"Mara nyingi nimetoa maelezo kulaani vitendo vya kuonewa watu mbalimbali. Hata Mhe. Freeman Mbowe alipokamatwa na kuwekwa ndani kwa kisingiziyo cha kutohudhuria mahakamani na nikaenda kumtazama Central Police Station. Kila mtu ana haki ya kuunga mkono chama na wanasiasa anaowapenda lakini si vyema kupotosha na kujenga chuki". Aandika Prof Lipumba kwenye blog moja nchini.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: WATANZANIA TUSIKUBALI KUINGIZWA KATIKA MAPAMBANO YA KIIMANI
Nchi yetu imeingia katika mgogoro na mtafaruku mkubwa baada ya kijana mmoja kukojolea kitabu cha Qur’an tukufu maeneo ya Mbagala na kufuatiwa na baadhi ya makanisa hapa nchini kuharibiwa na kuchomwa moto. Kwa Waislam kitendo cha kuinajisi Qur’an ni udhalilishaji wa hali ya juu na vyombo vya dola vinapaswa kuelewe kuwa hisia za Waislam wengi zinaathiriwa sana na kitendo hicho. Hatua za haraka za kumkamata na kumuhoji kijana aliyehusika na kutoa maelezo kwa umma kuwa suala hili linashughulikiwa ipasavyo kungewatuliza wananchi wengi. Kuchelewa kuchukua hatua kulitoa mwanya kwa watu wengine na vibaka kuvamia Makanisa kupora, kuyaharibu na kuyachoma moto. Kitendo hiki kimewaumiza, kuwakasirisha na kuwafadhaisha Waumini wa Makanisa hayo na Watanzania kwa ujumla.
CUF Chama Cha Wananchi kinalaani vikali kitendo kilichofanywa na kijana kunajisi Qur’an tukufu. Huku ni kuporomoka kukubwa kwa maadili ya vijana wetu. Kitendo cha kijana huyu kilipaswa kuchukuliwa hatua mara moja baada ya taarifa kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
CUF Chama Cha Wananchi kinalaani vikali kitendo kilichofanywa na kijana kunajisi Qur’an tukufu. Huku ni kuporomoka kukubwa kwa maadili ya vijana wetu. Kitendo cha kijana huyu kilipaswa kuchukuliwa hatua mara moja baada ya taarifa kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Kitendo cha kijana huyu hakihalalishi kwa namna yeyote ile kuvamia makanisa, kuyapora, kuyaharibu na kuyachoma moto. CUF Chama Cha Wananchi kinalaani vikali vitendo vya kihalifu na vya kuchochea mfarakano ndani ya jamii vilivyofanywa na watu na vibaka waliovamia makanisa haya. Tunawapa pole Waumini wote walioathirika na matukio haya.
Baada ya matukio ya kuharibu makanisa, polisi walieleza wamewakamata watu waliohusika na vitendo hivyo na kuwa watawafikisha Mahakamani. Rais Kikwete alienda kukagua makanisa yaliyoathirika na kuwapa pole waumini wa makanisa hayo. Hii ilikuwa hatua ya mwanzo yakulirudisha taifa katika maelewano.
KUSHIKWA KWA SHEIKH PONDA
Katika hali hii ya kuvurugika kwa amani kulikochangiwa na vyombo vya dola kutochukua hatua za haraka dhidi ya kijana aliyeinajisi Qur’an, polisi walimkamata Sheikh Ponda. Vyombo vya Habari vimemnukuu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akieleza pamoja na mambo mengine kuwa Sheikh Ponda “Amekuwa akifanya maandamano kinyume cha sheria na hata kutishia umwagaji damu Dar es Salaam, kipindi chote tulikuwa katika uvumilivu wa kufuatilia nyendo zake kila kukicha,...licha ya hali hii, Oktoba 12, mwaka huu, Ponda pamoja na wafuasi wake, walisababisha kuvunjwa makanisa usiku wa manane, uharibifu wa magari na wizi na upotevu wa vifaa katika makanisa… haya yote yameongozwa na Ponda na madhara yake ni makubwa.” (Mtanzania ALHAMISI, OCTOBA 18, 2012 05:06)
Unaweza usikubaliane na Sheikh Ponda katika maelezo na msimamo wake kuhusu dhulma dhidi ya Waislam, lakini ni makosa makubwa kumsingizia mambo ambayo hakuyatenda. Kwa jeshi la polisi kutoa shutuma hizi ambazo hazina msingi wowote kunaongeza mfarakano ndani ya jamii.
Hata hivyo kesi aliyoshitakiwa Sheikh Ponda ni ya kuvamia kiwanja kisochokua chake. Kiwanja ambacho Sheikh Ponda anadaiwa kukivamia ni kiwanja kilichokuwa kinamilikiwa na East African Muslim Welfare Society kwa madhumuni ya kujenga Chuo Kikuu cha Kiislam. Baada ya serikali kuivunja East African Muslim Welfare Society na kuanzisha BAKWATA, mali zake zilikabidhiwa BAKWATA. Anachodai Sheikh Ponda ni kuwa kiwanja hicho cha Waislam kimeuzwa kinyume cha utaratibu na sheria zinazolinda mali ya Waqfu.
Kesi ya viwanja ni ya mahakama ya ardhi. Mwenye kiwanja alistahiki kwenda mahakama ya ardhi na kueleza kuwa kiwanja chake kimevamiwa. Kutumia polisi wa FFU kumkamata Sheikh Ponda kwa tuhuma za kuvamia kiwanja ni kitendo ambacho kimechochea vurugu. Matamshi ya Kamanda Kova yakumuhusisha Sheikh Ponda na uchomaji wa Makanisa jambo ambalo hakuhusika nalo na kutoa wito kwa wafuasi wa Sheikh Ponda kujisalimisha polisi ndilo lililochochea maandamano ya Ijumaa tarehe 19 Oktoba 2012.
Jeshi la Wananchi ni la kulinda mipaka yetu siyo la kwenda kupiga raia wanaoandamana. Kitendo cha kuwaingiza barabarani wanajeshi kupambana na raia ni kitendo cha aibu na cha kusikitisha. Serikali iepuke kujenga uhasama kati ya Jeshi la Wananchi na raia.
Kitendo cha kumnyima dhamana Sheikh Ponda na wenzake siyo cha haki.
Kuinusuru nchi isingie katika mgogoro, Sheikh Ponda na wenzake wapewe dhamana. Hiyo ni haki yake yao ya msingi. Mwenye kiwanja apeleke malalamiko yake mahakama ya ardhi na kesi hiyo ya kiwanja ihamishiwe huko.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, Rais Kikwete alizungumzia mgawanyiko wa kidini uliotokea wakati wa uchaguzi. Hata hivyo hajachukua hatua zozote za kuleta maelewano ya kujenga utamaduni wa kuvumiliana baina ya Watanzania wenye imani tofauti. CUF Chama Cha Wananchi kinatoa wito kwa Watanzania kuwa na mjadala wa kujenga mahusiano mazuri na kuvumiliana baina ya dini na madhehebu hapa nchini. Mijadala hii ifanyike katika ngazi ya kitaifa na katika maeneo ya wananchi na yahusishe viongozi wa dini wa taasisi zote, vyama vya siasa na vyama vya kijamii kwa lengo la kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuvumiliana na kuheshimiana. Watanzania wote wajisikie kuwa ni raia wa daraja la kwanza katika nchi yao.
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti - CUF
No comments :
Post a Comment