NA MWINYI SADALLAH
1st December 2012
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali yake imeamua kurejesha mitaala ya masomo ya uvuvi na kilimo, katika shule za msingi na sekondari ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri na kufikia lengo la kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurejea kutoka nchini Vietnam alikokuwa katika ziara ya wiki moja ya kiserikali, Dk. Shein alisema sekta ya uvuvi ina nafasi kubwa ya kutengeneza ajira kwa vijana wa Zanzibar.
Alisema mpango huo utakwenda sambamba na mpango kazi wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na tayari Serikali imefungua mlango wa uwekezaji katika sekta ya viwanda vya kusindika samaki na matunda.Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurejea kutoka nchini Vietnam alikokuwa katika ziara ya wiki moja ya kiserikali, Dk. Shein alisema sekta ya uvuvi ina nafasi kubwa ya kutengeneza ajira kwa vijana wa Zanzibar.
"Tayari Serikali imeshaamua kuanzisha mitaala ya uvuvi na kilimo kwa wanafunzi, kama mpango wa kuongeza ajira na kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa Zanzibar," alisema Dk. Shein.
Alisema kwamba Serikali imeamua kuanzisha vitengo vya utafiti katika kila wizara, kwa vile hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo bila ya kulipa kipaumbele suala la utafiti na tayari serikali imeanza kusomesha vijana ili kukijengea uwezo kituo cha taasisi ya utafiti iliyopo Kizimbani Zanzibar.
Alisema Serikali pia ina mpango wa kuanzisha benki ya wakulima na wavuvi, ambayo itasaidia wavuvi na wakulima katika mpango wake wa kuleta mapinduzi ya kilimo, na kutumia mali asili za bahari katika kuharakisha mapambano dhidi ya umaskini.
Alisema Vietnam imeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kufanikiwa kuwekeza katika sekta ya elimu na kilimo, ambapo ni nchi ya pili inayoongoza kwa uzalishaji wa mchele duniani.
Hata hivyo, alisema ili Zanzibar iweze kufanikiwa kimaendeleo lazima watu waache kufanyakazi kwa mazoea na badala yake wafanyekazi kwa kujituma ili kufikia malengo ya kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
alisema lengo la Serikali ni kuona Zanzibar inazalisha asilimia 50 ya chakula hadi ifikapo mwaka 2015 kwa kuimarisha kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ndiyo maana imeamua kupunguza bei za pembejeo za kilimo kwa asilimia 75.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment