Waziri Magufuli
18 Dec 2012.
Na Rehema Mohamed
WAZIRI wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, ameiagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kubomoa nyumba zote zilizopo kandokando mwa Barabara ya Mwenge hadi Moroco ambazo zimewekwa alama ya X, ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Dkt. Magufuri alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana wakati akizindua Bodi Mpya ya TANROADS, ambayo Mwenyekiti wake ni Bi. Hawa Mmanga pamoja na bodi ya Wakala wa Mfuko wa Barabara ambayo inaongozwa na Mwenyekiti Bw. James Wanyacha.
Alisema tayari fedha za kuwalipa fidia wamiliki wa nyumba hizo zipo lakini anashangaa kwanini TANROADS inasita kutekeleza mpango wa ubomoaji nyumba hizo.
Aliongeza kuwa, kazi ya ubomoaji inapaswa kufanyika haraka ili ujenzi wa barabara ya njia nne uanze mara moja.
“Barabara ya Mwenge hadi Moroco inasubiri ubomoaji wa nyumba, fedha za mkandarasi wa kujenga barabara hii zipo, nashangaa kuona nyumba zimewekwa alama bila kubomolewa, nataka ubomoaji huu ufanyike mapema,” alisema Dkt. Magufuli.
Alisema katika bajeti fedha ya mwaka 2012/13, wametenga pesa za kulipia fidia na wale wanostahili kulipa utaratibu ufanyike haraka kwani Watanzania hawana muda wa kusubiri bali wanataka kuona matokeo.
Katika hatua nyingie, Dkt. Magufuli ameutaka Mfuko wa Barabara nchini, kutozipa fedha halmashauri ambazo hazijaajiri Wahandisi.
Alisema hatua hiyo itasaidia matumizi ya fedha za mfuko kutumika kama inavyokusudiwa pamoja na miradi ya barabara kutekelezwa kwa kiwango kinachostahili.
Aliongeza kuwa, mwaka huu Bodi ya Barabara itakusanya sh. bilioni 430 ambazo zitatumika katika ujenzi na uboreshaji barabara zilizopo katika halmashauri zote nchini.
“Nataka bodi zote zitekeleze majukumu yao kwa ufanisi mkubwa, Bodi ya TANROADS ihakikishe inawafukuza kazi Mameneja wote wa Wilaya ambazo halmashauri zao zitavurunda katika utekelezaji wa miradi ya barabara,” alisema Dkt. Magufuli.
Akizungumzia agizo lake la ubadilishaji namba za magari ya Serikali, Dkt. Magufuli alisema hadi sasa magari 746 ndiyo hayajasajiri namba mpya na yaliyosajiri ni 974.
Alisema Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, inaongoza kwa kuwa na magari ambayo hayajasajiriwa ikifuatiwa na TAMISEMI.
Wajumbe walioteuliwa katika Bodi ya TANROADS ni Bw. Joseph Haule, Bw. Joseph Nyamanga, Bi. Edina Kayanda, Bw. Elijius Mwakanja, Bi. Balkel Sahel, Bw. Aron Kisaka na Bw. Richard Rugimbana.
Kwa upande wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Bw. Helbert Mgango, Dkt. Ramadhani Kijja, Bw. Jumanne Sagimi, Bw. Joseph Nyamhanga, Bw. Wilges Mbogoro, Bw. Feldisn Mbube na Bw. Peter Chowilo.
Chanzo: Majira
|
No comments :
Post a Comment