Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 28, 2012

Zanzibar kurejea tena kwa Bamkwe


Kulia ni Sheikh Azzan Khali Hamdan katika kati ni Sheikh Farid Hadi Ahmed na kuchoto ni Sheikh Mussa Juma Issa ambao wote wapo ndani wakishitakiwa kwa kosa la kusababisha vurugu na kuharibu hali ya usalama wa nchi, kesi yao hawajapewa dhamana. nyuma ni Rashid Ahmed (Joe) Ali Saleh


Kovu za majeraha yaliyowapata na adhari za bakora zilizoachwa katika miili ya Wazanzibari bado zipo bada ya miaka arobaini na nane ya mapinduzi. Kovu za majaraha hayo yaliyoachwa na Field Marshal Okello na kundi lake kwa upande mmoja na athari za bakora za akina Rashid Abdulla Mamba kwa upande mwengine bado zinatukumbusha wapi tumetoka. Ilikuwa ni zama za ujahilia nguvu na amri zilitawala na sharia pamoja na utawala wake vikapewa kisogo.
Kipindi hiki ni kipindi kilichoacha kiza katika historia ya Zanzibar. Kuna wale ambao wamepotea ndani ya mikono ya serikali na mpaka leo hii serikali imeshindwa kutoa kauli kuhusu wapi wapo watu hao, akina Abdu Nadhif, Abdulla Kassim Hanga, Othman Shariff, Jaha Ubwa na wengineo wengi.
Wazanzibari hawa hawakuwahi kuhukumiwa kifo na Mahkama wala hata hawakuwahi kufikishwa Mahkamani na kuambiwa kosa ambalo washitakiwa nalo. Kimya hiki cha kutojua khatima ya watu hawa na wengi wengine kina ashiria kwamba watu hawa wameuwawa nje ya mahkama (Extra judicial killings), kwani kama watu hawa wako hai basi miaka arobaini na nane sasa hawajaletwa mbele ya Mahkama kufunguliwa kesi au angalau kujulikana wapi wapo na kama wapo basi waarifiwe watu wao kuwa wako hai.
Watu wanasema tusikumbushe kilio matangani, lakini kama hujakumbusha kilio matangani utakikumbushia wapi?. Sio kila anaelia matangani anamlilia marehemu au maiti anaesubiri kuzikwa au aliezikwa basi wapo wengi wanaokumbuka ndugu na jamaa zao ambao walishatangulia na msiba huo au tanga hilo huwa linawakumbusha msiba wao pia.
Jengine waswahili tuna msemo wetu wa Kiswahili kama ilivyo katika lugha zote , tunasema “ilopita si ndwele tugange ijayo”, ndio hili tunataka kulizungumza. Matokeo ya utekaji nyara watu na kufichwa kwa kutuhumiwa kuwa wamekiuka sharia. Mambo haya ya utekwaji nyara watu na watu wa usalama yalikithiri na kushamiri katika Awamu ya Kwanza ya Rais Karume na kuendelea hata katika Awamu ya Pili ya rais Aboud Jumbe, ambapo Jumbe aliweza kidogo kidogo kukomesha hilo.
Tunakumbuka vyema utekaji nyara uliokuwa ukifanywa na usalama na kuwafanya Wazanzibari kutokuwa na raha wala buraha na kuwatia khofu watu katika majumba yao hata kufikia hadi kusema chumvi imeadimika unaogopa kusema kwa kuhofia na wewe kutiwa ndani, Kwani wapo waliotiwa ndani kwa kusema bidhaa fulani imeadimika.
Hiyo nyara inayotekwa mtu haiishi kituo cha polisi bali moja kwa moja “kwa Bamkwe” na huku ndio utakiona kilichomtoa kanga manyoya. Mateso ya kwa Bamkwe hayasimuliki kwani baada ya mateso huwa kuna kiapo kwa kutakiwa kuwa hayo mambo na mateso ya kwa Bamkwe usiyasimulie uyawache hapo hapo. Lakini binaadamu hawezi kujizuiya na hasira na kila akijitizama bakora za Bamkwe zilizoota mgongoni kama alama za punda milia anakumbuka mateso ya Bamkwe. Mwisho humtoka yale ya kule kwa Bamkwe.
Naam ilifika hata watu kususia gari ya Taxi ya mmoja kati ya hao walokuwa wakitesa wtu. Wapo wengi hao Bamkwe wengine wamefikia kuwa na nafasi kubwa serikalini na wanajulikana.
Leo hii tunazungumzia kutekwa nyara kwa Sheikh Farid Hadi Ahmed. Kesho atatekwa mtu mwengine au kiongozi mwengine, hili si la kulinyamazia. Dola inayofuata utawala wa Sheria na kuzingatia huru binafsi na haki za kibinaadamu haiwezi kukaa kinya na kuacha hali hii ikaendelea. Leo Sheikh Farid kesho mwengine, hawa wanaoteka nyara watazoea ni lazima wawajibishwe kama kweli tunataka kweli kusimamisha Utawala wa Sheria na kulinda Haki za Binaadamu. La vyenginevyo tutakuwa tukiimba wimbo wa Komandoo Salmin Bin Amour , SHERIA, SHERIA , SHERIA. Vyenginevye itakuwa ni jina tu la mzee sharia uzia.
Komandoo, Salmin alijilabu sana na wimbo wake wa SHERIA ,SHERIA, SHERIA, lakini kwa kweli ni katika kipindi chake utawala wa sharia na kulindwa haki za binadamu havikuwepo.
Tutamkumbuka Salmini na maskani zake ambazo alikuwa akizifadhili. Huku zikitukana na kuvunjia heshima watu pamoja na kujingiza katika vitendo vya uvunjivu wa haki za binaadamu, si hao tu bali hata wale vijana wa “JANJAWID” ambao walikuwa wanatumiliwa kuingia majumbani na wengine kupelekwa Pemba kuwaadhibu watu na kuwaibia. Tutamkumbuka pia Komando kwa kupandikiza mbegu ya fitna na chuki ya Upemba na Uunguja na mengi mengineyo.
Wazanzibari tusikubali kurejeshwa tena nyuma kule kwa “BAMKWE’ na kina FUMU pamoja na JANJAWID, tusiruhusu uhalifu huu unaotaka kurudi tena. Tudumishe ustaarabu wetu pamoja na ustaarabu wa kuimarisha UTAWALA WA SHERIA na Kusimamia HAKI za Binaadamu.
Utaratibu wa kufunguliwa kesi upo sasa ya nini haya ya kutekwa nyara. Kama mtu anashukiwa kuvunja sharia za nchi basi utaratibu wa sharia utumike katika kumshughulikia na sio kufanya vitendo vya uharamia vya utekaji nyara watu. Hili lisipite ,lilaaniwe kwa nguvu zote na serikali lazima lifanye uchunguzi.
Baraza la Wawakilishi lazima liitake serikali kufanya uchuguzi. Tusikubali kurejeshwa tena kwa BAMKWE. Utekaji nyara umefanyika Mrima haukuchunguzwa hiyo umepita bila kulaaniwa sasa umevuka bahari nakuja tena visiwani, Wazanzibari tulikuwa tumeshasahau watu kusombwa usiku na kutiwa ndani ya vigari vya usalama kwa kupelekwa kwa BAMKWE sasa haya yanarudi tena.
Tukiyanyamazia na kusema aah ni huyo Sheikh Farid wa Uamsho basi tutakuwa tumekosea kwani huu ni mwanzo leo Farid kesho mwengine Vuai Ali Vuai wa CCM au Ismail Jussa Ladhu wa CUF. Vitendo viovu haifai kupewa fursa kukujichomoza na kumea katika jamii hasa vile tunaamini na kukubali Utawala Bora pamoja na kulinda Haki za Binaadamu. Maandiko ya Kusimamia Utawala Bora na Hifadhi ya Haki za Binaadamu Katika Katiba yatakuwa hayana maana ikiwa yatabaki katika kurasa za Katiba bila ya kusimamiwa na kutekelezwa.

  1. Chanzo: ZanzibariYetu

No comments :

Post a Comment