Maswali mengi Kadhia ya Sheikh Farid
KIONGOZI wa Taasisi za Kiislamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed ameonekana baada ya kupotea kwa siku nne katika visiwa vya Zanzibar huku akionekana kuwa na afya njema na furaha baada ya kuonana na familia yake iliyopo Mbuyuni Mkoa wa Mjini Magharibi.
Sheikh Farid ambaye kutoweka kwake kulizusha ghasia kubwa mjini Zanzibar tangu Jumatano iliyopita kwa vijana kupambana na polisi huku polisi mmoja akichinjwa na raia mmoja kuuawa kwa risasi ya moto alionekana juzi usiku saa 2:15.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Sheikh Farid nyumbani kwake Mbuyuni muda mfupi baada ya kufika kwa familia yake alielezea historia ya kukamatwa kwake ambapo alisema hakutekwa bali alichukuliwa na Jeshi la Polisi na vikosi vya usalama wakitaka kumhoji kuhusiana na harakati zake za kuitetea Zanzibar ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa kweli nazungumza neno kutoweka lakini mimi sikutekwa bali nilichukuliwa na watu ambao ni polisi na wakaniingiza katika gari na kunipeleka sehemu moja ambayo mimi nilikuwa siijui wakanifunga kitambaa machoni na kunipeleka sehemu nisiyoifahamu na kuniingiza katika nyumba yenye geti nikiwa na kitambaa cheusi usoni,” alisema huku akionesha furaha.
Sheikh Farid alipatikana saa 2:15 baada ya umeme kukatika ambapo kwa mujibu wa maelezo yake anasema alishushwa ndani ya gari kama mzigo kwa kusukumwa sehemu ile ile ambayo awali alichukuliwa na ametambua hilo baada ya kuona ameshushwa katika Msikiti ambao aliingia siku ya kwanza alipochukuliwa.
“Nilifungwa kitambaa cheusi na tokea nimefungwa sikufunguliwa mpaka leo (juzi) walipokuja kunitupa sehemu ile ile walionichukua ndio wakanifungua, na mimi mwenyewe sikuwa nimeweza kukifungua kwa muda wote huo kutokana na jinsi walivyokifunga,” alieleza.
Kiongozi huyo alilakiwa na viongozi wenzake wa Uamsho ambao walifika kumfariji na wakati anakumbatiana nao alikuwa anatokwa na machozi.
Awali kabla ya Sheikh Farid kuonekana viongozi wa Uamsho wakiwa na maofisa polisi walikwenda Mwangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja kuangalia kaburi ambalo lilionekana huko huku kukiwa hakuna taarifa za mtu aliyefariki dunia.
Naibu Amiri wa Uamsho, Azzan Khalid Hamdan alisema waliliona kaburi hilo jipya lakini kwa vile Sheikh Farid ameonekana hakukuwa na haja tena ya kuwasiliana na Mwanasheria ili kaburi hilo lifukuliwe.
Akizungumzia hali aliyoikuta huko ndani ya nyumba alipokuwa ameingizwa, Sheikh Farid alisema kwa kuwa alikuwa amefungwa uso hakuweza kutembea sehemu yoyote ndani ya hiyo nyumba na kwamba alikuwa akienda chooni kujisaidia na kurudi ambapo kwa muda wa siku tatu hajawahi kula chakula chohote zaidi ya kunywa maji alipokuwa akienda chooni.
“Sijala kitu chochote kwa sababu hiyo nyumba haikaliwi na mtu lakini hata kama ningeletewa chakula nisingekula kwa sababu siwezi kuwaamini kula chakula chao kwa hivyo nilichokuwa nafanya nikienda chooni kujisaidia ndio nakunywa maji ya mferejini kwa wingi sana na Alhamdulillah (nashukuru Mungu) amenisaidia,” aliongeza Sheikh huyo ambaye alikuwa amezongwa na umati mkubwa hapo nyumbani kwake.
Alisema katika kipindi hiki alichokamatwa hakuwahi kupigwa hata mara moja wala hajadhuriwa kwa hali yoyote zaidi ya kutiwa hofu wakati akifanyiwa mahoajiano na baadhi ya wakati alikuwa akihojiwa kwa hasira na ukali ili atoe maelezo yote kuhisiana na harakati zake na masuala mengi yalikuwa yakimlenga yeye binafsi, uhusiano wake na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na uhusino wake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na safari zake za kwenda na kurudi nchini Oman.
“Safari hii kunipiga hawajanipiga hata mara moja Alhamdulillah lakini walilokuwa wakitaka kujua masuala yangu binafsi maana walichukua simu yangu na kila kitu changu na walitaka kujua hizi harakati zetu tunazofanya walitaka kujua na katika masuala yao walikuwa wakiniuliza zaidi masuala yangu binafsi, harakati zangu, uhusiano wangu mimi na viongozi wa serikali lakini pia walitaka kujua hizi safari zangu za kwenda Oman na kwa ufupi walitaka kujua kila kitu,” alisema na kuongeza kwamba: Simu yangu hawakunirudishia”.
“Walitaka kujua kila kitu changu na kwa kweli walikuwa wanataka kujua kila kitu na ilikuwa ni vitisho na baadhi ya wakati walikuwa wakipiga risasi miguuni ili watimize lengo lao wanalolitaka,” alisema kiongozi huyo ambaye maarufu anaitwa Simba huku akionesha huzuni.
Alisema watu waliokuwa wakimhoji walikuwa wakitofautina kwa kuwa kila mmoja alikuwa akitumia namna yake ya kuhoji ambapo wengine wakitumia ukali na wengine wakihoji kwa utaratibu na upole.
Akiendelea mazingira ya nyumba hiyo aliyowekwa alisema ni hofu ilikuwa imetanda lakini aliweza kuvumilia katika kipindi chote hicho kwa kuwa hakuwa akiona kitu chochote kwa kuwa alikuwa amefunikwa uso wote.
Akitoa wito wake kwa umma akiwataka watulie na wasifanye fujo huku ombi lake kwa viongozi wa serikali ni kutenda uadilifu na wawe wanafuata kauli zao kivitendo na sio kusema bila ya kutenda haki kwani amani haiwezi kudumishwa iwapo watu wanayimwa haki.
“Naomba watu watulie wasifanye fujo na wasifanye vurugu za aina yoyote lakini hizi ni awamu za kudai haki lakini wawe na subira kwani hii ni nchi yetu na tunaipenda na tutaitetea kwa nguvu zote na wito wangu kwa viongozi wa serikali wawe waadilifu na watende haki kwa sababu hii ni nchi yetu na hizi ni awamu za mabadiliko na asiyetaka mabadiliko basi wakati utambadilisha akitaka asiteke,” alisema.
Sheikh Farid alisema licha ya vitendo vyote hivyo lakini hatarejea nyuma kamwe na ataitetea Zanzibar hadi tone lake la mwisho kwani anachokifanya yeye na wenzake ni kitendo kinachokubalika kisheria na hakuna wa kuwazuwia.
“Tutaitetea nchi yetu ya Zanzibar hadi tone la mwisho kwa sababu tunachokifanya hatujavunja sheria wala hatujaenda kinyume na sheria za nchi kwa hivyo tutaitetea Zanzibar mpaka iwe na dola kamili na mamlaka kamili haiulizwi na mtu na irudi katika hadhi yake kama 1963,” alisema Sheikh Farid.
Akitoa maelezo ya kukamatwa kwake alisema kwamba awali alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wake wa Madrassa ya Mahdi Mahfoudh kwamba anataka kuonana naye na kumtaka waonane katika eneo la Mbweni karibu na duka ambapo mbele yake kuna msikiti mdogo usiosaliwa na watu wengi.
“Mimi napigiwa simu na watu mbali mbali kwa hivyo nilipopokea simu kuwa mwanafunzi wangu wa Mahdi Mahfodh sasa wakati huo natoka nyumbani nilikuwa nahitaji umeme kwa hivyo mimi nilipofika pale nikamwambia yule kijana wangu kwamba nataka kununua umeme na nikamwambia kijana nenda kanunue umeme na mimi naingia humu msalani kujisaidia sasa yule kijana akaondoka kwenda kununua umeme, kile kitendo cha yule kijana kuondoka tu na mie ndio nimetoka chooni naona gari ndio hiyo imekuja imepaki na kuna mtu mmoja akashuka akaniita Maalim na akajitambulisha pale kwamba mimi ni askari wa usalama na naomba uingie humu ndani ya gari tunataka kukuhoji na ndipo wakati huo huo watu wengine wawili wakashuka ndani ya gari wakiwa wamejifunika nyuso zao vitambaa vyeusi isipokuwa macho wakiwa na bunduki …sasa mimi sikutaka tena nikimbie au vipi kwa sababu ningekataa pengine ingekuwa ni hatari zaidi sikuwa na sababu ya kukataa nikaingia ndani ya gari na nilipoingia tu nikafungwa kitambaa, gari ikaondoka,” alisimulia mkasa huo Sheikh Farid.
Alisema baada ya kuingia ndani ya gari gari hiyo haikurudi nyuma ilionekana inakwenda njia ya Uwanja wa Ndege kwa kuwa ilikuwa imeelekea huko na kisha kupita ’round about’ kama mara sita ili kumpotezea lengo asifahamu wapi anapelekwa na kuanzia hapo hakuweza kujua wapi anapelekwa hadi hapo alipofika katika nyumba na kuwekwa huko kwa muda wote akiwa amefunikwa uso wake na hajafunguliwa hata mara moja zaidi ya siku ambayo amerudishwa sehemu ile ile na kutupwa kwa kusukumwa tu ndani ya gari.
Muda mfupi baada ya taarifa hizo kuenea kwamba Sheikh Farid ameonekana watu mbali mbali walikuwa wakitumiana ujumbe kwa njia ya simu na facebook wakiulizia alipo ili wamuone kwa macho yao na ndipo Sheikh Farid alipotoka hapo alipotupwa alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa mama yake eneo la Malindi ambapo alikutana na watu mbali mbali na kusalimiana nao na kisha akashauriwa kwenda Mbuyuni kwa mke wake mmoja ambaye anaishi enoeo hilo karibu na Msikiti wa Mabuyuni karibu na uwanja wa mpira wa Malindi.
Muda mfupi waumini wa dini ya Kiislamu walimiminika kwa wingi sana na kukaa nje ya geti la nyumba wa Sheikh Farid hapo Mbuyuni wakitaka kumuona kwani wengi wao walikuwa hawaamini kama angeachiwa akiwa hai kutokana na taarifa za awali zilizokuwa zikisambazwa kwamba Sheikh huyo amefariki dunia kwa kupigwa sindano ya sumu na wanajeshi jambo ambalo halikuthibitishwa na chombo chochote nchini.
Waumini wa kike na wa kiume, wakubwa na watoto kwa wingi walikusanyika huku wakisikika wakimsifu na kumshukuru Mwenyeenzi Mungu kwa kumrejesha kiongozi wao salama kwa kutoa neno la Takrbir …yaani Mwenyeenzi Mungu Mkubwa na kisha kuimba wimbo wa kumpongeza na kusema Simba ……ameachiwa …Simba ameachiwa…Simba ameachiwa ambapo kulikuwa na ngoma za dufu zikipigwa na wengine kuitikia.
Wakati waumini hao wakiwa nje ya geti na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki) wakiwa ndani waumini hao walikuwa wakipiga makelele kila mara wakimuomba Sheikh Farid atoke achungulie ili waweze kusalimiana nao ambapo baadhi ya wakati walikuwa wakipenya na kuingia ndani kwa lengo la kutaka kukumbatiana naye na kupiga picha.
Katika mitandao ya facebook watu wengi hasa vijana wameweka picha zao wakiwa wamepiga pamoja na Sheikh Farid huku wengine wakibadilisha maelezo yao na kumuweka picha yake huku wengine wakisema huyo ndio shujaa wanayemtaka kuwa kiongozi wa nchi yao.
Waumini hao walibakia hapo kwa muda na hata pale walipoambiwa kwamba amechoka na hangeweza kutoka nje walisema shida yao wamuone japo akiwa huko juu ya nyumba yake muhimu achungulie nje ili kuwatolea mkono na kila baada ya muda alikuwa akisimama na kuchungulia huku akishangiliwa na baadae waumini hao walitoka kidogo kidogo na kufanya maandamano yao huku wakiimba wimbo wao wa Simba ametolewa na kuelekea katika barabara zote za mjini huku wakipiga dufu.
Hali ya mji wa Zanzibar jana ilianza kurudi kwenye hali ya kawaida kwa wafanyabishara kuanza shughuli zao na magari ya abiria yakiwa yamejaa katika kituo kikubwa cha magari cha Darajani mjini hapa.
Wakati jana mchana hakukuna na gari hata moja Darajani jana hali ilikuwa nzuri na watu walianza kumiminika mjini kufanya shughuli zao.
Kwa muda wa siku tatu kuanzia Jumatano hali ilikuwa ya mtafaruku katika mji wa Zanzibar kufuatia kutowekwa kwa kiongozi huyo wa taasisi ya dini ya Kiislamu kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana.
No comments :
Post a Comment