
Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kuwa na mwelekeo mpya wa kujenga uchumi wa kisasa, kwa kushiriki katika shughuli za ujenzi wa viwanda sambamba na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa viwanda na kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwatunuku vyeo wahitimu 513 waliofaulu zaidi mafunzo ya Uofisa na Ukaguzi, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es salaam, Rais Magufuli alisema kuwa imefika wakati Jeshi la Polisi kuwa na mwelekeo mpya wa uchumi wa kisasa ili kusaidia majeshi hayo kuwa na uwezo wa kujiendesha vizuri bila kutegemea sana Serikali.“Mtafute mwelekeo mpya wa majeshi yetu, unaolenga kujenga uchumi wa kisasa, mjipange kushiriki shughuli za uchumi hasa ujenzi wa viwanda, pamoja na kupanua wigo wa kutengeneza sare zenu, na bidhaa mbalimbali za viatu au maji hali itakaosadia kuwa na bidhaa za ziada badala ya kununua na kuweza kujiendesha” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alitolea mfano baadhi ya majeshi kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara ,ambapo alisema Jeshi la nchi ya China limejenga mji mkubwa nchini humo.
Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza kushirikiana na majeshi mengine nchini likiwemo Jeshi la Polisi kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali pamoja na kusaidiana masuala kadhaa.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameahidi kukipatia Chuo cha Taaluma ya Polisi nchini kiasi cha shilingi milioni 700 kabla ya ijumaa wiki ijayo kwa ajili ya kukarabati chuo hicho kwa kujenga mabweni na madarasa ya kisasa kwa lengo la kuboresha hali ya chuo na kuongeza ufanisi kwa wahitimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, alisema ujenzi wa makazi ya Polisi unaendelea kwa kutumia fedha walizopewa na Serikali kiasi cha shilingi bilioni 3.7, na wanatarajia kukarabati nyumba 400 za Polisi mara baada ya kupewa kiasi cha fedha kilichobaki ikiwa ni ahadi ya Rais Magufuli, aliyoitoa mapema mwaka huu ya kuwapa Jeshi hilo shilingi bilioni 10 ambazo ameahidi kuwapa ndani ya kipindi cha wiki moja.
Vilevile, IGP Sirro, alisema kuwa nchi iko salama kwani hali ya uhalifu imepungua kwa kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kufanyakazi kwa kuzingatia nidhamu na weledi
“Hali ya uhalifu imepungua nchi nzima,makosa ya barabarani yamepungua kwa asilimia 32.6, ajali zimepungua kwa asilimia 30.8, kwa ujumla kumekuwepo na upungufu wa matukio ya uhalifu kwa sababu Jeshi la Polisi linashirikiana na wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao”alisema IGP Sirro.
No comments :
Post a Comment