dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, October 10, 2019

Tumefiwa walimwengu: Mohamed Mlamali Adam (1944-2019)!

Tumefiwa walimwengu: Mohamed Mlamali Adam (1944-2019)
Na Ahmed Rajab
SHEIKH Mohamed Mlamali Adam,  aliyefariki dunia katika hospitali moja jijini London usiku wa Jumamosi iliyopita, akiwa na umri wa miaka 75 alikuwa mtu wa vipaji vingi.  Alikuwa mwandishi, mtangazaji wa redio, mhariri wa magazeti, mkalimani (aliyezimudu vilivyo lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu), mfasiri wa riwaya na mhakiki wa mashairi.

Lakini watu wengi hususan Waisilamu wa Ulaya watamkumbuka kwa ushekhe wake na umahiri wake wa kutoa mawaidha ya kuwavutia watu katika dini

Mlamali hakuwa shekhe wa vilemba, kashda na majuba. Sana sana akivaa kofia ya mkono.  Na  hiyo akiivaa kwa nadra. Mara nyingi akenda kichwa wazi, akiwa amevaa shati, suruwali na koti.  Akipenda kujificha, hakutaka ajulikane, akifuata moja ya miongozo ya tariqa yake ya Kisufi ya Ba ‘Alawi inayojulikana pia kwa jina la Tariqa ‘Alawiyya.


Ingawa mara nyingi kichwa chake kilikuwa wazi lakini ndani ya kichwa hicho mlikuwa bahari. Nayo ilikuwa shuwari, isiyochafuka.  Na juu ya bahari hiyo pakielea ilmu, hasa ilmu ya dini ya Kiisilamu. 

Tukimuona Mlamali akijiendea, kumbe akiibeba bahari iliyomgeuza naye awe bahari.

Kwa nilivyomjua ninathubutu kusema kwamba katika mwisho wa uhai wake Mlamali alikuwa ni “al Arif Billah”.  Hii ni hii ni daraja kubwa katika tasawwuf (Sufism). Masufi wanaamini kwamba watu wenye kufikia daraja hii ni wenye kumjua Mwenye Ezi Mungu, siri na asirari zake.

Kwa mujibu wa mashekhe wa Kisufi watu wa aina hiyo ya Mlamali huko akhera Mungu huwajaalia yale ambayo macho yoyote hayakuwahi kuyaona, yale ambayo hayakuwahi kamwe kusikiwa na masikio yoyote, na yasiyowahi kuzipitia nyoyo za wanadamu (maa laa ‘aynun ra’at wala udhunun sami‘at wa laa khatara ‘ala qalbi bashar).

Tumeondokewa si na mtu bali na jitu la ilmu. Si mti bali gogo.  Alikuwa kama ensaiklopidia Ukiwa na tatizo la kidini ilikuwa umuulize tu. Naye alikuwa tayari kukwambia wapi pa kukupatia jawabu yako ama kwenye Qur’an au kwenye vitabu vingine. “Hebu tazama kitabu fulani, mahala fulani, utapata jawabu.” Alikuwa ni mtu wa aina hiyo.

Ubongo wake ulikuwa mithili ya simaku. Alikuwa hodari  wa kuhifadhi alichokisoma.  Mfano ni dua zote za Al Habib Ali bin Muhammad bin Hussein al Habshi ambazo alizihifadhi kwa moyo. Dua hizo, ambazo ni nyingi mno, alikuwa akizisoma tangu utotoni kwenye msikiti wa Sharifu Abudu huko Vikokotoni, Unguja. 

Katika kusaka kwake ilmu alikuwa akihudhuria darsa zilizokuwa zikiendeshwa huko saa za alfajiri. Wala hakuwa akiona taabu kuazimia vitabu vya dini kutoka kwa Prince Seyyid Haroub, mjukuu wa sultan wa enzi Seyyid Khalifa bin Haroub. 

Mwana huyo wa kifalme alikuwa pia ni sufi naye na Mlamali wakikutana kwa Alhabib Omar bin Sumeit.  Mlamali akimuitakidi sana pia Habib Swaleh bin Alwi Jamalul-leyl wa Lamu (1853-1932).

Miongoni mwa mashekhe waliomlea Mlamali katika mambo ya dini, ya kiroho, ni Alhabib Sayyid Omar bin Ahmed bin Sumeit, Sayyid Ahmed bin Hussein, Mwinyi Baraka na Sheikh Muhyiddin bin Omar ambaye katika zama za siasa alikuwa mmoja wa wasomaji dua kwenye mikutano ya chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).  Mlamali aliwahi kwa muda kukaa kwake na akihudhuria darsa zake wenye msikiti wake Baraste Kipande. 

Pamoja na kutoa mawaidha katika mikusanyiko mbalimbali, jijini London alikuwa akiendesha darsa mbili.  Iliyokuwa kubwa ilikuwa ile ya eneo la Wembley iliyoanzishwa katika miaka ya 1980 kwa idhini ya al Habib Ahmed Taha Mash-hur al Haddad.  Darsa hizo akizitoa kwa lugha ya Kiingereza na zikihudhuriwa na wanaume pamoja na wanawake wa kabila mbali mbali.

Mwanzoni alikuwa akiziendesha kila baada ya wiki mbili, halafu zikawa za kila mwezi mara moja na mwishoni mwa uhai wake, hali yake ya afya ilipokuwa si nzuri, alikuwa akidarisisha kila baada ya miezi miwili.

Darsa nyingine ilikuwa ni ya kila Jumamosi aliyokuwa akiendesha nyumbani kwake.  Hii ilikuwa ndogo, ikihudhuriwa na watu wachache aliowataka mwenyewe.

Miongoni mwa waliokuwa wakihudhuria ni Sheikh Abdal Hakim Murad, ambaye sasa ni profesa katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza.  Murad ni Muingereza aliyesilimu alipokuwa kijana mdogo na sasa ni alim wa dini ambaye mihadhara yake huwavutia wengi.

Darsa za nyumbani kwake Mlamali zilikuwa zikianza kwanza kwa kiarabu,  kwa wanafunzi wake waliobobea katika lugha hiyo. Halafu zikawa kwa Kiswahili kwa wanafunzi wake wa Afrika ya Mashariki.

Mlamali alikuwa akisomesha sana mambo ya fiqhi. Mara moja moja akigusia mambo ya “tasawwuf”. 

Akishikilia watu waelewe mambo ya msingi katika dini kama kwa mfano namna ya kutawadha kabla ya kutaka kujua mingine.

Mlamali alikuwa akiwasomesha wanafunzi wake utadhani kama akiwashika mikono na kuwapitisha katika njia itayowafikisha kule alikotaka wafike, kwenye ucha ungu.

Mohamed Mlamali Adam alizaliwa Misufini, Unguja, Oktoba 8, 1944. Nyumba yao ilikuwa jirani sana na kwa kina Salim Said Salim, ambaye siku hizi ni miongoni mwa waandishi wakongwe wa Zanzibar. Tuliyekuwa tukimjua Mohamed Mlamali tangu miaka ya 1950 tumezoea kumwita kwa jina lake la pili, Mlamali, jina la baba yake. 

Bwana huyo alikuwa akifanya kazi kwenye Jumuiya ya Walimaji Karafuu (CGA). Pembeni akinunua samaki kwa jumla, akiwakaanga na mkewe Bi Asha, mamake Mlamali, akiwauza.

Mlamali alikirithi kipaji cha ufasaha wa kusema na kuandika nyumbani kwao kutoka kwa bibi yake mzaa mama, Bi Mwanriziki, bibi wa Kingazija aliyekuwa ameolewa na bwana mmoja kutoka sehemu za shamba.  Bibi huyo aliyekuwa na ustadi mkubwa wa lugha ya Kiswahili alimrithisha kipawa hicho Mlamali pamoja na mdogo wake Adam Mlamali aliyekuwa gwiji wa mashairi ya nyimbo za Taarab.

Mohamed Mlamali hakuwa akitunga mashairi ingawa alikuwa na ujuzi mkubwa wa mashairi hayo.

Utotoni alikuwa mbele yangu katika madrasa (chuoni Msikiti Barza), katika skuli ya msingi ya Darajani na pia katika skuli ya Sekondari ya King George VI ambayo sasa inaitwa Skuli ya Lumumba.

Miongoni mwa waalimu wake katika skuli ya Darajani walikuwa Ibrahim Kassim, Omar Ahmed Muhdhar (Sharif Mapanga) na Abdalla Kassim Hanga. Utotoni Mlamali akimhusudu Hanga kwa umombo wake na Hanga ndiye aliyemsaidia kukikuza Kiingereza chake.

Mlamali alikuwa hodari skuli lakini uhodari wake haukuwa wa kuzaliwa nao ila aliupata kutokana na jithada zake kubwa katika masomo. Yeye na kaka yake, Said Mlamali, waliruhusiwa kufanya mtihani wa kuingia skuli ya sekondari wakiwa darasa la saba badala ya la nane. Wote walifuzu.

Alipohitimu masomo ya sekondari Mlamali alipata kazi ya kuwa mkalimani mahakamani kwanza Unguja kwa kipindi kifupi na baadaye Chake Chake Pemba. Mapinduzi ya Januari 1964 yalimkuta Pemba. 

Siku moja akiwa Unguja alikamatwa pamoja na baadhi ya mashekhe wakubwa. Walituhumiwa kuwa wakisoma dua kuiapiza serikali na kutaka kuipindua. Hakika ya mambo ni kwamba walikuwa wakikutana kila wiki kuomba dua. Walikuwa na ada hiyo hata kabla ya Mapinduzi. Walifungwa jela kwa muda bila ya kufanyiwa kesi.

Walipofunguliwa, Mlamali alihamia Dar es Salaam ambako kwa muda akifanya kazi katika ubalozi wa nchi moja ya Ulaya ya Mashariki.  Nilimkuta Dar mwaka 1968 nilipokwenda kwa mapumziko kutoka London.  Aliniuliza iwapo nikimjua mtu katika kitengo cha BBC kilicho Nairobi cha kunasa na kuzisajili taarifa za steshini za redio za baadhi ya nchi za Afrika na Mashariki ya Kati.

Nilimjulisha na Pat Edwards, Mwingereza aliyekuwa mkuu wa kitengo hicho na aliyewahi kuwa msimamizi wa vipindi vya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London. Baada ya kufuzu mtihani aliopewa aliajiriwa na alifanya kazi Nairobi kwa takriban miaka sita akitafsiri kwa Kiingereza taarifa zilizokuwa zikitangazwa ama kwa Kiswahili au Kiarabu na steshini za redio za nchi za Afrika ya Mashariki na za Kiarabu.

Katika kufasiri taarifa za Kiarabu akishirikiana na kina Salim Bakhressa, Profesa Said Hamdun na Muhsin Attas.

Hatua nyingine ya maisha yake ilimfikisha jijini Cologne, Ujerumani kwenye stesheni ya Sauti ya Ujerumani (DW) alikoianza tasnia ya uandishi habari na utangazaji wa redio.  Nafasi yake ya kazi Nairobi ikajazwa na Othman Miraji. Wawili hao baadaye wakafanya kazi pamoja DW.

Huko Cologne Mlamali alikutana na mwandishi maarufu wa Kinigeria, Peter Enahoro aliyekuwa mhariri DW na aliyekuwa pia akifanya kazi London kwenye jarida la Africa Magazine.   

Enahoro na Mlamali walikuwa wakishiriki katika kipindi kimoja cha Kiingereza na ndipo Enahoro alipovutiwa naye.  Enahoro alipohamia gazeti la New African  akiwa mkurugenzi wa uhariri alimchukua Mlamali. Hapo ndipo ulimwengu usio wa Kiswahili ulipoanza kumtambua kwa uandishi wake mahiri.

Mwaka 1983 nilikuwa mtu wa kwanza kuajiriwa na kampuni moja iliyokuwa ikitaka kuanzisha gazeti jipya la kila mwezi kuhusu Afrika.  Hatua yangu ya mwanzo ilikuwa kuwapata wenzangu wa kuliendesha gazeti. Nilifanikiwa bila ya tashwishi kubwa kumtoa Yusuf Hassan kutoka Idhaa ya Kiingereza ya BBC.  Halafu tukaanza jitihada za kumtoa Mlamali kutoka Africa Now, gazeti alilolianzisha Enahoro, ili ajiunge nasi. 

Hassan, siku hizi Mbunge wa Kamukunji, Nairobi, alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi katika gazeti la kila siku huko Baghdad, Iraq, kabla ya kujiunga na BBC. 

Mimi nilikuwa na uzoefu wa kuhariri kurasa za Afrika na Mashariki ya Kati za jarida la Uingereza lililokuwa likichapishwa kila baada ya miezi miwili. Jarida hilo, Index-On-Censorship linahusika na uhuru wa kujieleza na wanafasihi wanaoingia matatani.

Mlamali pekee alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi kwenye gazeti la kila mwezi kama tulilokuwa tunalianzisha. Tulimbembeleza na kumbembeleza. Hatimaye alikubali na tukamwachia yeye, kwa sababu ya umri na uzoefu wake, awe mhariri wetu mkuu. Aliyetoa jina la gazeti jipya alikuwa Yusuf Hassan na muda si muda Africa Events likaingia mitaani Afrika nzima na nje ya Afrika likinguruma.

Peter Enahoro alinikasirikia kwelikweli kwa kumyang’anya Mlamali. Alinipiga simu na kunambia:

“Ahmed, ahsante sana kwa kutaka kutuua.” Akaibwaga simu.

Pamoja na umaarufu alioupata Africa Events wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC wakifurahikiwa sana na makala yake kwenye kipindi cha ‘Barua Kutoka London’.

Tangu aondoke Unguja hakurudi. Ingawa mwenyewe hakusema, inaweza kuwa sababu ni uonevu aliofanyiwa wa kutiwa jela bila ya kufanya kosa.

Atakumbukwa kwa mengi yakiwa pamoja na kazi zake za uandishi na tafsiri mbali mbali.  Tafsiri yake ya “Things Fall Apart”,  riwaya ya mwandishi wa Kinigeria Chinua Achebe, aliyoiita “Hamkani si shwari tena” ni tafsiri ya mwanzo ya Kiswahili ya kazi kubwa ya fasihi ya Kiingereza.

“Ikisiri ya Inkishafi” alichokiandika akitumia jina Muhamadi wa Mlamali kilichapishwa 1980 na shirika la uchapishaji vitabu la Longman huko Nairobi. Kwa “ikisiri” alikuwa na maana ya ufafanuzi. Na kitabu hicho kinaufafanua utenzi wa Kiswahili “Al Inkishafi” uliotungwa na Sayyid Abdallah bin Ali Nasir wa Lamu baina ya mwaka 1810 na 1820. 

Kwa vile lugha aliyoitumia Mlamali katika ufafanuzi wake ni ya “babu kubwa” nikimtania kwamba panahitajika kitabu kingine chenye jina la “Ikisiri ya Ikisiri ya Inkishafi.”

Tukiviweka kando vitabu hivyo viwili vyote vingine alivyovifasiri vinahusika na dini. Miongoni mwavyo ni vya Habib Ali al Jifri, Imam Abdullah Alawi al Haddad na vya Al Habib Ahmad Mash-hur al Haddad. Pia ameandika kwa Kiingereza kitabu cha wasifu wa Al Habib Ahmad bin Zayn al Habshi Naf’an.

Mshairi mmoja wa Tanga, Hassan R. Hassan, aliposikia tu kuhusu kifo cha Mlamali alitunga shairi lifuatalo la beti tano alilolipa anuwani ya “Tumefiwa Waswahili”:

“Ai! Yabidi ninene, imenishinda nafusi

Msiba huu muone, ni  mzito si mwepesi

Yu wapi tena mwengine, wa kuongoza kikosi

Aketi pa Mlamali, mpenzi wa Kiswahili

*

Yeye alikuwa bingwa, lugha aliihandisi

Hojaze hazikupingwa, alikuwa mdadisi

Watajwapo hakutengwa, alitajika farisi

Katutoka Mlamali, mpenzi wa Kiswahili



Isilamu yake dini, hakuitia mkosi

Alisoma yakini, akasomesha unasi

Hatunaye duniani, nani pake ajilisi?

Awe kama Mlamali, mpenzi wa Kiswahili



Kifoche kubwa ajali, tumeondokewa sisi

Na mtu aliye ghali, muungwana si mtesi

Ninakuomba Jalali, mpe mema majilisi

Akae pa watu wema, mpenzi wa Kiswahili

*

Beti tano kaditama, hapa ninasema basi

Moyo wangu waniuma, kwa zito liso kiasi

Shime tusirudi nyuma, tuliobaki ni sisi

Tumuenzi Mlamali, mpenzi wa Kiswahili”

No comments :

Post a Comment