Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, January 20, 2013

Dk Slaa: Tutaipeleka puta CCM hadi 2015

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa akiongozana na viongozi wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama hicho (CHASO) wakati wa ufunguzi wa Kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu lililofanyika katika Ukumbi wa Msimbazi jijini Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix 


Posted  Jumapili,Januari20  2013  saa 8:49 AM
KWA UFUPI
AHUTUBIA WANAFUNZI WA VYUO,AAHIDI KUHAMASISHA WANANCHI KUDAI HAKI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa amesema kuwa kuanzia mwaka huu hadi 2015, chama chake kitaipeleka mchakamchaka CCM, kwa kuwa chama chake kimefanikiwa kuwaamsha Watanzania.
Alisema kwamba Watanzania sasa wameamka na kutambua utajiri wa nchi yao na jinsi   rasilimali zinavyotoroshwa nje ya nchi na kuanza kudai kufaidika nazo kwa nguvu. Hivyo Chadema kitaitumia fursa hiyo kuipeleka puta CCM, lengo likiwa kuhakikisha kila Mtanzania anaishi maisha bora.
Dk Slaa alisema hayo alipokuwa akizungumza katika kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini, ambao ni wafuasi wa chama hicho (CHASO), lililofanyika Dar es Salaam jana.

Alieleza kuwa kinachotokea mikoa ya Lindi na Mtwara, pamoja na maandamano ya hivi karibuni ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ni majibu tosha kwa CCM, kwamba mikutano ya Chadema iliyofanyika mikoa mbalimbali nchini imewaamsha wananchi.
Wanafunzi zaidi ya 500 walihudhuria kongamano hilo kutoka  IFM, Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) na  Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), pamoja na vyuo mbalimbali vilivyopo Dar es Salaam na mikoani.
Desemba 18 mwaka jana Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alisema kuwa mwaka huu utakuwa ni wa kuunganisha nguvu ya umma kitaifa, baada ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa kuzifanyia kazi hoja mbalimbali zinazotolewa na chama hicho.
Dk Slaa ambaye alitumia saa 1:06 kuzungumza na wanafunzi hao, alisema kuwa elimu ya uraia waliyoitoa kwa wananchi katika mikutano ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), pamoja na Operesheni Sangara, wamefanikiwa kwa asilimia 99.
“Tumewapa elimu ya uraia wananchi katika mikoa yote nchini na sasa wanajua haki zao,.Hiyo ni kazi na mikutano yetu pamoja na maandamano tuliyoyafanya” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Nawapongeza wanafunzi wa IFM kwa kuandamana, najua wapo watakaosema nachochea maandamano, lakini wanatakiwa kujua kwamba wanafunzi hawa walikuwa na haki, haiwezekani wanabakwa kisha wakae kimya, tena wametoa taarifa polisi na hakuna kilichofanyika.”
Mbali na kutaka Mkuu wa Jeshi la  Polisi nchini, IGP Said Mwema na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kujiuzulu kwa kitendo cha kuamuru  wanafunzi wa IFM kupigwa wakati walikuwa wakililia usalama wao, alisema kwamba kuna tofauti kubwa kati ya vurugu na kudai haki za msingi.
“Inakuwaje polisi wanawapiga mabomu wanafunzi wanaofanya maandamano, lakini wanashindwa kuzuia Twiga wanaotoroshwa nje ya nchi, tuungane, tushirikiane na tupige kelele, ili mali zetu zirudi,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Wananchi wa Mtwara na Lindi sasa wanaandamana kutaka gesi iwanufaishe wao kwanza.
Hayo yote ni matokeo ya elimu ya uraia tuliyoitoa nchi nzima. Hivi sasa wananchi hawaogopi wanasema ukweli.”
Alisema kitendo cha Watanzania kudai rasilimali za nchi yao kitafanya rasilimali hizo zitumike kwa maendeleo ya wananchi.
Alifafanua kuwa rasilimali za nchi ya Japan, Canada na Italia zilitumika kujenga nchi hizo na sasa zina utajiri mkubwa, lakini rasilimali za Tanzania zinapakizwa katika ndege ya kupelekwa kusikojulikana.
“Rais Paul Kagame wa Rwanda aliibadilisha nchi hiyo kwa sababu hana utani, kwetu Tanzania watu hawawajibishwi, utani umejaa kila kona,” alisema Dk Slaa.
Aliongeza kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kwa kuangalia maendeleo ya mkoa mmoja tu, huku akisisitiza sera ya majimbo kuwa ni sahihi na ikitumika itaweza kuliletea taifa maendeleo makubwa.
Dk Slaa alisema kwamba Serikali ya CCM iliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini hadi sasa kuna Watanzania wanaoshindwa kulipa kodi ya nyumba na wanakula mlo mmoja kwa siku.
“Ngoja niwaeleze kitu, tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 3 ya matajiri nchini wanamiliki asilimia 97 ya rasilimali za taifa hili, tutaipigisha mchakamchaka CCM mwaka huu hadi 2015,” alisema Dk Slaa.
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya alisema kuwa kuna mchezo unafanywa na CCM ili Katiba Mpya iwe na mlengo wa chama hicho na kufafanua kuwa wanasubiri rasimu ya Katiba itolewe na kwamba ikiwa itakuwa sawa na mapendekeo yaliyotolewa na chama hicho tawala, hawataikubali.
Akizungumzia nidhamu ndani ya chama hicho alisema: “Chadema ni tumaini la Watanzania, hivyo hatuwezi kuwa na wanachama au viongozi wasio na nidhamu, kama ni demokrasia basi inatakiwa kuishia pale inapoishia pua yao.”
Urais 2015
Akizungumzia urais 2015, kiongozi huyo alisema kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010,  kazi aliyopewa ni kukijenga chama hicho na siyo vinginevyo.
“Tangu 2010 kazi niliyopewa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ni kukijenga chama na siyo kuangalia urais, hao wanaozungumzia urais shauri yao,” alisema Dk Slaa.
Chanzo: Mwananchi

No comments :

Post a Comment