NA DANIEL LIMBE
16th December 2012
.Walimfyatulia risasi, wakashambuliwa kwa silaha za jadi
Tukio hilo lilitokea baada ya askari polisi kudaiwa kumuua mwananchi mmoja waliyemtuhumu kwa wizi.
Askari hao wanadaiwa kumfyatulia risasi mbili mwananchi huyo na kufa papo hapo.
Baada ya tukio hilo, wananchi wenye hasira walivamia kituo kidogo cha polisi cha Mgoma wilayani humo, na kuwaua askari waliokuwepo.
Taarifa zinadai kuwa wananchi hao walitumia silaha za jadi na mawe kufanikisha mauaji hayo.
Mwananchi aliyeuawa alitambulika kwa jina la Said Mkonikoni, anayetajwa kama fundi pikipiki aliyekuwa akifanya shughuli zake wilayani humo.
Wakizungumza na NIPASHE Jumapili, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo ambao hata hivyo hawakutaka majina yao kuandikwa gazetini, walisema lilitokea jana saa 8:15 mchana.
Walidai kuwa ilikuwa baada ya askari hao kumkamata mwananchi huyo, kumshambulia kwa virungu na mateke, kisha kumfyatulia risasi kwenye kifua na miguuni.
Ilidaiwa kuwa askari polisi walimfyatulia risasi baada ya mtuhumiwa huyo kukaidi kupigwa na kupelekwa kituo cha polisi.
Kufuatia hali hiyo, wananchi waliokuwepo eneo hilo walionekana kukasirishwa na kitendo hicho, hivyo kuhamasishana na kuwafuata askari hao kituoni.
“Niliwaona askari polisi wakikimbia baada ya kuona umati wa wananchi ukiwafuata, nadhani walikuwa wananusuru maisha yao,” alieleza shuhuda mmoja.
Mbali na jitihada hizo, askari hao walishindwa kukwepa mikono ya wananchi ambapo mmoja alidondoka jirani kabisa na kituo hicho.
Wananchi waliokuwepo walimshambulia kwa mawe na marungu hadi alipokufa.
Kutokana na wingi wa wananchi hao, wengine walilazimika kumkimbiza askari mwingine na kumkamata, kisha kumshambulia kwa kipigo hadi mauti yalipomfika.
Hasira za wananchi hao hazikuishia hapo, kwani baadaye walikwenda kuteketeza kwa moto kituo cha polisi.
Askari waliokufa wametajwa kuwa ni Koplo Paschal na Sajenti Alex, waliokuwa wanafanya kazi kituoni hapo.
Baada ya kituo hicho kuchomwa moto, baadhi ya mali za serikali, zikiwemo pikipiki tatu na silaha moja viliteketea na kusababisha hasara ambayo hata hivyo thamani yake haijafahamika.
Habari za kuaminika zimeeleza kuwa kituo hicho kidogo cha Mgoma kina askari polisi wanne, na kwamba hakuna hata gari linaloweza kutoa msaada kwa askari hao kunapotokea dharura ya aina yoyote.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Alex Kalangi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo alisema yupo safarini kuelekea eneo la tukio na kwamba atazungumza zaidi baada ya kufika eneo la tukio.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment