Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, December 20, 2012

Serikali yaifunga hoteli ya Double Tree


Hoteli  ya Kitalii iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, yenye hadhi ya nyota tano imeumbuka baada ya kubainika kumwaga maji ya chooni baharini. 


NA MWANDISHI WETU

20th December 2012


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa ( wa pili kushoto), akitoa maelekezo kwa wamiliki wa hoteli ya Double Tree baada ya kuifunga rasmi hoteli hiyo ya jijini Dar es Salaam jana.
Serikali imeifungia hoteli ya kitalii ya Double Tree by Hilton ya jijini Dar es Salaam kutokana na kukaidi agizo la kuacha kutiririsha majitaka baharini.

Hatua hiyo ilichukuliwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa.

Hoteli hiyo ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano iko Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Huvisa alitoa agizo la kuifunga hoteli hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga.

Ziara hiyo ililenga kuona utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa awali na Kitwanga Desemba 6, mwaka huu, alipofanya ziara kutembelea viwanda na hoteli zilizoko pembezoni mwa bahari ya Hindi kuona mfumo wa majitaka.

Katika ziara hiyo, Kitwanga aliiagiza hoteli hiyo kuwa na mpango wa muda mfupi na wa haraka wa kusitisha utiririshaji wa maji taka baharini, lakini hadi kufikia jana agizo hilo halikutekelezwa.
Sambamba na kuifunga, Waziri Huvisa pia alifuta hati ya ukaguzi wa Mazingira (Environemental Audit) na kuitaka hoteli hiyo kurekebisha mara moja mfumo huo ikiwa na kulipa faini kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira  (Nemc).

Waziri Huvisa alisema hoteli hiyo itafunguliwa baada ya kutekeleza maagizo ya serikali.

Wakati wa ziara ya Naibu Waziri Kitwanga katika hoteli hiyo, ilibainika kwamba mfumo wa majitaka haujajengwa vizuri kuruhusu maji hayo kusafishwa kabla hayajamwagwa au kuingizwa kwenye mfumo wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco).

Kitwanga na maofisa wa Nemc walifika kwenye hoteli na kuhoji mfumo wa majitaka pamoja na sababu za kujengwa hadi baharini.

Mameneja wa hoteli hiyo walimweleza Naibu Waziri kwamba maji hayo yanahifadhiwa vyema kisha kuzolewa kwa magari ambayo huenda kuyamwaga kwenye mabwawa ya majitaka.

Hata hivyo, Kitwanga alihoji linapopita gari la kwenda kuchukua maji hayo kwa kuwa eneo zima limezungukwa na majengo pamoja na ukuta usioruhusu gari kupita.

Baada ya kuendelea kukagua, ndipo ilibainika kwamba uchafu wote wa hoteli hiyo na hasa maji ya chooni yanamwagwa baharini.

“Tulichoona hapa ni kinyesi kabisa, harufu ya maji ya chooni inatoka halafu hawa wanatudanganya eti ni mtiririko wa maji wa kawaida, hali hii haikubaliki," alisema Kitwanga alipofanya ziara hiyo.

Kitwanga alisema serikali inawahamasisha wawekezaji waje kuwekeza nchini, lakini kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, vinginevyo itawachukulia hatua stahiki.

Alimweleza Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Sven Lippinghof,  kumwaga kinyesi baharini ni suala lisilovumilika na kumtaka kuzingatia sheria ya mazingira na nyinginezo ili kulinda afya ya viumbe wa baharini na za wananchi.

Naibu Waziri huyo aliitaka Nemc kufuatilia kwa kina usitishwaji wa kumwaga maji hayo na kumpa mwekezaji huyo wiki moja kwamba hadi Desemba 14, mwaka huu awe amefanya marekebisho ya kina.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Nemc, Manchere Heche, aliitaka hoteli hiyo kusitisha kumwaga maji hayo baharini kuanzia siku hiyo na kumwandikia barua ya kusisitiza amri hiyo.

Alisema kuanzia Desemba 6, mwaka huu Nemc ingefanya ukaguzi katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba agizo hilo linatekelezwa.

Alisema: “Afya za watu haziwezi kusubiri muda, na tutawatoza faini kwa uchafuzi huu wa mazingira.”

Kwa upande wake, Lippinghof alisema atatekeleza maagizo hayo ya Nemc na kwamba suala la kuzingatia sheria halina mjadala.

Alisema atawasilisha pia maagizo hayo kwenye kikao cha bodi ya wakurugenzi wa hoteli hiyo kwa hatua zaidi.


CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment