
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF, Sabra Issa Machano amewaomba radhi Wajasiriamali waliokuwepo kwenye maonesho ya kwanza yaliyoandaliwa na Taasisi yao kwa kitendo cha kutohudhuria Msanii Maarufu nchini Diamond Platinumz (SIMBA) kwa mujibu wa ratiba zilivyopangwa.
Mfuko wa Hifadhi Ya Jamii Zanzibar ZSSF uliandaa maonesho yao ya kwanza yaliyowakutanisha Wajasiriamali wa bidhaa tofauti kutoka ndani na nje ya Zanzibar kuonesha bidhaa zao katika kiwanja cha kufurahishia Watoto Kariakoo na kuahidi maonesho hayo yaliyofunguliwa kuanzia tarehe 5 Disemba kuwa yatafungwa tarehe 10 Disemba na Msanii Diamond Platnumz jambo ambalo halikutendeka.
Taarifa iliyotolewa ni kuwa Diamond atakwenda kuzungumza na wajasiriamali hao akiwa na kundi lake la Wasafii majira ya saa 11 jioni lakini hadi kufikia majira ya saa 2:00 Usiku Wajasiriamali na watu mbalimbali walikuwa wakisubiri ujio wa msanii huyo lakini hakuonekana.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Sabra Machano ameomba radhi kufuatia tukio hilo na kusema Diamond alishindwa kufika eneo hilo kwa wakati kutokana na hali yake kutokuwa nzuri baada ya kuanguka Stejini wakati akitumbuiza huko Sumbawanga.
No comments :
Post a Comment