Wednesday, October 17, 2012
Taarifa ya Serikali kuhusu Vurugu
iliyotokea leo
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli
zao kama kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali
ya ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa leo usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado
ni shwari na inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu.
Akizungumzia tukio la vurugu zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri
Mohamed Aboud alisema vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi
wa Sheikh Farid Hadi walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani,
Michenzani, Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh wao haonekani
na kudhani amekamatwa na vyombo vya Dola na kuwekwa ndani.
Waziri Mohamed Abud alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya
Dola ikiwemo Polisi,Jeshi la wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa,
Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo,
Zimamoto na Valantia ambapo vyombo vyote hivyo vimeeleza kutoelewa
chochote kuhusu Sheikh Farid.
Waziri huyo alisema kwamba Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya
kutoonekana kwa Sheikh Farid ambapo kwa sasa Jeshi hilo linaendelea
kumtafuta na kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ili kupata ukweli wake
na kuchukua hatua zinazofaa.
Alisema kwamba wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wake,
wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi
au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.
Waziri Mohamed Aboud amesema Serikali inawasihi wwananchi waache
kujiingiza katika vitendo vya fujo na vurugu kwani kutenda hivyo ni kosa
kwa mujibu wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo.
Katika tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa
Sheikh Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto
Maskazini za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu
miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
17/10/2012
ZANZIBAR,TANZANIA
Source: Zanzinews
No comments :
Post a Comment