile ya Septemba 7, 2017. Hili ni jambo jema na nakushukuru sana.
Hata hivyo, kaka Dotto, nadhani unafahamu ule msemo wa Waingereza 'the road to hell is paved with good intentions', yaani, 'njia ya jehanamu/kuzimu imepambwa na nia njema.'
Nina wasi wasi kwamba nia yako njema ya mimi kupatiwa matibabu inaweza ikasababisha mimi na/au watu wengine waumizwe zaidi.
Hii ni kwa sababu, badala ya kuzungumzia wajibu, unazungumzia fadhila. Badala ya kudai nitendewe haki, unataka nionewe huruma. Badala ya kutanguliza sheria za nchi yetu, umejificha nyuma ya maandiko matakatifu.
Kaka Dotto Serikali yetu haina, na Bunge la Tanzania halina, dini. Nchi yetu haiongozwi na misahafu. Bali nchi yetu inatakiwa kuongozwa kwa Katiba na Sheria na Kanuni au taratibu zenye nguvu ya sheria, kwa mlolongo huo.
Katiba ya nchi yetu haijaweka utaratibu wa matibabu ya Wabunge na stahili zao nyingine. Badala yake, Katiba imeelekeza kwamba utaratibu huo utawekwa katika sheria iliyotungwa na Bunge.
Mwaka 2008, Bunge letu lilitunga Sheria ya Uendeshaji wa Bunge. Sheria hiyo ndiyo iliyoweka utaratibu wa matibabu ya Wabunge na stahili zao nyingine.
Kifungu chake cha 24 kinasema 'matibabu ya Mbunge yatagharamiwa na Bunge ndani na nje ya Tanzania.' Huu ndio msingi pekee wa kisheria katika masuala ya matibabu ya Wabunge.
Kwa hiyo, katika masuala yote yanayohusu matibabu yangu na ya Wabunge wengine, waliopita na wajao, hapa ndio mahali pa kuanzia.
Hoja zozote zinazohusu mgogoro wa matibabu yangu, zinatakiwa kupimwa kwa kipimo kilichowekwa na Sheria hii.
Kwa mfano, Spika Ndugai na watu wake wamedai kwamba siwezi kutibiwa kwa gharama ya Bunge kwa sababu sikufuata 'utaratibu.' Na wewe umeyarudia maneno hayo, lakini bila kuuliza ni utaratibu gani huo ambao nilitakiwa kuufuata, huku nikiwa nimezirai kwa majeraha ya risasi niliyoyapata!!!
Kwa vile hujausema, mimi nitakueleza utaratibu ambao Spika Ndugai anadai sikuufuata.
Kwanza, Spika Ndugai anadai nilitakiwa kuomba ruhusa ya kwenda kutibiwa nje kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Baada ya hapo, Katibu Mkuu huyo alitakiwa kuteua jopo la madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambao, baada ya kunipima kwa kina, wangempelekea Katibu Mkuu taarifa na mapendekezo yao kwamba ninastahili kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Baada ya kupata mapendekezo hayo, Katibu Mkuu alitakiwa kupeleka maombi Ikulu ili kupata idhini ya Rais Magufuli ya pesa kutolewa kwa ajili ya matibabu yangu.
Hii, more or less, ndio kauli rasmi ya Bunge, iliyotolewa Bungeni na Spika Ndugai, na kwa maandishi kwa familia yangu.
Swali muhimu kuliko yote ulilotakiwa kuliuliza kwenye makala yako, lakini hukufanya hivyo, ni je, huu ndio utaratibu uliowekwa katika Sheria ya Uendeshaji wa Bunge???
Ulitakiwa kuhoji ni kifungu kipi cha Sheria hiyo kinachotaja maombi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, au jopo la madaktari wa Muhimbili au idhini ya Rais Magufuli katika masuala ya matibabu ya Wabunge.
Hukufanya hivyo. In fact, hujataja neno 'sheria' katika makala yako yote. Picha uliyojenga, kwa kufahamu au la, kwa makusudi ama kwa bahati mbaya, ni kwamba masuala ya matibabu ya Wabunge hayawekewa utaratibu wa kisheria.
Na kwa sababu hujafanya hivyo, athari mojawapo kubwa ya nia yako njema ni kuwasaidia wale wote ambao hawajatimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria, ama kwa makusudi ama kwa hofu au kwa mashinikizo, kujificha.
Badala ya kuwaumbua hadharani kwa kukiuka Sheria wanayopaswa kuiheshimu na kuitekeleza, umewapatia kichaka cha kujifichia, i.e. wanatakiwa wawe na huruma na upendo, warudishe mioyo yao nyuma na kunisaidia, etc., lakini sio wawe watiifu kwa Sheria za nchi yetu.
Badala ya kudai uwajibikaji, umeomba fadhila kwa niaba yangu. Badala ya kukemea utovu wa utiifu kwa sheria za nchi yetu, umepiga magoti kwenye altare ya 'ubinadamu.'
Unaitaka Serikali ya Magufuli na Bunge la Spika Ndugai linionee huruma kama Magufuli alivyofanya kwa Ruge Mutahaba, marehemu King Majuto au marehemu Sajuki. Ulitakiwa ujiulize kwanza je, utaratibu wa matibabu ya Wabunge unalingana na utaratibu wa matibabu ya hawa waliopatiwa msaada na Serikali???
Ungetaka kufahamu uongo na unafiki wa hawa wanaodai sikufuata utaratibu, ungeweza kutumia mfano uliotolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, kuhusu gharama za matibabu ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, marehemu Samuel John Sitta.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, marehemu Spika Sitta aliomba apatiwe msaada wa Bunge na/au Serikali wa fedha za matibabu kwa njia ya barua pepe (email), wakati akiwa tayari matibabuni nchini Uingereza.
Pamoja na kwamba alishastaafu Ubunge na Uspika, Bunge la Spika Ndugai na Serikali ya Magufuli walitoa fedha za matibabu na gharama za kujikimu kwa ajili ya marehemu Spika Sitta na msindikizaji wake mpaka alipofariki dunia, na alizikwa kwa gharama ya Bunge na Serikali na kwa heshima zote za kibunge na kiSerikali.
Ungeweza kuhoji kwa nini utaratibu huo uliwezekana kwa mtu ambaye wala hakuwa Mbunge tena, lakini umeshindikana kwa Mbunge aliyeshambuliwa kwa risasi akiwa Dodoma kwa vikao vya Bunge.
Hukufanya hivyo. Matokeo yake ni kwamba makala yako inaficha, badala ya kufichua, aibu kubwa ya wale ambao wameapa kulinda, kuheshimu na kuhifadhi Katiba na Sheria za nchi yetu, lakini wanazivunja na kuzinajisi hadharani kwa sababu ya chuki zao za kisiasa.
Badala ya kuleta nuru na uelewa zaidi katika suala hili, makala yako imeongeza giza na sintofahamu kubwa miongoni mwa wasomaji wako wengi.
Mimi na ndugu zangu na familia yangu hatujawahi, na hatutegemei, kuomba kufadhiliwa au kuonewa huruma au kusaidiwa na Bunge wala Serikali katika suala hili la matibabu yangu.
Tumedai, na tutaendelea kudai, kutendewa haki kama ilivyoelekezwa na Sheria iliyotungwa mahsusi kwa ajili hiyo na Bunge letu. Tunachotaka ni utawala wa sheria, sio hisani ya Rais Magufuli au Spika Ndugai.
Naomba uniwie radhi kama nitakuwa nimekukwaza kwa haya niliyoyaandika, au kwa namna nilivyoyaandika.
Tundu AM Lissu (MB)
Tienen, Ubelgiji
Novemba 22, 2018

No comments :
Post a Comment