CUF, CCM sasa ni jino kwa jino
11th October 2012
Makungu aliapishwa mbele ya Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho, saa 3:10 asubuhi baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa Bububu uliofanyika Septemba 16, mwaka huu.
Mara baada ya Spika Kificho kuanza kutangaza ratiba ya kuapishwa kwa mwakilishi huyo, ghafla mawaziri wa CUF na wawakilishi wake, walisimama na kuanza kutoka nje ya ukumbi.
Tukio hilo liliwafanya wawakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuimba `CCM... CCM...CCM...CCM'.
Hata hivyo, mawaziri wawakilishi hao wa CUF, walirudi ukumbini muda mfupi baada ya kukamilika kwa kazi ya kuapishwa kwa mwakilishi huyo.
Akizungumza na NIPASHE, Mnadhimu wa CUF katika Baraza hilo, Abdallah Juma Abdallah, alisema wameamua kususia tukio la kuapishwa mwakilishi huyo kwa vile hawamtambui kwa madai uchaguzi hakuwa huru na wa haki.
Alisema uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa taratibu na sheria za uchaguzi, jambo ambalo ni kinyume cha misingi ya utawala bora.
Hata hivyo, alisema CUF tayari imemshauri aliyekuwa mgombea wake, Issa Khamis Issa, kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi na tayari amekata rufaa Mahakama Kuu tangu Septemba 25, mwaka huu.
“Tumeamua kususia kushuhudia akiapishwa. Hatuwezi kuvumilia uchafu ukifanyika katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa,:”alisema Abdallah, Mwakilishi wa Jimbo la Chonga, Pemba.
Kuhusu kufanya naye kazi za Kamati Makungu, alisema iwapo Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) litamteua katika kamati za Baraza hilo, watafanyanaye kazi kwa kuzingatia kuwa kazi ya uteuzi siyo jukumu lao.
“Tutaendelea kutomtambua Makungu hadi Mahakama itakapotoa hukumu yake tena iwe ya haki,” alisema Mnadhimu huyo wa CUF.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa, Makungu alisema kazi moja tu ambayo ipo mbele yake ni kutekeleza ahadi za kutatua kero za wananchi.
Alisema maeneo mengi katika jimbo hilo yanakabiliwa na ukosefu wa huduma ya maji ya uhakika na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kutafutia ufumbuzi wa matatizo hayo.
Hata hivyo, alisema hana hofu yoyote na kitendo cha mpinzani wake kukimbilia mahakamani kwa kuamini kuwa yeye ndiyo mshindi halali katika uchaguzi huo.
Alisema vurugu zilizotokea katika uchaguzi huo, zilisababishwa na wafuasi wa Uamsho na CUF walikuwa wakiwazuia wanachama wa CCM kwenda katika vituo kupiga kura kabla ya vyombo vya ulinzi kuwatawanya.
“Sina hofu wala shaka, naamini mie ndiyo mshindi halali, sasa mwanga wa maendeleo ya Jimbo la Bububu umefunguka,” alisema Makungu.
Hata hivyo, alisema amesikitishwa na kitendo cha mawaziri wa CUF kumsusia wakati akiapishwa huku wakiwa ni viongozi wa serikali siyo chama cha siasa.
“Tukio la mawaziri wa CUF kunisusia, limenisikitisha naliona sawa na tukio la ubaguzi dhidi yangu wao ni viongozi wa serikali hawakupaswa kufanya hivyo,”alisema Makungu.
Kuhusu shughuli ya kuapishwa kutoonyeshwa na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Zanzibar Cable, Spika Kificho alimtaka Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk kueleza chanzo cha kutokuonyeshwa kwa shughuli hiyo.
Kificho alisema kazi ya kuapishwa kwa mwakilishi huyo ilikuwa ikifuatiliwa na wananchi kupitia televisheni na kitendo cha kutoonyesha, kimewanyima haki ya kushuhudia wakiwemo wananchi wa Jimbo la Bububu.
Mgombea huyo alisindikizwa kuapishwa kwa mbwembwe za msafara mkubwa wa magari yakiwa yamewabeba wana-CCM walivalia sare huku wakiimba nyimbo za kukitukuza chama chao.
Utaratibu wa kususia vikao vya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, uliibuka kwa mara ya kwanza mwaka 1995 kama shinikizo la kutomtambua Rais wa Zanzibar wakati huo kabla ya maridhiano ambayo yameleta Serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba, 2010.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment