Chama hicho kimemeguka katika makundi mawili likiwapo linaloongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif na lile la Profesa Lipumba, mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Madai ya Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo yalitolewa jana na Katibu wa Ulinzi na Usalama wa CUF upande wa Lipumba, Khalifa Suleiman Khalifa alipozungumza na wanahabari akidai wamebaini suala hilo baada ya hivi karibuni vyama sita vya upinzani kufanya mkutano wa faragha mjini Zanzibar.
Hata hivyo, Maalim Seif alikanusha madai hayo jana alipozungumza na Mwananchi na kusema mkutano huo haukuwa na ajenda ya yeye kujiunga na ACT-Wazalendo, bali ulihusu na mambo mengine ya kisiasa kama yalivyoelezwa kwenye maazimio yao.
Alisema hakusudii kuihama CUF na haiwezi kutokea kwa kuwa yeye ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho.
“Nafikiri nilishaeleza kwenye mkutano wetu kwamba tayari tunayo plan B ambayo tutaitumia kama chama, iwe tumeshinda kesi au tumeshindwa na hilo ndilo la kuchukua kwa sasa,” alisema.
Wakati Maalim Seif akisema hana mpango wa kuiacha CUF, Khalifa alidai kuwa moja ya ajenda za mkutano huo ilikuwa ni kupanga Maalim Seif na baadhi ya viongozi wa chama hicho watakavyojiunga ACT Wazalendo huku akisisitiza kuwa makubaliano yameshafikiwa.
Alitaja baadhi ya aliyodai kuwa ni makubaliano kwamba upande wa Maalim Seif uachiwe nafasi zote za uongozi upande wa Zanzibar na Zitto Kabwe (kiongozi wa ACT- Wazalendo) na wenzake washike upande wa Tanzania Bara.
Khalifa alisema watabaki kuwa imara zaidi pindi kiongozi huyo atakapoondoka.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa CUF, Mohamed Habib Mnyaa alisema wamejipanga na wako tayari kupokea uamuzi wowote.
Mnyaa alisema anaamini kuondoka kwa Maalim Seif kwenye chama hicho hakutakuwa na madhara yoyote akidai kuwa wananchi kwa sasa wanaujua ukweli.
No comments :
Post a Comment