31/10/2012
BAADHI ya watu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wanadhani kwamba wanatawala badala ya kuongoza, ndio maana pamoja na tambo za majigambo na porojo nyingi majukwaani, bado hali halisi inawasuta kuhusu suala zima la Wazanzibari kutaka mabadiliko katika muundo wa Muungano.
Miongoni mwa wana CCM hao, wengine ni viongozi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) wanafikiri ukiwapo Muungano wa mkataba hawataukwaa tena ukubwa, na kwa dhana hiyo wanaamini ili waendelee kubaki kwenye madaraka watatumia vitisho vya kuwavua uanachama wenzao kwa kisingizio cha kuyasaliti Mapinduzi, au kwamba wanataka kuvunja Muungano.Mara nyingi wapo madarakani kutetea maslahi yao na matumbo yao pekee kiasi kwamba wanadiriki hata kusahau kwamba kinachowafanya waitwe viongozi ni kwa sababu ya Uzanzibari wao, na wala si kitu kingine.
Watetezi wa mfumo wa sasa wa Muungano wanashindwa kuisemea Zanzibar katika kugawana rasilimali ya gesi asilia ambapo tangu kuanza kupatikana katika Mikoa ya Tanzania Bara, Zanzibar haijapata hata senti moja licha ya kuelezwa na kuandikwa kwenye katiba ya sasa kwamba jambo hilo ni la Muungano.Wazanzibari wanaotaka Muungano wa mkataba wana hoja na kwa sababu ya hoja yao ndio maana kila siku idadi ya waumini wa mfumo huo wamekuwa wakiongezeka. Ipo siku hali halisi itawasuta, ingawa hawatasutwa hadharani, lakini watajisuta wenyewe kwenye nafsi zao pale ambapo raia watakapoamua kuachana na muundo mkongwe wa Muungano na kuingia katika mfumo mpya.
Tunampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kuunda Tume kuwauliza wananchi wanataka Katiba ya aina gani au iliyopo iendelee. Huu ulikuwa uamuazi wa busara kwa Mkuu wa nchi, hata hivyo tunashangazwa na virukia waliochipuka kutaka kuwashurutisha wananchi kusema au kutoa maoni ambayo sio wanayoyaamini wananchi.
Ikiwa Serikali imeunda Tume ya kuchukua maoni ili kukuza demokrasia katika nchi, vipi wazuke watu wanaotaka kuichezea demokrasia kwa kulazimisha jambo ambalo kila mtu ana haki nalo kulitoleaa maamuzi? Ikiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa ameeleza bayana siku ile alipozindua Tume ya Jaji Warioba pale Ikulu, Dar es Salaam kwamba kila mmoja awe huru kutoa maoni yake na wala usichukie pale mwenzako anapotoa maoni ambayo wewe hayakupendezi maana hata yako pia kuna watu hawayapendi, kwanini watu walazimishwe kutoa maoni ya aina fulani?
Katiba ya nchi katika nchi yoyote ya kidemokrasia ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya wananchi na hivyo ni wananchi pekee ndiyo wenye haki ya kuibadili na sio genge kama la mahafidhina ambalo halina haki kuwashurutisha raia wenzao kufuata matakwa yao.
Na kama si hivyo, hizi chuki za wazi zinazooneshwa dhidi ya wananchi wa Zanzibar sababu yake nini? Sauti tunazozisikia kutoka kwa mahafidhina kila kukicha ni kwa niaba na maslahi ya nani? Na kama watadai kuwa wanatumia haki yao ya msingi kama raia katika kutoa maoni kuhusu mambo ya nchi, ni lini wananchi wa Zanzibar walinyang’anywa haki hiyo ili wasiwe na uwezo wa kufanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale wanapoona inafaa kama hili la kutaka Muungano wa mkataba.
Hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya Watanzania na si vinginevyo, ni Wazanzibari na Watanganyika pekee wenye haki ya kuibadili, na sio kiongozi wa Chama cha Siasa, muhafidhina atakayeweza kutoa agizo la kuzuia nguvu ya umma kutoa maoni wayatakayo.
Ni kawaida ya wakati kuwa ndio muamuzi wa kweli na huu ni wakati wa ukweli na uwazi, kwa hivyo ni wakati muafaka kuachana na tabia ya ubabe,vitisho na kusingiziana mambo yasiyokuwepo. Tuachane na ngonjera, Propaganda za wanasiasa vitimbakwiri.
Katiba ya Tanzania ni ya wananchi wote na katu si ya chama tawala cha CCM, hivyo si sahihi suala la mabadiliko ya kabla ya nchi yakafanywa ni agenda ya kujadiliwa na kuamuliwa na wana-CCM tu kwani CCM kwa sasa sio tena Chama Dola, ule wakati wa Chama Dola ulishapita tangu mwaka 1992.
Azma ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya muundo wa Muungano kuwa wa mkataba ni jambo ambalo halina ubishi kuwa lina mantiki ndani yake na wala isichukuliwe kuwa ni usaliti wa Mapinduzi au mfumo wa Muungano wa kikatiba. Tumesikia maoni yaliyotolewa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipokutana na Tume ya Jaji Warioba walipotaka mamlaka kamili ya Zanzibar.
Wadadisi wa mambo Zanzibar wanasema hawakuamini pale walipowasikia baadhi ya Wawakilishi wa CCM wakiitetea nchi yao kutaka mamlaka kamili.Pengine kilichowafanya kuchukua uamuzi mgumu na sahihi ni uzalendo wao kwa Zanzibar maana pamoja na yote hayo wao watabaki kuwa Wazanzibari maana Muungano umekuja baadaye tu, Zanzibar ilikuwepo, itakuwepo na itaendelea kuwepo iwe katika Muungano au nje ya Muungano.
Suala linaloulizwa kigenge cha mahafidhina kinasimamia upande upi ikiwa Mnadhimu na Mjumbe wa Kamati Kuu anapendekeza Zanzibar isimamie yenyewe uhusiano wa kimataifa na mamlaka kamili ya uendeshaji wa mambo yake kama vile kujiunga na OIC, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Shamsi Vuai Nahodha anataka orodha ya mambo ya Muungano kupunguzwa na pia gawio la asilimia 4.5 Zanzibar liongezwe hadi angalau asilimia 15, wewe mpigakura wa Pongwe, Kinduni, Matemwe, Kitope,Wawi, Chake Chake, Umbuji na kwingineko unasubiri nini kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar?
A
u kwa kuwa wengi wanaounga mkono mabadiliko ya muundo wa Muungano ni watu walioanzisha na kuunga mkono maridhiano ya kisiasa Zanzibar yaliyosababisha marekabisho ya 10 ya Katiba yaliyozaa SUK, hivyo kuendeleza hulka ya kupinga hata kwa jambo zuri lenye manufaa kwa nchi?
Genge hili naliona ni lenye donge dhidi ya watu wenye fikra ya mabadiliko katika siasa za Zanzibar na wengine wana chuki binafsi na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad ambao ni manahodha wa maridhiano ya kisiasa Zanzibar yaliyosabisha nchi kupata utulivu wa kisiasa.
Kundi la pili, ni wale watu hasa wa upande wa Tanganyika wasiopenda kuona Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili, hawataki kuitambua kuwa Zanzibar iliingia katika Muungano mwaka 1964 ikiwa ni nchi yenye mamlaka kamili na kwamba iliingia kwa makubaliano na siyo kutekwa au kulazimishwa na kubaki na mamlaka ya mwisho juu ya masuala fulani chini ya Serikali yake.
Huu si wakati tena wa wanasiasa, wasomi, wakulima, wafanyakazi au wakwezi kuendelea kukwepa ukweli, lazima tubadili mambo kutegemea na wakati uliopo, muundo wa Muungano wa mkataba ndio tiba sahihi kwa Muungano wetu, na ikiwa kuna watu wa kulaumiwa katika hali hii ya udhaifu wa muundo wa Muungano tuliyonayo ni wale waliochangia au kusababisha kuwepo kwa hali.
Ni dhahiri sasa kuwa waasisi wa muundo wa Muungano wa kikatiba ambao wengine tumewasikia wakitamka katika mikutano ya hadhara katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu, kuwa muundo wa Muungano utabaki kama ulivyo watu watake wasitake hautabadilika, na kula viapo kuulinda kwa gharama zozote kama ulivyo, kila mmoja alikuwa na sababu nyingine za ziada zilizomfanya aukubali Muungano kwa wakati ule.
Baba na muasisi wa Taifa la Zanzibar, marehemu Mzee Abeid Amani Karume kama angekuwa hai hivi leo sidhani kama angeweza kupingana na mawazo ya wanaotaka mabadiliko ya muundo wa Muungano, bali angeunga mkono fikra za kuwa na Muungano wa mkataba kwani siku za mwanzoni mwa kuundwa kwa Muungano alisikika akisema wananchi (Wazanzibari) wasiwe na shaka, Muungano ni kama koti, likikubana unalivua.
MWISHO.
MWISHO.
Chanzo: Mwananchi
No comments :
Post a Comment