KER0 ZA MUUNGAN0: CHANZ0
NA SABABU
Na Amar Bawaazir
Dokezo:
Katika
Hati ya Muungano, kitu kilichofanyika ni kwamba, jina la Serikali ya Tanganyika
likabadilishwa na kupewa jina la Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar. Baadae ikabidilishwa kuwa Tanzania, na kutaka kuufuta
kabisa utaifa wa Zanzibar. Wako wanaosema kuwa hiyo haikuwa sawa. Hata Katiba
ya Tanganyika ikatumika, baada ya kurekebisha mambo machache tu, kama
kubadilisha jina na bendera.
Uhuru wa
Kuujadili Muungano
Katiba
ni makubaliano ya wananchi juu ya namna wanavyotaka kujitawala. Kwa hivyo wana
haki ya kuijadili juu ya mambo yote yanayowahusu wao. Bila shaka, tutaona kuwa
Muungano ni jambo muhimu sana linalowahusu waZanzibari zaidi ya mambo yote
mengine yaliyomo katika katiba. Rais Shein tayari ametuhakikishia kwamba tunao
uhuru kamili kuijadili Katiba Mpya.
Shirikisho au
Muungano?
Kabla ya kuujadili Muungano, inafaa tutazame chanzo cha dhana
ya Umoja wa Afrika Mashariki. Tukumbuke kwamba kabla ya uhuru wa nchi zote za
Afrika Mashariki, vyama vyote vya siasa hapa Zanzibar na Afrika Mashariki
vilikubaliana na wazo la kuungana katika Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF).
Mw. Nyerere alikuwa tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika
kama nchi zote za Afrika Mashariki zingeweza kupata uhuru kwa pamoja na
wakaungana. Kwa bahati mbaya, hili halikuwezekana. Mwaka 1961 Tanganyika
ilipata uhuru wake kamili.
Miezi 4 tu kabla ya uhuru wa Zanzibar, Agosti, 1963, Waziri
Tom Mboya wa Kenya alipelekwa na Kenya, Uganda na Tanganyika, kuiuliza Serikali
ya Zanzibar kama wako tayari kuanza mazugumzo juu ya EAF ya nchi 4. Zanzibar
ilitafakari na ikajibu kwamba walikuwa tayari.
Zanzibar ilipata uhuru wake kamili Disemba 10, 1963. Kama
tunavyojua, Mapinduzi yakatokea Januari 12, 1964, lakini Zanzibar bado ilibakia
na uhuru na madaraka yake kamili, pamoja na bendera, nembo, na haki zote za
kitaifa, pamoja na kiti chake Umoja wa Mataifa (UN) na OAU.
Kwa ghafla ilitangazwa Aprili 1964, siku 100 tu baada ya
Mapinduzi, kwamba Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
zinaungana katika Muungano wa nchi 2 tu. Kuna maswali mengi ya kujiuliza hapa.
:
Suali la kwanza: Kwa kiasi gani watu wa Zanzibar walishauriwa
kabla ya kubadilisha muundo mzima wa serikali, na kupoteza uhuru wetu
tuliopigania kwa miaka mingi?
Tunajua kwamba watu wa kawaida hawakuulizwa;
Inajulikana kwamba Marehemu Mzee Karume hakupewa fursa ya
kuwa na mshauri wa kisheria wake mwenyewe – Hati ya Muungano iliandikwa na
washauri wakizungu 2 wa Mw. Nyerere, na wao walitumia mfumo wa kikoloni wa
Ireland ya Kaskazini kutuandikia Hati ya Muungano.
Hati ya Muungano haikuridhiwa (ratified) na Baraza La
Mapinduzi, na Mwanasheria Mkuu wa SMZ amesema katika Mahakama kwamba SMZ haina
nakala ya Hati ya Muungano.
Suali la pili: Kwa nini tukaiacha dhana ya Shirikisho ya
Afrika Mashariki ya nchi 4, na tukavumbuwa Muungano mwengine mpya wa nchi 2 tu?
Hata Afro-Shirazi Party (ASP), ilikuwa haijataja katika
katiba na ilani yake kwamba dira yao ilikuwa muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
Hebu na tujiulize, kama kweli Mw. Nyerere alikuwa anaheshimu
utaifa wa Zanzibar sawasawa na wa Tanganyika, pale alipoamua kuimeza sehemu
kubwa ya Zanzibar ili isiweze kusimama tena kama nchi kamili?
Ingekuwa kweli azma ilikuwa kuleta Muungano wa Afrika nzima,
mbona hata marafiki wake, Obote wa Uganda na Kaunda wa Zambia, walishindwa
kujiunga katika Muungano wetu?
Mw. Nyerere alikua anapenda kuueleza Muungano kutumia mfano
wa makapu, na leo hii tutautumia mfano huo huo. Kama nilivyosema mwanzoni,
Tanganyika ilipata uhuru wake kamili 1961, na Zanzibar vilevile ilipata uhuru
wake kamili 1963. Kwa hivyo, nchi mbili hizi zilikuwa na madaraka na haki za
kimataifa sawasawa pale walipopata uhuru wao, na hata baada ya Mapinduzi.
Imeelezwa na Balozi wa Marekani kwamba aliporudi kutoka Dar
es Salaam, Mzee Karume alikuwa anaamini kwamba amesaini Mkataba wa Ushirikiano
baina ya nchi mbili hizi, kama alivyokuwa anaifahamu. Alipoulizwa Mzee Karume
kwa nini haipo serikali ya Tanganyika kama ya Zanzibar, alijibu kwamba hilo
lilikuwa shauri lao wenyewe. .
Jibu hilo halikuwa sawa, kwa sababu imeipa fursa Tanganyika
kubadilisha gamba na kuvaa gamba la Tanzania, na kumeza madaraka mengi ya
Zanzibar, kama tutavyoona.
Hati ya Muungano
Katika Hati ya Muungano, kitu kilichofanyika ni kwamba, jina
la Serikali ya Tanganyika likabadilishwa na kupewa jina la Muungano wa Jamhuri
ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Baadae ikabidilishwa kuwa
Tanzania, na kutaka kuufuta kabisa utaifa wa Zanzibar. Wako wanaosema kuwa hiyo
haikuwa sawa. Hata Katiba ya Tanganyika ikatumika, baada ya kurekebisha mambo
machache tu, kama kubadilisha jina na bendera.
SMZ ikabakia, lakini madaraka 11 ya serikali hiyo
yalihamishwa na kupelekwa kwenye Serikali ya Muungano. Sasa, tukiweka serikali 2
hizi katika mizani, zitakuwa hazina usawa tena, kwa sababu Serikali ya Muungano
sasa imekusanya madaraka yote ya Tanganyika na mambo 11 ya Zanzibar.
Mambo
haya 11 ya Muungano si yote yana sura ya kimataifa, bali yanahusu mambo mengi
ya uchumi wa ndani. Biashara ya Nje ni katika mambo hayo ya Muungano, lakini
uchumi wetu wakati ule ulikuwa unategemea sana uuzaji wa karafuu nchi za nje.
Hali
kadhalika, Kodi ya Mapato na Ushuru wa Bidhaa yote haya yamehodhiwa na Serikali
ya Muungano, na SMZ inapewa ruzuku ya aslimia nne nukta tano (4.5%) tu.
Vilevile, SMZ inakosa madaraka juu ya biashara na kodi, hivyo inakosa uwezo wa
kupanga uchumi wa nchi moja kwa moja. SMZ imeachiwa kazi ya kuendesha serikali
bila kupewa nyenzo ya fedha. Kwa hivyo, hata mgawanyo wa madaraka haukuwa wa
usawa.
Hati
ya Muungano ni mkataba wa kimataifa kama unavyojulikana katika sheria ya
kimataifa, na haiwezi kubadilishwa kila mara. Iligawana madaraka kati ya SMZ
iliobakia na mambo yote yasiokuwa ya Muungano, na Serikali ya Muungano iliokuwa
na madaraka yote ya Tanganyika yasiyo ya Muungano, na Mambo 11 ya Muungano ya
Tanganyika na ya Zanzibar.
Mambo ya Muungano ya Ziada
Lakini
mambo hayakuishia hapo. Kila mwaka au miaka 2, madaraka mengine ya Zanzibar
yalikuwa yananyakuliwa na kufanywa Mambo ya Muungano, haya ni pamoja na sarafu
(1965), mafuta na gesi (1968), na hata Baraza la Mitihani (1973). Mpaka sasa,
mambo mengine 11 yamehamishwa kutoka katika madaraka ya SMZ na kupelekwa Dodoma
– wengine wanasema mambo haya ni 22. Maana yake ni kwamba ile mizani iliyoinama
sana baada ya kuundwa Muungano, basi sasa imelala chini kabisa.
Hapa
tunapaswa tujiulize suali, jee hii ilikuwa ni halali? Hapa hatuna budi kumnukuu
Prof. Shivji, mwanasheria aliyebobea katika sheria ya katiba. Huyu sio
Mzanzibari lakini ni Mtanganyika; yeye si adui wa Mw. Nyerere bali ni mpenzi wa
mawazo ya Mw Nyerere, na sasa hivi anakalia kiti cha Uprofesa wa Mw. Nyerere
kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; yeye hachukii umoja, bali ni mkereketwa wa
Umoja wa Afrika, na kiti chake cha Uprofesa kinaitwa Kiti cha Muungano wa
Afrika.
Mwaka
wa 1990 alitoa hotuba yake muhimu sana kama tunataka kufahamu chanzo na sababu
za ‘Kero za Muungano’:
Alieleza
kwamba sehemu ya Hati ya Muungano inayotaja mambo 11 ya Muungano, ndiyo
iliyogawana madaraka kati ya serikali mbili, na kwa hivyo haiwezi kubadilishwa
bila kuvuruga muundo mzima wa Muungano.
Na
anaendelea kusema kwamba, si Bunge wala Baraza la Wawakilishi, kwa kila mmoja
peke yake, hawana madaraka ya kubadilisha sehemu hii ya Hati ya Muungano. Kwa
hivyo, Bunge kubadilisha sehemu hii,
kama
ilivyofanya mara 11, ni kuzidisha madaraka yake, na kuipokonya Zanzibar. Huu ni
‘unyang’anyaji na ubomoaji wa mfumo halisi wa Muungano.’ Mwisho wake SMZ
itabakia na kete tupu.
Prof
Shivji anamalizia kwa kusema kwamba, mabadiliko yote yaliyofanyiwa sehemu hii
ya Hati ya Muungano ni ‘haramu na batili.’
Kwa
bahati mbaya, Serikali ya Tanzania hawakujali onyo la Profesa Shivji, baada ya
miaka miwili tu, waliporejesha mfumo wa vyama vingi, wakaendelea na mtindo wao
wa kawaida. Wakachukuwa fursa ya kumnyima Rais wa Zanzibar, anaechaguliwa na
watu wa Zanzibar, nafasi yake kama Makamo wa Rais wa Tanzania, iliyotajwa
katika Hati ya Muungano. Yeye alikuwa kiungo muhimu kati ya SMZ na Serikali ya
Muungano. Sheria hii ilipitishwa na Bunge bila kuhitaji kura ya Thuluthi Mbili
(2/3) kwa pande zote mbili. Wabunge wengi wa Zanzibar waliogopa kupinga msimamo
wa chama tawala, na wakihiari kwenda kunywa chai au kwenda kujisaidia chooni
badala ya kupinga chama chao.
Baadaye
tu wakazinduka na wakaamua kumuingiza Rais wa Zanzibar kama Waziri bila Kazi
Maalum katika Baraza la Mawaziri la Tanzania, ambayo ni kumvunjiya heshima
yake. Badala yake, wakaleta mfumo wa Makamo Mwenza anaechaguliwa na Watanzania
wote, na anatakiwa awashughulikie Watanzania wote, lakini hana nafasi katika
SMZ.
Kwa
ufupi, ongezeko la Mambo ya Muungano baada ya 1964, na kumuondosha Rais wa
Zanzibar kutoka nafasi yake ya Makamo wa Rais wa Tanzania, yamevuruga kabisa
muundo wa Muungano. Vilevile, yamevunja Hati ya Muungano, ambayo ilikuwa
mkataba wa kimataifa kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Hati
ya Muungano ndio Katiba Mama ya Tanzania. Kwa kiasi kikubwa, mambo yaliofanyika
baada 1964 kwa makusudi hayakutaka kuheshimu makubaliano kati ya Marehemu Mzee
Karume na Mw. Nyerere, na kuheshimu utaifa wa Zanzibar. Sasa, hata Jaji Mkuu na
Waziri Mkuu wanathubutu kusema Zanzibar si nchi.
Katiba ya Muungano, 1977.
Lakini
mambo hayakuishia hapa. Tuangalie Katiba ya Tanzania ya 1977 inayoendesha nchi
hii kwa sasa hivi. Nirudie maneno niliosema mwanzoni kwamba katiba ni makubaliano
ya wananchi juu ya namna wanavyotaka kujitawala. Lakini, kabla ya katiba kupata
uhalali, inahitaji kupata ridhaa ya wananchi walioshirikishwa katika uundaji wa
katiba ile, kama sasa tunavyoshiriki katika kuandika Katiba Mpya – hi ndio
maana ya uhalali (legitimacy) tunapofikiria katiba.
Tukumbuke vipi Katiba ya 1977 iliandikwa. Mwaka ule vyama viwili vya ASP na TANU viliamuwa kuungana na kuunda chama kimoja, yaani CCM. Wenyeviti wawili waliteua kamati ya watu 20 chini ya Marehemu Thabit Kombo kuandika Katiba ya CCM – hiyo haitahusu sasa hivi.
Walipomaliza kazi ile, palepale, tarehe 16 Machi, 1977, Mw Nyerere, kama Rais wa Tanzania, aliteua kamati ileile kuandika Katiba Mpya ya Tanzania. Baada ya wiki moja tu, Tume ya Katiba ikawasilisha Muswada wa Katiba kwenye NEC ya CCM kupata baraka zake. (Hapa tufahamu kwamba muswada ule ulikuwa umeshatengenezwa hata kabla ya kuundwa Tume). Baada ya wiki 4 tu, na bila wananchi kupata fursa kuisoma na kuujadili muswada ule, ikapelekwa katika Bunge la Katiba.
Bungeni,
watu watatu tu walijaribu kuijadili, lakini palepale Waziri Mkuu Sokoine
akawambia kwamba muswada ule ushakubaliwa na Chama tawala chini ya mfumo wa
chama uliokuwepo, kwamba Chama kimekamata hatamu, kwa hivyo haina haja
kuujadili tena. Iliyobaki ni kupigiwa makofi.
Sasa tujiulize kama katiba iliyopitishwa namna hii bila kuwapa fursa wananchi kuijadili katiba yao, kama sisi sasa tunavyoijadili, inastahiki kukubaliwa kama ni takatifu na halali– kwa maana tuliotaja hapo mwanzoni?
Kuna matatizo mengi katika Katiba ya 1977, na ndio maana hata Serikali ya Muungano imekubali kuandika Katiba Mpya badala ya kutia viraka juu ya viraka. Lakini kuhusu Muungano, mimi nataka kuongea juu ya mambo 2 tu.
Jambo la kwanza ni kwamba nchi 2 ziliungana 1964, na kitu kilichowaunganisha ni Hati ya Muungano, na ndio inahisabika kama Katiba Mama ya Tanzania. Hio Hati ndio iliyozaa Katiba ya Serikali ya Tanzania na ya Serikali ya Zanzibar kama watoto wawili pacha. Katiba ya Tanzania haikuzaa Katiba ya Zanzibar, kwa sababu Serikali ya Tanzania haina madaraka juu ya mambo yasio ya Muungano ya Zanzibar.
Katiba ya Zanzibar inapata uhalali wake kutoka wananchi wa Zanzibar tu. Sasa, kwa nini Katiba ya Tanzania ya 1977 imeingiza sura nzima juu ya Serikali ya Zanzibar? Katiba ya Muungano haina madaraka yoyote juu ya rais wa Zanzibar, BLM au SMZ kwa ujumla, wala juu ya Baraza la Wawakilishi linalochaguliwa na watu wa Zanzibar tu chini ya Katiba ya Zanzibar.
Sasa kwa nini katiba ya Tanzania imetaka kujiingiza katika madaraka ya Zanzibar? Hii ni kutaka kujidai tu kwamba Katiba ya Zanzibar inatokana na Katiba ya Muungano, ambayo si kweli. Katika Katiba Mpya tunayotaka kuandika sasa, tusikubali kabisa kuwa na sura kama hii.
Mlango wa Nyuma wa Kuzidisha Mambo ya Muungano
[Katiba
ya Tanzania kulipa Bunge mamlaka hata katika mambo yasiyo ya Muungano kwa
Zanzibar.] Baya zaidi ni Ibara 64 ya Katiba ya Muungano ya 1977. Tunavyofahamu,
Katiba ya Muungano inatakiwa ishuhulikie Mambo ya Muuangano na Mambo ya Yasio
ya Muungano ya Tanganyika tu, na Katiba ya Zanzibar inatakiwa ishuhulikie Mambo
yasio ya Muungano kwa upande wa Zanzibar. Lakini Ibara 64 kwa makusudi imeweka
mlango wa nyuma wa kuzidisha mambo ya Muungano kinyemela.
Kifungu
cha 4 kinasema kwamba:
(4)
Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote haitatumika Tanzania
Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo-
(a)
Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile
Tanzania Zanzibar
29.
Huu ni udanganyifu mtupu. Kama jambo ni la Muungano, haihitaji kusema kwamba
itatumika Zanzibar vile vile; lakini kama si la Muungano, basi Bunge haina
madaraka ya kusema itafanya kazi Zanzibar, full stop.
Lakini
ndugu zetu wa damu waliendelea kutumia njia hii kutunyonya damu, na kuipora
madaraka Zanzibar kila mwaka kutoka 1977. Kati ya 1977 na 2011, wamepitisha
sheria ***? juu ya mambo yasio ya Muungano, na wakabandika bango kusema
itatumika Zanzibar. Kwa mfano:
Siasa
na vyama vya siasa sio mambo ya Muungano, lakini Sheria ya Vyama vya Siasa ya
1992 inasema kwamba sheria ile itatumika Bara na Zanzibar.
Bahari
na uvuvi sio mambo ya Muungano, lakini Mwaka 1989 Bunge lilipitisha sheria ya
Mamlaka ya Bahari na Maeneo ya Uchumi wa Bahari (Territorial Sea &
Exclusive Economic Zone), ambayo ilisema kwamba hata maili 12 ya bahari
wanamovua wavuvi wetu iko chini ya Muungano; na mwaka 1998 ikapitisha sheria ya
Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, na yote yalitamka kwamba yatatumika Zanzibar.
Juzi
juzi Waziri wa Bara alikwenda New York kutaka kuzidisha maeneo ya Tanzania
katika Bahari Kuu bila kushauriana na kukubaliana na SMZ. Wiki mbili
zilizopita, Wachina waliokamatwa wakivua kwa njia ya haramu Mashariki ya
Zanzibar 2009, walitozwa faini ya Sh. 20 billion na Mahakama ya Dar es Salaam –
pesa hizi zitaishia Bara kama wale samaki wa Magufuli.
Kupora
mamlaka ya Zanzibar ni suala la kikatiba, lakini Bunge halikuhitaji ata kura ya
2/3 kupitisha sheria hizi. Ni dhahiri kwamba hii ndio ilikuwa njia ya siri ya
kuitekeleza sera iliomponyoka Mhe. Ali Hasan Mwinyi katika Bunge mwaka 1994[?].
G55
waliposema kwamba bora kulifikiria suala la Serikali Tatu kutatua kero za
Muungano, Mzee Mwinyi aliteleza ulimi na akasema kwamba sera ya CCM ilikuwa
kutoka Serikali Mbili na kuenda kwenye Serikali Moja, sera ambayo haikuwahi
kutangazwa kabla ya hapo. Ajabu ni kwamba Mw. Nyerere alilaumu sana G55 na
Waziri Mkuu Malecela kwamba Serikali Tatu haikuwa sera ya CCM, lakini hakukataa
na hakumlaumu Mzee Mwinyi kwamba yeye vilevile aliokosea.
Bila shaka tuhakikishe kwamba Ibara kama hii isiwepo katika Katiba Mpya, na sheria zote zilizopenyezwa chini ya ibara hii zifutwe mara moja.
Bila shaka tuhakikishe kwamba Ibara kama hii isiwepo katika Katiba Mpya, na sheria zote zilizopenyezwa chini ya ibara hii zifutwe mara moja.
Hitimisho:
Kabla
ya Uhuru tulikubaliana vyama vyote Zanzibar na nchi zote za Afrika Mashariki
kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini lilioundwa 1964 haikuwa
shirikisho lakini ni Muungano wa Serikali moja na nusu (1 ½).
Wananchi hawakuulizwa juu ya suala la Muungano. Hati ya Muungano haikupata ridhaa (ratification) ya BLM, na Mwanasheria Mkuu wa SMZ alisema Mahakamani kwamba haijulikani iko wapi. Kwa ufupi, inakosa ridhaa na uhalali kutoka kwa wananchi;
Hati ya Muungano ilitaja mambo 11 ya Muungano, lakini mambo mengine, kama biashara za nje na kodi, yanaathiri uchumi wa Zanzibar moja kwa moja;
Mambo mingine 11 yamezidishwa kinyemela, pamoja na mafuta na gesi, na Profesa Shivji anasema yanavuruga mfumo wa Muungano wa 1964, na ni haramu na batili;
Ibara 64 ya Katiba ya Muungano wa 1977 imefunguwa mlango wa nyuma ya kuipora mambo mengine mengi ya Zanzibar, kama Bahari Kuu.
Tukiendelea na mfumo huu wa Muungano, mwisho wake Serikali ya Zanzibar itakuwa kete au kapu tupu
–
tutabakiwa na bendera na wimbo ya Taifa,
-
BLW itakuwa halina kazi ya kupitisha sheria;
-
SMZ itakuwa haina kazi ya kutawala nchi yetu;
-
tutakuwa na mawaziri wanaopunga upepo tu;
-
tutakuwa na rais wa pambo tu.
Basi
na tujiulize kwamba, Huko ndiko tunakotaka kwenda?
Suala
ni tuende wapi kutoka hapa kutatua ‘kero za Muungano’ zote.
Ni
dhahiri kutokana na uchambuzi wetu tutaona kwamba hizi sio kero za juu juu tu;
lakini ni matatizo na hata migogoro iliyosababisha kulazimishwa Rais Jumbe
ajiuzulu. Matatizo haya yanatokana na:
§ Muundo (structure)
wenyewe wa Muungano,
§ Tafauti kubwa ya kiwatu
na ya kieneo kati ya nchi yenye watu milioni moja na nchi yenye watu milioni
45,
§ Maslahi na uchumi
tafauti kati ya pande mbili,
§ Makosa yanayotokana na
dharau wanayoionyesha Serikali ya Muungano tunapolalamika,
§ Udanganyifu na
kutoaminiana pande zote mbili, n.k., n.k.
Hatuwezi
kuendelea hivi. Lazima tukubali kwamba kuna matatizo mengi sana. Katika miaka
48 ya Muungano tumeunda tume na tumeandika ripoti zaidi ya 40, bila kutatua
matatizo ya maana, na kila siku yanajitokeza matatizo mengine.
Sasa na tuwe majasiri kuandika Katiba Mpya ambayo itaweza kufikiria muundo muafaka na itakayoweza kukidhi mahitaji ya Zanzibar: serikali moja, mbili, tatu, Muungano wa mkataba, au nchi mbili hizi ziungane katika Shirikisho la Afrika Mashariki.
Pia jambo la msingi ni kuwashirikisha wananchi Wazanzibari juu ya suala la Muungano pekee. Wazanzibari hawajapata kushiriki kwa kuulizwa kuhusu Muungano, hivyo ni wakati muafaka kwa SMZ na Baraza la Wawakilishi kuwauliza Wazanzibari kuhusu Muungano. iIkiwa tunania njema na Zanzibar na Muungano wenyewe hili linawezekana na Katiba ya Zanzibar inaturuhusu kuwauliza jambo lolote la kitaifa wananchi kupitia Kura ya Maoni kabla ya kuingia kujadili na kupiga Kura ya Maoni kuipitisha hio Katiba Mpya ya Tanzania.
Sasa na tuwe majasiri kuandika Katiba Mpya ambayo itaweza kufikiria muundo muafaka na itakayoweza kukidhi mahitaji ya Zanzibar: serikali moja, mbili, tatu, Muungano wa mkataba, au nchi mbili hizi ziungane katika Shirikisho la Afrika Mashariki.
Pia jambo la msingi ni kuwashirikisha wananchi Wazanzibari juu ya suala la Muungano pekee. Wazanzibari hawajapata kushiriki kwa kuulizwa kuhusu Muungano, hivyo ni wakati muafaka kwa SMZ na Baraza la Wawakilishi kuwauliza Wazanzibari kuhusu Muungano. iIkiwa tunania njema na Zanzibar na Muungano wenyewe hili linawezekana na Katiba ya Zanzibar inaturuhusu kuwauliza jambo lolote la kitaifa wananchi kupitia Kura ya Maoni kabla ya kuingia kujadili na kupiga Kura ya Maoni kuipitisha hio Katiba Mpya ya Tanzania.
No comments :
Post a Comment