Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake ya ufunguzi
rasmi wa Mkutano wa pili wa Wanazuoni wa Bara la Afrika,
ulioanza leo katika Ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wageni kutoka nchi mbalimbali za Bara la Afrika,
waliohudhuria mkutano huo leo, wakimsikiliza Makamu
wa Rais, Dkt. Bilal.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja
na baadhi ya washiriki wa mkutano huo, baada ya ufunguzi.
Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amehimiza umuhimu wa kujenga maelewano mazuri baina ya wafuasi wa dini mbalimbali, vinginevyo, Bara la Afrika linaweza kushuhudia migogoro ya kidini kama ilivyoanza kujitokeza huko Nigeria na hata hapa nchini.
Dk. Bilal ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa wanawazuoni wa Bara la Afrika uliofanyika katika ukumbi wa Karume, PTA viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es salaam.
Alielezea matumaini yake kuwa mkutano huo utayatafakari matukio mbalimbali ya vurugu za kidini ambazo zimetokea hapa nchini hivi karibuni kwa lengo la kuweka mustakabali mzuri wa kuishi kwa kuheshimiana baina ya wafuasi wa dini kuu mbili za Kiislamu na Kikristo.
"Imani si ugomvi bali imani inapaswa itujenge kimaadili na moja katika tunu za maadili ni kuishi vizuri na watu wengine hata kama si wa imani yako," alibainisha
Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa elimu ya mwongozo na ile ya maarifa ya dunia kwa Waislamu na kusema itawawezesha kutatua matatizo yanayowakabili wananchi yakiwemo ya uharibifu wa maadili, uasherati, maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukosefu wa ajira na unyanyasaji wa kijinsia.
Alitoa changamoto kwa wanawazuoni wa Kiislamu na viongozi wengine wa dini kuangalia ni jinsi gani utandawazi hautoathiri imani na maadili ya waumini lakini pia ni jinsi gani waumini watanufaika na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyofikiwa na mwanadamu hivi sasa.
Malengo ya umoja huo wa wanawazuoni Barani Afrika ni pamoja na kutilia nguvu masuala ya elimu, ushirikiano na kuheshimiana baina ya jamii mbalimbali Barani Afrika.
Makamu wa Rais aliyaelezea malengo hayo ni mazuri na ya kujenga ambayo kama yakiwekwa katika matendo, itaondoa ile picha hasi kuwa waislamu ni watu wenye kufarakana, wasio na elimu, wasioheshimu dini za wengine na wasiotambua nafasi na mchango wao katika maendeleo ya nchi hizo.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es salaam
Jumamosi – Disemba 15, 2012.
Chanzo: Mjengwa Blog
No comments :
Post a Comment