NA MUHIBU SAID
3rd December 2012
Jitihada za Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kutafuta mwafaka katika mgogoro unaohusisha viwanja vitatu katika eneo la Chasimba, jijini Dar es Salaam, kati ya wakazi wake na kiwanda cha saruji cha Wazo (Twiga Cement), zimekumbana na wakati mgumu, baada ya kutaka hatimiliki ya eneo hilo inayomilikiwa na kiwanda hicho ifutwe.
Wakazi hao wapatao 903 wakiongozwa na madiwani, ambao eneo hilo lenye mgogoro limo ndani ya kata wanazoziwakilisha, walitoa madai hayo kupitia maombi waliyoyatoa kwa Waziri Tibaijuka jana, wakitaka ayafikishe kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya utekelezaji.
Hata hivyo, pamoja na kutoa maombi hayo, katika kesi namba 129 ya mwaka 2008, wakazi hao wameamriwa na Mahakama ya Rufaa kuondoka katika viwanja hivyo, baada ya kujiridhisha kuwa walivamia na kujenga ndani yake, kinyume cha sheria.Wakazi hao wapatao 903 wakiongozwa na madiwani, ambao eneo hilo lenye mgogoro limo ndani ya kata wanazoziwakilisha, walitoa madai hayo kupitia maombi waliyoyatoa kwa Waziri Tibaijuka jana, wakitaka ayafikishe kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya utekelezaji.
Viwanja hivyo vyenye mgogoro, ni namba 1, 4 na 7 Wazo Hill vilivyoko katika eneo la Chasimba, ambalo linamilikiwa na kiwanda hicho.
Mkutano kati ya Waziri Tibaijuka na wakazi hao, ulifanyika jijini Dar es Salaam jana kwa lengo la kutafuta mwafaka juu ya utekelezaji wa hukumu ya mahakama hiyo na serikali kuwalipa fidia ya viwanja hivyo kama ilivyoahidi, kwa amani na utulivu.
Mkutano huo ulioongozwa na Waziri Tibaijuka, ulihudhuriwa pia na watendaji wa wizara hiyo, madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa, baadhi ya wakazi wa eneo hilo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana.
Diwani wa Kata ya Wazo, John Moro, alisema katika jumla ya mambo, ambayo walizungumza na Waziri Tibaijuka, ni pamoja na kumuomba awafikishie maombi yao ya kutaka hatimiliki ya kiwanda hicho, ifutwe ili waendelee kulitumia eneo hilo bila bughudha.
Alisema iwapo ombi la kufutwa kwa hati hiyo halitawezekana, basi uthamini wa mali za wananchi katika eneo hilo ufanyike ili walipwe fidia kwa haki kulingana na thamani ya sasa.
“Wananchi wanaona kama wanaonewa, wanadhulumiwa. Hivyo, watakaopima wapime kwa uadilifu na kwa haki,” alisema Moro.
Pia, aliitaka serikali kushughulikia tatizo la watu kutoendeleza maeneo wanayopata.
Alilaumu utekelezaji wa hukumu hiyo ya mahakama kuchelewa akisema hali hiyo inawafanya wananchi waliojenga katika eneo hilo, ambao ni wa kipato cha chini kuteseka, hivyo akataka haki itendeke.
Akijibu ombi kuhusu hatimiliki hiyo, Waziri Tibaijuka alisema uwezekano wa kufuta hatimiliki ya kiwanda hicho kinachomilikiwa na Kampuni ya Tanzania Portland Cement Limited (TPCC) ni mdogo kwa kuwa mgogoro kuhusu eneo hilo ulikwishaamuliwa na mahakama, hivyo Rais hawezi kufuta amri ya mahakama.
Diwani wa Kata ya Bunju, Majisafi Sharifu, aliwataka wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu katika kipindi hiki, ambacho serikali kupitia Waziri Tibaijuka, inashughulikia mgogoro huo.
Awali, Waziri huyo alisema serikali inataka mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu uishe na kwamba, mkutano wa jana kati yake na wakazi hao ulikuwa ni kielelezo cha jinsi ya kumaliza migogoro ya ardhi kwa mazungumzo ya amani na wadau badala ya kutumia nguvu.
Alisema katika kufikia lengo hilo, serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuwatafutia wakazi hao eneo mbadala.
Waziri Tibaijuka alisema baada ya mahakama kuamua wakazi hao waondoke katika eneo hilo kwa kuwa ni mali halali ya kiwanda hicho, serikali iliwatafutia eneo mbadala na kuwapimia viwanja katika eneo la Kibaha, mkoani Pwani.
Hata hivyo, alisema zoezi hilo lilikwama baada ya wakazi hao kutokubaliana na eneo hilo kwa madai kwamba, liko mbali na mji.
Alisema kutokana na pingamizi hilo, serikali iliamua kutwaa eneo la Mabwepande kwa ajili ya kuwahamishia.
Hata hivyo, alisema mkakati huo ulikwama baada ya serikali kulazimika kutumia viwanja vya Mabwepande kama dharura ya kuwahamisha waathirika wa mafuriko ya Bonde la Msimbazi na Jangwani mwishoni mwa Desemba, mwaka jana.
Kutokana na hali hiyo, alisema jana serikali kupitia wizara yake iliamua kukaa na wakazi hao pamoja na madiwani wao ili kufanya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa mgogoro huo.
“Wizara tunataka mgogoro uishe. Tunatafuta mawazo. Migogoro inakwamisha maendeleo,” alisema Waziri Tibaijuka.
Alisema katika mkutano huo wamekubaliana na wananchi hao kwenda katika eneo lenye mgogoro na kulipima ili eneo la kiwanda hicho lijulikane.
Waziri Tibaijuka alisema kazi hiyo inatarajiwa kufanyika ndani ya siku saba.
Alisema hatua itakayofuatia ni eneo hilo kufanyiwa uthamini na kwamba, kazi hiyo inatarajiwa kufanyika ndani ya siku 14 kabla ya ulipaji wa fidia kufanyika.
Hata hivyo, alisema hukumu ya mahakama hiyo iliyomaliza mgogoro huo Agosti 25, mwaka 2010, itaendelea kusimama kama ilivyo, na kwamba, watahakikisha inatekelezwa vizuri.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment