Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 7, 2019

Kanuni 15 za Ujasiriamali ambazo ni lazima uzifahamu!

Ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa ajira umekuwa wa shida sana, watu wengi hujikuta wakiwa na chaguo la kuwa wajasiriamali pekee kwenye maisha yao.

Wengi hutamani au hata kujiingiza kwenye ujasiriamali, lakini siyo wote wanaofanikiwa kutokana na kutokufahamu kanuni muhimu za ujasiriamali. Ni wazi kuwa ili uanzishe kitu chochote chenye mafanikio, ni lazima ufahamu kanuni za kukifanya kitu hicho jinsi ipasavyo.

Ikiwa wewe ni mjasiriamali, au unataka kuwa mjasiriamali, basi fuatilia makala hii ili nikufahamishe kanuni 15 za ujasiriamali.

1. Kuwa mtatuzi wa matatizo
Ujasiriamali ni zaidi ya kupata pesa, ni lazima kwanza utatue changamoto ya mtu ndipo utaweza kupata pesa kutoka kwa mtu husika. Ni muhimu ukafahamu kanuni hii kama mjasiriamali kwani hutojikita kutafuta pesa bali utajikita kutatua matatizo ya watu.Kwa mfano kama kuna tatizo la upatikanaji wa mboga katika mji au eneo unalokaa, ikiwa wewe utaleta mboga katika eneo hilo ni wazi kuwa watu watakupa pesa ili uwape mboga. Hivyo ni muhimu kila mara ukatafuta changamoto ukaitatua, nawe bila shaka utapata pesa za uhakika.

“Pesa ni matokeo ya kutatua shida ya mtu”

2. Kuwa na maono
Hakuna ujasiriamali bila maono. Kuwa mjasiriamali bila maono ni sawa na kuendesha gari isiyokuwa na usukani. Maono katika ujasiriamali yatakuwezesha kukuongoza ufanye nini na kwa muda gani. Ni lazima ujiulize kuwa unataka kuwa nani, lini na unataka kufanya nini baadaye? Jonathan Swift alisema maono ni sanaa ya kuona kile ambacho wengine hawaoni. Ni lazima uwe na lengo na ufanye bidii kulifikia.

“Wajasiriamali waliofanikiwa ni wale walioweza kubadili maono yao kuwa uhalisia”

3. Chagua washirika au timu sahihi
Wakati mwingine utahitaji kufanya kazi na watu au mtu fulani. Ni muhimu kuwa makini wakati wa kuchagua washirika au timu ya kufanya nayo kazi ili kuhakikisha maono yako hayakwamishwi. Kamwe usichukue mtu tu kwa kigezo kuwa ni rafiki au ndugu yako, bali chukua mtu ambaye unaamini anaweza kufanya kitu chenye tija kwa ajili ya kufanikisha malengo yako kama mjasiriamali.

4. Toa huduma au bidhaa yenye tija
Hivi leo sokoni kuna bidhaa na huduma nyingi ambazo ni za aina moja, lakini siyo zote zinafanya vizuri. Hii ni kutokana na baadhi ya bidhaa au huduma kutozingatia kuwa na tija kwa wateja wake. Ikiwa unatengeneza bidhaa au huduma fulani hakikisha itakuwa na manufaa makubwa na ya uhakika kwa wateja wako.

Kwa mfano nimewahi kuona vitafunwa vilivyoandaliwa katika mazingira duni na kuwa na dosari mbalimbali kama vile marashi, vipande vya nywele, mchanga n.k. Ni wazi kuwa bidhaa za namna hii zitakosa wateja kutokana na kuwa na ubora duni.

Kila mara kumbuka kuwa ushindani ni mkubwa, hivyo jitahidi kuongeza tija na ubora wa huduma na bidhaa zako.

5. Fahamu na jali wateja
Ikiwa wewe ni mjasiriamali, basi futa mawazo kuwa wateja wanakuhitaji wewe. Fahamu kuwa wewe kama mjasiriamali, ndiye unaye wahitaji wateja ili ukuze biashara au huduma yako. Hakikisha mambo haya kuhusu wateja:

  • Fahamu wanataka nini.
  • Sikiliza maoni na ushauri wao.
  • Hakikisha unakamilisha mahitaji yao.
  • Tumia lugha nzuri na rafiki kwa wateja.
  • Mfanye mteja aone unamthamini.
  • Mfanye mteja aone kuwa umetanguliza huduma kabla ya pesa.

Naamini kwa kufanya hivi utaweza kujijengea msingi mzuri wa wateja kwa ajili ya huduma au bidhaa zako kila siku.

6. Tumia pesa vyema
Changamoto ya matumizi mabaya ya pesa inawakabili watu wengi kuanzia kwenye matumizi yao binafsi ya pesa. Watu wengi wanapata pesa lakini zinaisha bila ya kufahamu wamezitumiaje au wamefanya kipi chenye tija.

Ni wazi kuwa matumizi mazuri ya pesa ni kanuni muhimu sana kwa mjasiriamali, kwani kwa njia hii utaweza kukuza biashara yako kila siku. Jifunze kufahamu hii ni pesa kwa ajili ya nini, na uitumie kwa mambo ya msingi pekee. Epuka tabia za kibadhirifu na anasa. Ikiwa biashara au uwekezaji wako ni mkubwa, basi unaweza kumwajiri mtu aliye na taaluma ya utunzaji na usimamizi wa pesa.

Unaweza pia kujifunza wewe mwenyewe jinsi ya kutunza na kutumia pesa vyema; unaweza pia kutumia programu za bure za kompyuta kama vile Wave app kutunza mahesabu yako.

7. Jifunze kusema hapana
“Hapana” ni jibu dogo lakini lenye manufaa makubwa. Ikiwa wewe ni mjasiriamali ni muhimu kuzingatia kanuni hii ya kusema hapana kwani itakutenga na mambo au mipango isiyokuwa na ulazima.

Kuna watu, mipango, vitu au hata tabia ambazo zinaweza kukuathiri vibaya sana kwenye ujasiriamali wako. Hivyo kusema hapana kutakuepusha kwa kiasi kikubwa na mambo haya.

8. Usipuuze nafasi ya teknolojia
Tunaishi kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia, hivyo wewe kama mjasiriamali huwezi kujitenga nao. Kwa kupitia teknolojia kama vile simu na mtandao wa intaneti, unaweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza mauzo ya huduma au bidhaa zako.

Hakikisha wewe kama mjasiriamali unakuwa karibu na wateja wako ili kutatua shida na mahitaji yao; pia hakikisha unajifunza mbinu bora za kufanya biashara kupitia mtandao.

Soma pia: Makosa 8 ya Kuepuka Unapofanya Biashara Kwenye Mtandao.

9. Fahamu soko
Kanuni mojawapo ya kuongeza mauzo yako kama mjasiriamali ni kulifahamu soko vyema. Hakikisha huduma au bidhaa unayoitoa inakidhi mahitaji na inafika kwenye soko stahiki.

Kwa mfano ikiwa wewe ni mzalishaji wa mayai, lakini eneo ulilopo soko ni duni, basi tafuta eneo jingine ambalo soko la bidhaa hii ni nzuri. Ikiwa wewe huwezi kwenda, unaweza kutafuta mtu kwenye eneo lenye soko zuri akakuuzia bidhaa yako na ukampa gawio fulani.

Kwa kufanya hivi utaweza kulenga soko na kujiongezea faida zaidi wewe kama mjasiriamali.

10. Ongeza maarifa
Kwanza nikupongeze kwa kusoma makala hii, ni wajasiriamali wachache sana ndiyo hupenda kusoma makala na vitabu mbalimbali ili kuongeza maarifa. Ni muhimu sana kila mara ukajizoesha kujiongezea maarifa, hasa ya ujasiriamali pamoja na kile unachokifanya; hili liitakuwezesha kuwa na tija na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Unaweza kusoma vitabu, majarida na tovuti mbalimbali (kama fahamuhili.com) ili kuongeza maarifa yako.

11. Jifunze kutokana na makosa
Moja ya kanuni inayozingatiwa na wajasiriamali waliofanikiwa ni kujifunza kutokana na makosa. Makosa ni shule nzuri sana kwa kila mtu hasa wajasiriamali. Ikiwa uliwekeza ukapata hasara, basi jifunze nini hasa kilikuwa chanzo cha hasara ili mbeleni uweze kukiepuka. Usikubali kukwamishwa na makosa, bali yawe ni hamasa kwako ya kuendelea mbele zaidi.

“Uzoefu ni kufanya makosa na kujifunza kutokana na makosa hayo”

Bill Ackman
12. Jifunze kwa waliofanikiwa
Watu wengi wameshindwa kufanikiwa kwenye maisha yao kwa sababu wanajifunza kwa walioshindwa. Walioshindwa wana maneno mengi, hasa ya kukatisha tamaa kama vile hili haliwezekani, hili linahitaji pesa nyingi sana, mimi lilinishinda, linachosha, lina faida ndogo, kuna wengi wanaolifanya, fulani alishindwa n.k.

Wewe kama mjasiriamali, epuka watu hawa na ujifunze kwa waliofanikiwa, fahamu walitatua vipi changamoto walizokabiliana nazo pamoja na mipango waliyoitumia hadi wakafika hapo walipo.

13. Tumia muda vizuri
Hakuna mtu mwenye zaidi ya saa 24 duniani; lakini mwingine muda unamtosha wakati mwingine analalamika  muda haumtoshi. Ni wazi kuwa mpangilio au matumizi mabaya ya muda ndiyo husababisha changamoto hii. Wewe kama mjasiriamali ni muhimu ukaondoa mambo yasiyokuwa na ulazima kwenye ratiba yako. Tambua ni kitu gani ni cha muhimu zaidi na ukifanye kwa wakati.

14. Weka vipaumbele
Wewe kama mjasiriamali, ni muhimu kuzingatia kanuni hii ya kujiwekea vipaumbele; vipaumbele vitakuwezesha kubaini ni kipi kianze na ni kipi kifuate kutokana na umuhimu wake.

Kwa mfano ikiwa kuna wateja walipata shida kupata huduma au bidhaa yako, maliza kwanza swala hili kabla ya kuendelea kuweka jitihada za kuuza bidhaa mpya. Kwa kufanya hivi utaweza kufanya mambo kutokana na umuhimu wake, jambo ambalo litakuwezesha kukua.

15. Usikate tamaa
Ni wazi kuwa katika safari ya ujasiriamali utakutana na changamoto mbalimbali. Jambo la msingi ni kukumbuka kanuni hii kuwa usikate tamaa. Tumia changamoto kama chachu ya kukuhamasisha kufanya bidii zaidi na usirudi nyuma.

Changamoto zipo leo na kesho lakini keshokutwa hazitakuwepo tena; jambo unalotakiwa kufanya ni kutazama lengo lako na kufanya bidii kila kukikucha kuzikabili changamoto husika ili ufikie lengo lako.

“Siri ya mafanikio yetu ni kutokukata tamaa”

Wilma Mankiller

Hitimisho

Naamini umefahamu kuwa kuna kanuni muhimu ambazo wewe kama mjasiriamali unatakiwa kuzizingatia ili uweze kufanikiwa. Ni wazi kuwa bidii, mipango mizuri na kutokukata tamaa kutakuwezesha kufikia lengo lako la kufanikiwa kama mjasiriamali.
/Muungwana.

No comments :

Post a Comment