Huyo hapo juu sio ombaomba wa mitaani bali ni mzee wetu na mkulima hodari Mzee Mwanakijiji
akirejea kutoka kondeni na huku akiwa kachoka taabani - kama alivyopigwa picha
jana jioni huko Bagamoyo kwenye kijiji chake.
Dear Ndugu M.M. Mwanakijiji,
"Mtu
ambae ni mgonjwa wa akili akakushauri kitu na wewe ukamkubalia, basi utakuwa na
wewe ni mgonjwa wa akili kama yeye".
Mwenye upungufu wa akili siku zote hajijui na huwaona wengine
ndio wasiokuwa na akili na kuwa yeye ni
timamu. Hapa hatukuzungumzi wewe Mwanakijiji, kwasababu wewe ni mtu mwenye
akili timamu – kwa maneno mengine huwa tunasema 'zako zimetimia'. Ngojea kidogo
tutoe mfano mmoja ili ufahamu
tunakusudia nini, au nini maana ya kuwa na akili nyingi juu ya masuala ya
Unguja.
Madaktari wa wagonjwa wa akili wa Mental Hospital moja
walitaka kujua nani kati ya wagonjwa wao amepona na nani bado, ili aliepona
aruhusiwe kuenda nyumbani. Wakawatoa wagonjwa wote kwenye backyard ya hospitali
yao iliyozungushwa ukuta wa futi 12 ili wasitoroke.
Daktari mmoja alichora picha ya mlango kwenye ukuta mmoja
ndani ya ile backyard na baadae wagonjwa wakaambiwa kuwa mlango ni ule pale na
atakae atoke ili aende zake nyumbani.
Wagonjwa walipiga vigelegele na mayoeyoe, kwani walifurahi
sana na wakawa wanasukumana kutaka kufungua mlango, kwasababu kila mmoja
alitaka atoke yeye mwanzo. Msukumano ukaendelea kwa zaidi ya robo saa, lakini
hakuna alieweza kutoka nje, kwani ule haukuwa mlango – ilikuwa ni picha tu ya
mlango kwenye ukuta!
Wakati wagonjwa wanasukumana ili wafungue mlango,
mmoja kati ya wale wagonjwa alikaa pembeni
peke yake na akawa anacheka kwa nguvu sana na huku akawa anarukaruka kama vile
ameshinda bahati nasibu.
Madaktari walivyomuona yule mmoja anacheka na yupo
peke yake walifurahi sana, kwani walidhania kuwa yeye atakuwa keshapona na alikuwa
anacheka kwasababu alishajua kuwa ule sio mlango. Kwahivyo, madakatari wakataka
yule mmoja wamruhusu aende zake nyumbani. Lakini, kabla ya kumruhusu wakasema
hebu bora waende kuzungumza nae na kumuuliza masuala 2-3 kabla hawajamtoa.
Walipofika karibu yake wakamuuliza yeye anacheka nini? Jibu lake likawa ni
kicheko zaidi tena cha nguvu kubwa sana kuliko cha pale mwanzo. Alipomaliza
kucheka na kurukaruka akawauliza wale madakatari kuwa hivyo wao hawaoni wale wenzake
ambao wanagombania kutoka kwenye ule mlango ambao yeye aliufunga kabla kwa
kufuli? Alipoulizwa na madaktari upo wapi huo ufunguo wa kufuli, yeye alijibu
kuwa aliuacha chumbani kwake kwa makusudi, kwani alikuwa hataki hata mtu mmoja
atoke pale mlangoni!
Baada ya madaktari kusikia hivyo wao wenyewe
wakaanza kutizamana, kwani waliemdhania kapona kumbe ni mgonjwa zaidi ya wale
wengine na kwahivyo wagonjwa wote wakarejeshwa ndani kuendelea na tiba.
Nd.
Mwanakijiji, unapiga picha ya mlango ukutani na
baadae unatueleza Wazanzibari tufungue huo mlango ili tupate kutoka nje ya Muungano - mlango ambao ni picha tu
ukutani na sio mlango wa kweli. Mwanakijiji, unadhania sisi Wazanzibari ni sawa
na wale wagonjwa wa akili na kuwa utatudanganya na tutakurupuka ovyo? KAMA UNATAKA KWELI TUTOKE BASI WEKA
MLANGO WA KWELI NA SIO PICHA YA MLANGO!
Nd. Mwanakijiji unaandika na tunakunukuu kuwa….."Wazanzibari
walete mswada kwenye Bunge lao (Baraza la Wawakilishi) wa kusimamia kura ya
maoni na waulizwe tu swali moja jepesi "JE UNATAKA ZANZIBAR IJITOE KWENYE
MUUNGANO NA TANGANYIKA IFIKAPO JANUARI 1, 2014?"
Unaendelea Nd. Mwanakijiji kuwa…..”Ni kwasababu hiyo baadhi yetu tunataka Wazanzibari kama kweli wanataka
watoke kwenye Muungano waanze mchakato wa kuandika sheria ya kura ya maoni
mapema ili kura ya maoni iitishwe Julai mwakani na Zanzibar iwe taifa huru
ifikapo January 1, 2014.”
Inshaallah Zanzibar
itakuwa Taifa huru ifikapo January 1, 2014 au hata kabala ya hapo, lakini sio
kwa kupitia huo mlango unaouchora wewe ukutani. Nd. Mwanakijiji, hivyo kweli
kuishi kote hapa Bongo bado hujazijua siasa zetu za kikoloni za Mwafrika mmoja kumuonea
mwengine? Ikiwa Rais wa Zanzibar anachaguliwa
Dodoma, ikiwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yanaamuliwa Dodoma, hivyo
unadhania mswada gani utakaopita kwenye BLW letu bila ya kukubaliwa Dodoma? Wewe mwenzetu ni mwenye akili timamu au upo kwenye utani tu?
Kama kweli unataka Wazanzibari waamue
kuhusu Muungano, basi weka kwanza mazingira yatakayoruhusu hali hio. Waachie
Wazanzibari wawe huru kwanza, yaani waweze kujichagulia wenyewe Rais wao
wanaemtaka na chaguzi zao ziachie ziwe FREE
and FAIR, halafu tena ndio uwaulize
wanataka nini.
Wape Wazanzibari ‘a level playing field’ na baadae uone kama hawajakufunga 6-5!
Ni danganya toto kuwataka Wazanzibari waseme
wanataka nini wakati Serikali ya Zanzibar ipo chini yako. Hivi sasa ukitakacho
wewe ndio tunachokitaka sisi, kwasababu tupo chini yako na hatuna sauti yoyote
ile. Tukitoa sauti unatuziba midomo!
Mswada!!!!! You are really
joking again! Kama huamini hebu kesho muachie Dr Shein atamke hadharani kwa
utani tu (na sio kwa kuandaa mswada), kuwa katika mwaka 2013 Wazanzibari watakuwa
na kura ya maoni juu ya Muungano wautakao na uone itatokea nini. I swear to
God, within a second only Dr Shein
ataitwa Kizota na atatakiwa ajieleze na hapo hapo ataondolewa madarakani kama
alivyo ondolewa Shk Aboud Jumbe Mwinyi. Hivyo Nd. Mwanakijiji hujui kwanini
Jumbe alipinduliwa au wewe upo kwenye mzaha na utani tu kuhusu mambo ya Unguja?
Nd. Mwanakijiji, you need to take the union
issues very seriously na sio kiutani utani. PLEASE, STOP BEING A POLITICAL PLAY-BOY OVER THE ZANZIBAR ISSUES!
Wenzenu Visiwani tunaumia kwa huu mchezo wenu. Imekuwa sawa na ile hadithi ya
vyura na watoto – nyinyi mpo kwenye mchezo na mnarusha mawe dimbwini, lakini
wenzenu tunakufa!
Ikiwa watu wametamka tu Muungano hawautaki na wapo ndani mpaka leo,
je, Wawakilishi wetu wakiandaa mswada huo unaoutaja wewe sio watanyongwa
kabisa? Au wewe hujui kuwa hivi sasa unapotania wapo Wazanzibari waliowekwa jela
hapa Unguja!
Nd. Mwanakijiji, fahamu kuwa Wazanzibari
sio sawa na wale wagonjwa wa akili waliochorewa mlango ukutani na wakakimbilia
kutaka kutoka nje. Walichopata wale wagonjwa ni kugonga vichwa vyao pale kwenye
ukuta na nje hawakuweza kutoka. Nasi tukifuata ushauri wako tutamalizikia hivyo
hivyo - yaani tutagonga vichwa vyetu ukutani tu na kwenye Muungano hutotutoa.
Kwahivyo, usitaabike kuchora mlango ukutani. Sisi wenyewe tutatoboa huo ukuta
wako na tutatoka bila ya msaada wako - only time will tell when!
KUHUSU SUDAN YA KUSINI, PUERTO RICO NA SCOTLAND:
Mwanakijiji unachekesha kweli. Hivyo
unafananisha uhusiano uliopo baina ya Sudan na Sudan ya Kusini ni sawa na
uhusiano wa Zanzibar na Bara? Hujui kama Zanzibar ipo chini ya Bara na kuwa
Zanzibar haiwezi kufanya chochote bila ya Bara kukubali? Je, Sudan ya Kusini
inaipigia magoti Sudan? Je, Sudan ya Kusini haiwezi kufanya lolote mpaka Sudan
wakubali? Zanzibar ingelikuwa kama Sudan ya Kusini basi masuala ya Muungano leo
yasingelikuwepo hata kidogo, kwasababu zamani huo Muungano wenyewe ungelikuwa
marehemu.
Vipi kuhusu Puerto Rico na Marekani?
Hivyo Marekani inaingilia siasa za Puerto Rico kama Bara inavyoingilia hali ya
siasa ya Zanzibar? Hivyo Zanzibar wanao uhuru wa kuamua jambo lolote peke yao
kama Puerto Rico bila ya kuingiliwa? Hivyo mambo ya Puerto Rico yanaamuliwa Washington kama yetu sisi
yanavyoamuliwa Kizota?
Pia, umetoa mfano wa UK na Scotland. Zanzibar
ingelikuwa huru kama Scotland ilivyo unadhani ingelikuwepo haja ya kutengeneza
huo mswada? Zanzibar ingelikuwa ishatoka zamani!
Nd. Mwanakijiji, hizo nchi ulizozitaja hazilingani hata kidogo
na hali halisi ilivyo hapa kwetu baina ya Visiwani na Bara. Zanzibar huwezi
kuifananisha hata na nchi moja katika hizo ulizozitaja. Hizo nchi zipo huru,
wakati sisi mmetubana na wala hatuwezi kuamua chochote bila ya nyinyi kutaka. After
all, Rais wa Zanzibar ni Rais wenu,
mnamchagua nyinyi, sasa unategemea nini? Au hujui 2010 Wazanzibari walimtaka
nani awe Rais wa Zanzibar na nyinyi
mlituchagulia nani???Au wewe hukuwepo Kizota wakati ule? Ikiwa Rais wetu
mnatuchagulia nyinyi, hivyo tutaweza kutoa mswada unaokuenda kinyume na matakwa
yenu nyinyi na ukapita kwenye BLW???
Tulipiga kelele kidogo tena kwa midomo
tu na sio kwa kuandika mswada kwenye BLW, kuhusu gesi na mafuta na tulichopata
ni kuwa mpiganaji wetu alifukuzwa uwaziri kwa amri iliyotoka Kizota. Lakini,
kama unakumbuka mwisho suluhisho juu ya suala la gesi na mafuta lilitoka mji
gani? Kizota na sio Zanzibar!
Mtwara na wao sasa washaanza
kusikitika kama tunavyosikitika sisi juu ya Muungano, kuwa gesi yao inaletwa
DSM na wao wanaambulia kupitishiwa pipes tu kwenye mashamba yao. Sasa na wao
sijui utawaeleza watengeneze mswada au vipi? Maanake, inaonesha kuwa mswada ndio your magic word ya kumaliza matatizo yote yale ya wananchi!
Ukweli kama unautaka au huutaki ni
kuwa Tanzania Bara ndio inayoamua juu ya chochote kuhusu Zanzibar na hilo huwezi kulipinga. Tungelikuwa
huru kama walivyo Scotland, Puerto Rico au Sudan ya Kusini kwenye huu Muungano
basi tungelikuwa tushatoka zamani sana.
Kama nyinyi mngelikuwa ABSOLUTELY
NEUTRAL kama unavyojidai basi issue ya Zanzibar ingelikuwa imekwisha zamani!
KUGAWANA ASSETS BAADA YA MUUNGANO KUVUNJIKA
Eti unazungumzia juu ya kugawana mali baada ya
Muungano kuvunjika iwe kisheria ili hii process iwe nzuri isijekuleta matatizo
yoyote yale. Mwanakijiji, unamdanganya nani? Au ndio na tena unataka kuweka
picha ya mlango kwenye ukuta na unataka watu watoke? Ikiwa hii leo wakati bado
tupo pamoja bila ya kugombana – wakati bado tupo pamoja kama ndugu na kama
mtoto na baba you are already shortchanging us on the dividends of BoT,
je, hapo baadae baada ya kutafarikiana unadhani tutategemea kupata haki yetu
yoyote ile kutoka kwenu?
Ndugu Mwanakijiji, tunajua unajua kuwa 1+1 =2, lakini 82,840 out of 668,884 ni
ngapi %wise? - hio hutojua,
kwasababu hio ni hesabu kubwa na wewe hesabu inaonesha zinakupiga chenga!
On 5th of November your Finance and Economic Affairs deputy minister Janeth Mbene shamelessly
and carelessly refuted claims in the National Assembly that the government of
Zanzibar contributed to the start-up capital of the Bank of Tanzania (BoT).
Huyu waziri wenu mdogo anajitia kuwa
hajui kama Zanzibar ina-shares kwenye kuanzishwa kwa BoT. Definitely, huyu dada
hafahamu vipi BoT ilianza? Mzee Mtei sio bado yupo hai kwanini hamuulizi kama
anaona uvivu kufungua ma-files ya nyuma?
Kwanini Zanzibar haipewi haki yake? Hivyo hamjui
kuwa mlichukuwa haki yetu from the defunct East African Currency Board ili
tuanzishe BoT na leo mnatutoa?
Kwanini? Kwanini? Kwanini???? Sote tunania hio hio moja, sote tunataka kufika huko
huko mnakotaka kuenda nyinyi, kwanini wenzetu mnatumia circumlocution, deceit
and evasion ili mfike huko tuendako kwa haraka? Mjuwe kuwa 'haraka haraka haina
baraka'. Baada ya kufika huko mtakako, tunaona mtafika Switzerland tu kuficha
hizo mali zenu na mtabakia hapo hapo mkiwaneemesha wengine, wakati sisi ndugu
zenu tunakufa njaa! Matatizo mengi ya Muungano ni rahisi kuyatatua, lakini
wenzetu ni wazito kidogo kuutafuta ukweli.
Kwahivyo, Mwanakijiji don't talk about fair
distribution of the assets of the Union after the break up. Kama kupata basi
tungelipata hivi sasa our fair share, ili nasi tukafaidika. Kwa kweli, tunachotaka Wazanzibari
sio pesa au kugombania hizo assets za Muungano, bali uhuru wa kuamua mambo yetu
wenyewe bila ya kuja Kizota kupiga magoti!
Puerto Rico wamekubali kuwa jimbo la 51 la Marekani na wamekataa kuwa Dola
kamili kwasababu wanategemea kwamba kujiunga na Marekani itawaletea faida wao.
Nasi tulipojiunga na Tanganyika ile 1964 tulitegemea kuwa umoja ni nguvu na
kuwa tutafaidika na huu Muungano. Lakini, hivyo haikuwa, kwani Muungano
umetufanya tusisonge mbele. Tusisonge mbele kwa mambo mengi, lakini hapa
nitakutajia moja tu - nalo ni kuwa wenzetu mmezidi kupenda rushwa na ufisadi.
Nchi mnaifyonza kama mtu anavyoifyonza embe shomari na baadae mnakuenda kuficha
Switzerland na sisi mnatuacha wakavu. La kusikitisha zaidi ni kuwa, hata
mkielezwa nani anaeifyonza nchi wala hamjali na ndio kwanza mnawapigia makofi. Chenge,
Lowassa, etc pamoja na wale wote wezi wa Kiwira, BAE Radar, BoT Towers
(DSM+ZNZ), EPA Account, Richmond, Dowans, Ndege ya Rais, Buzwagi, ATCL plane
rental, etc, etc kama wangeliyafanya Unguja hayo waliyoyafanya huko kwenu basi
wangelipigwa risasi Mnazi Mmoja hadharani na wengine wangelikoma,
lakini nyinyi wenzetu ndio kwanza mnawachekelea na kuzidi kula nao sahani moja
na wengine hata urais watakuja kugombea hio 2015!
Mnajua vizuri sana kuwa yule Mhindi alie-organize
wizi wa pesa za Radar yupo Switzerland, lakini mnajifanya kama hamjayasikia
hayo. Ingelikuwa kiongozi wa UAMSHO
kakimbilia Switzerland hivi sasa tayari kupitia diplomatic channels mngelikuwa
mshamrejesha Zanzibar hata kwenye begi, lakini yule Mhindi mwizi anaetumbua
kule Switzerland mnaogopa kumsogelea, kwani mnajua kuwa atakutajeni nyinyi
nyote mlioshiriki katika wizi wa ile Radar. Zaidi, Chenge mwenyewe kakubali
kuwa vipo vijisenti nje, lakini hata hamjali kumpeleka kwenye vyombo vya sheria
ili akajieleza na mnachojali nyinyi zaidi ni kuwa Zanzibar iendelee kuwa chini
ya makucha yenu. Kwanini mnaing’ang’ania Zanzibar hivi? Kwani inanini zaidi?
Kama ni gesi na mafuta na nyinyi mnayo pia, tena mengi zaidi ya yetu.
Ni kweli kabisa kuwa ‘birds of a feather flock
together’. Mafisadi leo wanaoihujumu nchi kiuchumi mnawajua na mnawafumbia
macho, kwasababu ndio nyinyi wenyewe, lakini sisi tunaopigania uhuru wetu ili
tupate kunyanyua hali na maisha ya watu wetu kwa hicho kidogo tulichokuwanacho
mnatuwekea ngumu. Hata tukitaka kujiunga na mashirika ya nje ili tupate kukopa
mnatuwekea ngumu. Sasa sisi tutaendelea vipi ikiwa kwa kila jambo tuje kupiga
magoti kwenu kwanza? Hamtuonei huruma? Hayo magoti jamani sio mwisho
yatachubuka?
Wazee wanasema ukikaa na mlevi na wewe utakuwa
mlevi. Ukikaa na mwizi na wewe utakuwa mwizi. Ukikaa na fisadi na wewe utakuwa
fisadi. Hatutaki huu ufisadi wenu uvuke mipaka mpaka Visiwani na hili ndio
jambo moja linalotufanya tutake kutoka katika huu Muungano, ili tukuwachieni
mfanyiane ufisadi wenyewe kwa wenyewe mpaka mmalizane. Tanzania yetu imejaaliwa
na raslimali lakini yote inamalizikia Switzerland kutokana na ufisadi!
MKATABA
Ndugu Mwanakijiji, inaonesha neno ‘Mkataba’ linakuogopesha sana na kukutia
kiwewe. Kwahivyo, tunakuahidi kuwa hatutolitumia. Tutalitumia neno Katiba
(Constitution) ambalo inaonesha unalipenda – this way labda itasaidia kuipunguza
khofu uliyonayo. Anyway, kama ni Mkataba, Maktaba, Kutbu, Kitabu au Katiba au
chochote kile, Wazanzibari wanachotaka ni kuzuwia khatamu ya nchi yao, ili kila
jambo liweze kuamuliwa hapa hapa Zanzibar na sio Kizota. Kama baada ya
Wazanzibari kuwa na Dola yao patakuwa na
Mkataba au Katiba au kama hapatokuwa na chochote kile itakuwa ni sawa tu kwetu.
Kwahivyo, usijali sana hilo neno MKATABA – lakujali ni hio nia ya Wazanzibari
kutaka kuwa huru huria!
Hii mada inatupeleka kuzungumzia pia juu ya serikali
3. Pingamizi yako tunajua ni kuwa serikali 3 ni hasara. Hio sio kweli. Much can
be done with limited resources but with unlimited imaginations! Unlimited
imaginations Mwanakijiji hunazo. Ulichokuwa nacho wewe ni imaginations za kuficha
mapesa Switzerland tu basi! Tukiwa wenye mipango mizuri na sio ya wizi basi
gharama za kuiendesha serikali ya sasa hivi itaweza kuendesha hizo 3. Kutokana
na hesabu alizozitoa Mbunge Zitto Kabwe ni kuwa pesa zilizofichwa Switzerland
peke yake ni nyingi sana na kutokana na wingi wake zitaweza kuendesha sio
serikali 3 za Tanzania tu, bali zitaweza kuendesha serikali zote za Afrika
Mashariki kwa muda wa miaka 10. Kwahivyo, Mwanakijiji, pesa zipo za kuendesha
serikali 3, la umuhimu hivi sasa ni kuziendea mbio hizo pesa tu. Kama
hujaziendea mbio wewe basi ujue Zanzibar itakapokuwa Dola kamili itazidai hizo
pesa na ikizipata wewe hutoambulia kitu, kwasababu tunajua hizi pesa ni jasho
letu pia!
NIA
YA WAZANZIBARI
Nia yetu sisi Wazanzibari sio kuuvunja Muungano.
Muungano baina ya watu wa Bara na Visiwani hautovunjika milele, kwani
tushachanganya damu na damu siku zote ni nzito kuliko maji. Kitakachovunjika
kitakuwa ni jina tu la Tanzania, lakini mashirikiano baina ya watu wetu
yatabakia pale pale.
JINA
LA TANZANIA
Mwanakijiji, sote tunajua kuwa jina la Tanzania ni
zuri na tunalipenda sana. Itakuwa ngumu na kinyume kwenu nyinyi kujiita tena
Tanganyika, lakini Muungano ukivunjika sio nyinyi wala sio sisi watakaoweza
kulitumia jina la Tanzania isipokuwa kwenye mabuku ya historia tu.
Hapatokuwa na uwezekano wa watu wa Bara
kuamua kuendelea kujiita Watanzania. Wabara kuamua kuendelea kujiita Watanzania
- in
a diplomatic lingo that would amount to willfully fooling the world and that is
punishable by international laws!
Jamal Abdel Nasser alitamani (wakati umoja wa Egypt na Syria unavunjika ile 1961) ili
Egypt ibakie kuitwa United Arab Republic
(UAE) - due to his strong sentiments
of collective Pan-Arab nationalism, lakini haikuwezekana na ikabidi iendelee
kuitwa Egypt.
Rais wa Urusi Bw. Vladimir Putin inasemekana wakati
USSR inasambaratika na akiwa yeye kama boss wa KGB alitamani (kama unavyotamani
wewe), kuwa Urusi peke yake ichukue jina la USSR, lakini haikuwezekana na
ikabidi jina la USSR liende na maji.
Ushauri wetu ni kuwa, tumieni jina lile lile la Tanganyika kwani litaleta maana zaidi,
lakini kama hamtolikubali tena jina lenu la zamani kama ulivyoelezea huko nyuma
na mtataka kushikilia kuitwa Tanzania, basi labda baada ya Muungano kuvunjika
mjiite TANGANIA which is very close
to our beautiful name of Tanzania!
The name TANGANIA encompasses Tanzania, Tanganyika and even Tanga. What a great and a
beautiful name this will be !
Nduguyo Bakari Pandu Said (Kinyasini, Zanzibar).
Nimeisoma hii barua aliyopelekewa yule Ndugu Mwanakijiji. Ni ndefu na labda wengine hamna muda huo na kwahivyo mimi ninatoa muhtasari hapa chini:
ReplyDelete1. Wazanzibari wampelekea barua ya wazi kwa njia ya email Nd. Mwanakijiji!
2. Mwanakijiji afananishwa tena na mgonjwa wa akili.
3. Wasema Rais wa Zanzibar anachaguliwa Kizota na kwahivyo BLW halina nguvu ya kutoa mswada unaou-question Muungano.
4. Wasema Dr Shein akitaka kuitisha kura ya maoni kuhusu Muungano bila ya amri ya Bara ataitwa Kizota na atafukuzwa kama alivyofukuzwa Mhe Aboud Jumbe Mwinyi.
5. Waeleza kuwa Muungano ukivunjika jina la Tanzania litabakia kwenye mabuku ya historia tu na halitoweza kutumika tena.
6. Ufisadi ulioshamiri Bara ndio unaozidi kuchangia kutaka Waznz kujitoa kutoka kwenye Muungano.
7. Wasema mafisadi wa Kiwira, BAE Radar, BoT Towers, EPA, Richmond, Dowans, Ndege ya Rais, Buzwagi, ATCL Plane rental, etc etc wote wangelipigwa risasi hadhari kama wangefanya wizi wao Visiwani, lakini Bara bado wanapigiwa makofi na wengine watagombania urais 2015.
8. Wanastaajabu vipi yule Mhindi mwizi wa pesa za Radar bado hajarejeshwa Tanzania kutoka Switzerland. Walalamika kuwa kama kiongozi wa UAMSHO angelikimbilia Switzerland angelikuwa tayari kesharejeshwa Tanzania zamani hata kwenye begi.
9. Wamuuliza Mwanakijiji 82,840 out of 668,884 ni ngapi %wise? (0%, 4.5%, 12.4%, 100%) - Wamtaka achague jawabu sahihi katika hizo nne - kama mahesabu hayamchengi.
10. Wasema hawagombanii dividends za BoT bali wanataka wawe Dola kamili ili waweze kuamua mambo yao kule kule Zanzibar bila ya kuenda Kizota kupiga magoti, kwani waogopa kuwa mwisho magoti yao yatachubuka.
11. Wanasema hawaoni tofauti ya maneno haya: MKATABA, MAKTABA, KATIBA, KUTBU au KITABU. Neno lolote linaweza kutumika ambalo litaonesha kuwa wao wanachotaka ni kuwa Dola kamili itakayoweza kushirikiana na mashirika tele ya nje bila ya kutaka ushauri wa Kizota.
12. Waeleza kuwa kama wangelikuwa huru kama South Sudan, Puerto Rico au Scotland, basi suala la Muungano lingelikwisha zamani.
13. Waitaka serikali ya Muungano iwape ‘a level playing field’ ili wafunge 6-5!
14. Wasema Muungano wa Visiwani na Bara hautovunjika, kwani ni Muungano wa damu. Litakalovunjika itakuwa ni jina la Tanzania tu!
15. Mwishowe, wamuambia Ndugu Mwanakijiji:
• To stand up for justice between Zanzibar & Mainland or shut up!
• To stop being a political play-boy over union issues!
Muandishi hapa umenikuna sana na natarajia umewakuna Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao. Umewaeleza hawa jamaa nini wanachokitaka na nini wasichokitaka Wazanzibari kwa sababu nafikiri wengi wao hawaelewi hasa nini tunakidai. Naamini kila atakaeisoma hii barua atapata kuelewa kwa nini Tunataka tuachiwe tupumue.
ReplyDeleteNa mimi nawasihi Mwanakijiji pamoja na Watanganyika wenzake kama kuna kitu ambacho hawakukielewa waombe maelezo tutawapa maelezo ya kina badala ya kuropoka mambo wasiyoyaelewa.
Suala moja nafurahi sana kwamba umelitaja ambalo maranyingi huwa halitajwi ingawa watu wanalijua ni lile la uchaguzi wa raisi wa Zanzibar kuchaguliwa Dodoma. Inabidi wajue sasa kwamba chaguzi zote kuu tangu 1995 raisi wa Zanzibar amekua akichaguliwa Dodoma.
Hilo limetuchosha sasa tuna taka turuhusiwe kuchagua raisi wetu wenyewe hatutaki tena mamluki.