AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, June 30, 2023

Eid Njema kutoka Zanzibar!

Tukio la DP World limepelekea kuibua mambo mengi, lakini ni pamoja na chuki kwa Wazanzibari, hasira na mtizamo hasi wa kidini. Na jengine ni suala la Muungano kwa maana kiasi cha kuonekana kuwa katika hili kidonda bado ni kibichi na kuwa suluhu inahitajika kama leo kwa uhai na afya ya Taifa ambalo lina pande mbili za asili Zanzibar na Tanganyika.

ALLY SALEH analitizama jambo hilo huku bado mjadala ukiwa haujatuwama na unaendelea kupita katika mkondo.
Pamoja na miaka hamsini na tisa ya Muungano bado kunakosekana dhati katika jambo hilo. Na ni hakika uhai wake unaweza kutishiwa panapotokea jambo lolote ambalo Zanzibar itahusishwa.

Inashangaza sana baadhi ya watu Tanzania Bara, wakiwemo viongozi wa kisiasa, wanatamka wazi kuwa Zanzibar inafaidika zaidi ya Tanganyika ndani ya Muungano.Wanaficha ukweli kuwa Tanganyika ndio ambayo inautawala Muungano dhidi ya Zanzibar.

Watu hao wanadai Tanganyika ndio iliyopoteza zaidi katika Muungano huu, bila ya kufafanua kuwa Zanzibar kama Tanganyika ilikuwa ni dola kamili kabla ya Muungano.

Hata hivyo ikija kwenye kupata haki za Muungano, kama kufaidi usawa wa kodi au kufanya biashara iwe iliyozalishwa Zanzibar au vyenginevyo, basi Zanzibar hufanywa kama nchi ya kigeni kwa vikwazo inayowekewa.

Ieleweke Zanzibar haikupoteza tu mamlaka ya jeshi, eneo, sarafu, kiti Umoja wa Mataifa, wenyewe ambapo kuingia kwake kwenye Muungano huu imekua daraja la pili na mshirika wake kuwa mwenye sauti juu yake. Ingawa hakuna sababu yoyote ile ya kuwa mkubwa zaidi yake kwa mujibu wa kanuni za miungano za kimataifa hakuna dola ndogo na kubwa katika Muungano.

Sisi Wazanzibari tunaamini na tunao ushahidi wa kutosha kuwa Tanganyika inafaidi zaidi kwenye Muungano kwa sababu imevaa koti ambalo haistahili kuvaliwa na wao peke yao, ambalo ni msingi unaozipa haki sawa nchi zilizoungana.

Kumekuwa na husda na choyo kama kwamba Zanzibar inalazimishwa iwe maskini na ombaomba kwa kukabwa kwa maeneo kadhaa ikiwemo kutofaidi rasilmali zake kwa mfano gesi na mafuta yaliogundulika, kuzuia kuingia katika soko la Tanganyika na tabaan soko la Afrika Mashariki kwa bidhaa inazozalisha, kutofaidi mazao ya uvuvi yaliomo bahari kuu, kutoweza kufikia mikopo na misaada ya kimataifa, kutokuwa na sera zake za fedha, kutokuwa na maamuzi katika mambo ya utafiti, elimu ya juu hayo yote yakiwa yamepokwa kwa kutiwa katika kapu la Muungano kupitia Orodha ya ongezeko la kilasiku la Mambo ya Muungano.

Kwa miaka hii ya Muungano sera na mkakati vimekuwa ni kuongeza Mambo ya Muungano na sio kupunguza. Tume ya Jaji Warioba ni chombo cha mwisho kilichothubutu katika Rasimu ya Katiba Mpya, kufanya pendekezo la kupunguza tatizo hilo, lakini Bunge Maalum la Katiba likapindua pendekezo hilo na hakika likaongeza Mambo ya Muungano. Kwa Wazanzibari hicho kilikuwa ni kitendo kisicho tofauti na uendelezaji wa ukoloni. Tume ya Warioba ilipanga Mambo ya Muungano yawe n inane.

Wazanzibari wanajua kuwa watu wengi hawaelewi udogo wa Zanzibar ni lazima ulindwe ili wabaki na utamaduni wao kama vile Tanganyika inavyolinda makabila madogo kama Wahadzabe. Zanzibar si visiwa tu vya Unguja na Pemba bali ni uhai wake wote ambao wenyewe wanatamani wabaki nao milele na wako tayari kuulinda kwa hali yoyote ile. Lazima katika Muungano wowote vipengele kama hivyo viwepo ili nchi ndogo ziendelee kuwepo na masharti maalum lazima yawekwe kwa maslahi ya pande zote. Mfano wa China Bara na Hong Kong.

Zanzibar haiajawahi kudai haki sawa ndani ya Muungano hasa za kiuchumi. Ila kwa mfano tunajua kiwango kilichowekwa kwa asilimia mgawio wa 79-21 kwa ajira chini ya Wizara za Muungano kwa zaidi ya miaka mitano sasa, lakini tunajua kwa hakika hilo halitekelezeki kwa sababu watendaji katika hizo Wizara za Muungano hawako tayari kutekeleza agizo hilo, ambalo halikuwekwa kisheria hadi leo.

Hilo si la kustajaabisha maana Serikali ya Muungano muda mrefu iligoma kuilipa Zanzibar asilimia nne na nusu iliopangwa kulipwa baada ya tume iliyoundwa kutakiwa kupanga kiasi ambacho Zanzibar ingelipzwa kwa mchangao wake kutokana na fedha iliyotia katika Benki Kuu ya Tanzania pale ilipoundwa, lakini hilo likaunganishwa na ukubwa wa eneo la Zanzibar na idadi ya wananchi wake.

Ila msimamo Msimamo wa Zanzibar ni kuwa haistahili kulipwa asilimia nne na nusu kwa sababu ilichangia kumi na moja na nuusu wakati wa kuundwa Benki Kuu ya Tanzania kutoka na fedha zilizokuwa za Zanzibar katika Benki ya Sarafu ya Afrika Mashariki, ambazo zilihamishwa kimya kimya wakati huo bila ya idhini rasmi ya Serikali ya Zanzibar, ambayo ilikwisha ingia katika Muungano. Hilo limekaliwa kimya pamoja na lile la kuunda Mfumo wa Pamoja wa Fedha ambao ndio njia mujarab wa kuamua ni vipi fedha za Muungano zitatumika kwa mambo ya Muungano na ziada kutiririka kwa Washirika.

Hili pia Tume ya Warioba ilipatia suluhu kwa maana ya kupendekeza Serikali Tatu na kutandika mipaka ya kila Serikali tabaan kuundiwa mfumo wake wa matumizi ya fedha zinazotokana na taasisi za Muungano kwa kila upande na Serikali ya Muungano.

Katika kilele cha ujinga kinachosambazwa Tanzania Bara ni kuwa Zanzibar ina Baraza la Wawakilishi na hivyo kuwa wana chombo chao cha kutunga sheria na kwa hivyo pia sio sahihi kuingia Bunge la Dodoma kujadili mambo mengi ya Tanganyika na yasio ya Muungano. Usahaulifu wa baadhi ya Watanganyika wenye mtazamo hasi na Wazanzibari ni wa hatari. Wanasahau kuwa Rasimu ya Warioba ilipendekeza kuwa na mfumo wa vyombo vitatu vya kutunga sharia-Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kama lilivyo, Bunge la Tanganyika na Bunge la pamoja la Muungano ambalo lingekuwa na wabunge Sabiini na Tano.

Hoja hio utadhani katika Bunge la Muungano hakuna kifungu ambacho kinamtenga Mzanzibari. Awali kabisa ilikuwa kuna uwezekano wa Mzanzibari kushika nafasi ya Waziri Mkuu na ilitokea kwa Mhe. Salim Ahmed Salim aliyeteuliwa na Mwalimu Nyerere siku hizo Mtanzania yeyote alikuwa ana uwezo wa Kikatiba kumteua. Ila kwa sasa Mzanzibari yeyote hawezi kushika nafasi ya Waziri Mkuu kwa sababu Waziri Mkuu lazima awe Mbunge wa Jimbo lolote Tanganyika.

Upande mwengine hii ilikuwa ni hatua ya wazi ya kuonyesha kuwa mtizamo halisi kuwa nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina muundo wa Serikali tatu, ambapo msingi wa kuwa na Waziri Mkuu akitokea Tanzania Bara ilikuwa ni thabiti kusema kuwa ataongoza chombo ambacho kiuhalisia kinasimamia asilimia zaidi ya tisiini kwa mambo yasio ya Muungano na ambayo ni ya Tanganyika na pia kusimamia bajeti ya asilimi zaidi ya tisiini pia kwa mambo yasio ya Muungano na ni ya Tanganyika na hupitishwa na Bunge ambalo huitwa ni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama Tume nyengine ziliozundwa kutizama mambo ya Muungano, basi Tume ya Warioba iliona upungufu huu ambao ndio chanzo cha mgogoro kabisa wa haki za pande mbili za Tanganyika na Zanzibar ndani ya muundo wa Muungano, kila mmoja akiona anapunjwa, au mwengine anabebwa na kupendelewa au mwengine ameachiwa kuwa na uhuru mkubwa na mwengine akidhibitiwa.

Watanganyika wengi wakaingizwa katika ujinga wa kuona Rasimu ya Warioba haikuwa na maana na hawakukizuia Chama cha Mapinduzi kuinajisi rasimu hiyo katika Bunge Maalumu la Katiba na kwa visingizio sasa wanailamu Zanzibar, ambayo kama ni muundo wa Serikali kwa asilimia Sitini na Moja walieleza kuwa wanataka Mfumo wa Serikali Tatu, kama ambavyo pia asilimia kubwa ya Watanganyika.

Lilotokea Bunge la Katiba kwa sababu ya ulafi wa watu waliokuwa wanataka kulinda nafasi zao kwa nguvu zozote zile, ndio linaloila nchi hii, na sababu ya chuki na hasira ambazo zinatishia sio tu kuigawa nchi yetu ya Tanzania bali kuipasua

Wazanzibari wamekuwa wakitiwa kitanzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa njia mbalimbali. Hata viongozi wa dini wanapachikwa mashtaka ya uhaini na ugaidi na kudhalilishwa.Tumeona akina Sheikh Farid, Sheikh Msellem na wenzao wa Bara wamewekwa jela miaka kadhaa pamoja na mateso, ukatili na unyama wa hali ya juu. Watwambie baada ya mahakama kubainisha kuwa si waha;lifu wamewajali kiasi gani na kuwapa haki zao.

Masheikh hao waliposimama kudai kura ya maoni kuhusu muungano (kala ya katiba mpya), walikamatwa na kupelekwa katika magereza ya Tanganyika kinyume cha sheria na katiba ya nchi.Mashtaka waliyopewa yanaweza kusimamiwa na Mahakama ya Zanzibar. Lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilidharau uwepo wa Mahakama Zanzibar, pamoja na hukumu iliyotolewa na iliyotamka watu hao wasipelekwe nje ya Zanzibar. Ikawa kama imewapeleka Guatanamo Bay yao Tanganyika. Na haijasahaulika pale katika miaka ya tisiini Zanzibar ilipogombwa kuingia katika OIC – Jumuia ya Kiislamu ya Ulimwengu kwa tamko Tanzania itaingia, lakini hilo mpaka leo haijafanyika

Kwa kuhitimisha ni imani yangu na mtazamo wetu sisi Wazanzibari suluhu inaweza kupatikana ndani ya Katiba Mpya ambayo itasukwa kwa ajili ya maslahi ya pande zote za Muungano utaokuwa wa haki, usawa na kuheshimiana.

0777430022

(BBC Correspondent 1984-2011 / Mbunge Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).

No comments :

Post a Comment