Salim. A. Bimani, Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma, ACT Wazalendo.
Chama cha ACT Wazalendo kimefadhaishwa sana na kitendo cha vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliokuwa kwenye maandamano kushusha bendera za ACT Wazalendo na kuondoka nazo kwenye Barza ya Msumbiji Jimbo la Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharib 'B', Mkoa wa Mjini Magharib, Zanzibar jana tarehe 08 Januari 2020 majira ya saa 3.35 asubuhi.
Jambo la kustaajabisha, maandamano hayo yaliyokuwa yanatokea Amani kuelekea Airport yalikuwa yanasindikizwa na askari wa Jeshi la Polisi ambao hawakuchukua hatua yoyote kuzuia kitendo hicho cha kihuni.
Mara baada ya tukio, uongozi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Mjini Magharib ulichukua hatua kuripoti kwenye kituo cha Polisi cha Mwanakwerekwe na baadaye kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Magharib 'B' lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Jeshi la Polisi hadi sasa.
Vitendo vya vikundi vya kihuni vya vijana wa CCM kushusha na kuondoka na bendera za ACT Wazalendo kwenye barza mbalimbali za ACT Wazalendo vimeshamiri hivi sasa hapa Zanzibar.
Mifano ya hivi karibuni ni ya kushushwa bendera kwenye Barza ya Kibele na Michamvi zilizopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. Matukio yote haya yaliripotiwa Polisi (PAJ/RB/526/2019 na 495/ 2019) lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Jeshi la Polisi dhidi ya hujuma hizi za dhahiri kwa Chama cha ACT Wazalendo.
MSIMAMO WETU:
1. Tunalitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kuyapa uzito matukio haya ya ushushaji wa bendera za ACT Wazalendo na kuchukua hatua dhidi ya wahusika kwani yanahatarisha amani ya nchi.
2. Tunamtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kukichukulia hatua Chama cha Mapinduzi kwa vitendo hivi vinavyofanywa na makada wake. Chama cha ACT Wazalendo kimeshamuandikia Msajili wa Vyama vya Siasa kumlalamikia rasmi juu ya vitendo hivi.
3. Iwapo vitendo hivi havitadhibitiwa na Jeshi la Polisi, Chama cha ACT Wazalendo kitalazimika kujihami kwa kulinda matawi yake na kuchukua hatua kali dhidi ya wale wataothubutu kushusha bendera zetu.
Imetolewa Na:
Salim. A. Bimani,
Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma,
ACT Wazalendo.
Tarehe 09 Januari 2020.
No comments :
Post a Comment