.Aondolewa viti mkutanoni
.Akusanya maoni amesimama
.Akusanya maoni amesimama
Wahusika katika kadhia hiyo waliondoa pia viti na jukwaa dogo, vilivyowekwa jioni ya kuamkia jana ambapo ukusanyaji maoni huo ulifanyika.
Dk Salim na makamishna kadhaa wa tume hiyo inayongozwa na Jaji Joseph Warioba, walijikuta wakipokea maoni wakiwa wamesimama katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Kisonge uliopo Unguja.
Dk Salim ambaye aliwasili uwanjani hapo saa 1 asubuhi akiwa na makamishna wenzake, walilazimika kujitambulisha na kuanza kuchukua maoni kwa wananchi wakiwa wamesimama.
Watu kadhaa waliokuwa uwanjani hapo, waliiambia NIPASHE Jumapili kuwa, kabla ya ujio wa Dk Salim na makamishna hao, viti na meza vilionekana uwanjani hapo, vikisiwekwa na masheha kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Inasadikiwa kuwa watu wasiofahamika, walifika eneo la jukwaa alfajiri jana, wakabeba viti, meza na jukwaa, kisha kutoweka kusikojulikana.
Makamishna wengine waliokuwepo katika zoezi hilo, Fatma Said Allly, Al-Shymaa Kway-Geer na Ally Salehe ambaye ni mlemavu wa mguu, kupata wakati mgumu kwa kusimama muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo, walianza ukusanyaji maoni wakiwa wamesimama hadi ilipofika saa 3:30 asubuhi, vilipoletwa viti, jukwaa dogo na meza.
Vifaa hivyo vililetwa kwa kutumia magari aina ya Toyota Dyana yenye namba Z 879 AM na Toyota Hiace yenye namba Z 348 BR.
“Waheshimiwa makamishna, naomba msitishe kidogo zoezi ili mpate nafasi ya kuhamia katika jukwaa,”alisema Afisa aliyekuwa akiongoza mjadala huo ambaye hata hivyo jina lake halikupatikana mara moja.
Dk Salim na makamishna wenzake, walisitisha na baada ya muda walikwenda kuketi.
Mkuu wa wilaya ya Mjini, Kanali mstaafu Abdi Mahmoud, alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema njia mbadala zilitumika kupata viti vya kukodi.
Kanali mstaafu Mahmod, alisema alipokea taarifa za kuchukuliwa kwa jukwaa hilo akiwa kwenye kikao cha ulinzi na usalama ofisini kwake.
Hata hivyo, alipendekeza kwa tume hiyo kutumia utaratibu wa kukodi vifaa kama viti, meza na jukwaa, ili kuondokana na kasoro iliyojitokeza.
Naye Katibu wa Siasa na Uenzi wa CCM katika wilaya ya Mjini, Baraka Mohamed Shamte, alisema viongozi wa shehia ya Malandege na RahaLeo wanastahili kulaumiwa kutokana na tukio hilo.
Shamte alisema baada ya vifaa hivyo kuwekwa, ilitakiwa uwepo ulinzi na uangalizi wa vifaa hivyo na si kufungwa na kuachwa bila ya usimamizi.
WANANCHI WATAKA CHAGUZI NDOGO ZIFUTWE
Wakitoa maoni yao, baadhi ya wananchi walipendekeza kufutwa kwa chaguzi ndogo pindi wawakilishi kwa nafasi za ubunge, uwakilishi, udiwani, mwenyekiti wa kijiji, mtaa ama kitongoji wanapokufa.
Walisema badala yake, chama kilichomsimamisha mwakilishi, kihusike kumteua mtu wa kuziba nafasi hiyo.
Mashamu Kinani Abeid (61), alisema serikali inatumia gharama kubwa kuitisha uchaguzi mdogo, hivyo pendekezo hilo lifitekelezwa itachangia kupunguza upotevu wa fedha za umma.
Kapteni mstaafu Zaharani Mohamed (65), alipendekeza kuwepo ukomo wa awamu mbili kufikia miaka 10 kwa mshindi wa ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Alisema haifai kwa Rais wa nchi kuwa na ukomo wa kuongoza wakati Mbunge, Mwakilishi na viongozo wengine wa kuchaguliwa na wananchi wakihudumu kwa zaidi ya miaka 25 hadi 30.
WAGUSIA KERO ZA MUUNGANO
Kuhusu kero za Muungano, alisema muarubaini wa kumaliza matatizo hayo ni kushirikishwa kwa marais wa Muungano na Zanzibar katika vikao ili kupata suluhu kwa muda mfupi kuliko ilivyo sasa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment