TAMKO LA SHURA YA MAIMAMU MKOA MTWARA KUHUSU SAKATA LA GESI ASILIA
ILIYOPO MSIMBATI –MKOANI MTWARA, TAREHE 18/01/2013.
Yaliyomo:
1. Utangulizi
2. Tatizo la Gesi Mtwara
3. Majibu ya Serikali kwa madai ya WanaMtwara na Athari zake
4. Ukweli kuhusu Tatizo la Gesi Mtwara
5. Maoni na Msimamo wa Shura ya Maimam Mtwara Juu ya Kadhia ya Gesi
6. Utangulizi
Sifa zote njema zinamstahili Allah (Subhanahuwata’ala) ambaye uhai wa
nafsi zetu umo mikononi mwake naye ni msimamia kila jambo na Ambaye
ametuteremshia mwongozo ili tuweze kusimamia haki katika ardhi na
hatimaye kuishi maisha ya wema na uadilifu. Rehma na Amani zimuendee
Mtume wake mtukufu Muhammad (Swalallahu-alaihi-Wasalaam).
Allah(s.w) anasema:
“(Vyote) vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ni vya
MwenyeziMungu.Na kama mkidhihirisha yaliyomo katika nyoyo zenu,au
mkiyaficha,MwenyeziMungu atakutakeni hesabu ya (yote) hayo;kisha
amsamehe amtakaye(kwa kuwa katubia) na amuadhibu amtakaye(kwa kuwa
hakutubia).Na MwenyeziMungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu”( Qur an
2:284)Sote tunafahamu kuwa kwa sasa wananchi wa Mtwara wanaendelea
kuilalamikia serikari kuhusu mpango wake wa kusafirisha gesi kutoka
Mtwara kwenda Dar es salaam. Wananchi wa Mtwara walijitokeza kama
kundi Tarehe 27 mwezi wa 12 mwaka jana (2012) kuieleza serikali kuwa
wanapinga mpango huo wa kusafirishwa gesi unaotekelezwa kupitia mradi
wa bomba wa gesi ambao kwa mujibu wa serikali ujenzi wake utakamilika
katika kipindi cha miezi kumi na minane.
Baada ya maandamano hayo makubwa sasa suala la gesi limechukua sura ya
mjadala wa kitaifa kwani kila kona ya Tanzania sasa inajadili suala
hili kwa namna mbalimbali na kwa hapa Mtwara hali inazidi kuwa ngumu
zaidi kwani wananchi wanazidi kujizatiti zaidi kimisimamo kuwa gesi
haitoki na ikibidi basi wako tayari kufa na hilo likikaririwa katika
kauli mbiu maarufu kwa sasa ya GESI KWANZA UHAI BAADAE.
Sisi shura ya Maimam Mkoa wa Mtwara tumeona ni vema tutoe Tamko letu
baada ya uchunguzi wa kina juu ya Kadhia hii ya gesi kwa lengo la
kuishauri na kuinasihi serikali juu ya nini kifanyike ili kuleta hali
ya amani katika misingi ya haki na uadilifu. Kuna sababu kuu nne (4)
ambazo zimetusukuma kutoa Tamko hili.
Kwanza, tumeona kuwa sisi ni sehemu ya jamii ya WanaMtwara na ni
watanzania ambao kwa uelewa wetu juu ya kadhia hii tuna haki na wajibu
wa kutoa msimamo wetu juu ya kadhia hii ili dhima na wajibu ya kulinda
amani katika nchi hii tuwe tumeitekeleze kwani ni haki yetu.
Pili, Mpaka sasa kumekuwa na upotoshaji mkubwa juu ya kile
kinachoendelea katika kadhia hii ya gesi kuanzia kwa viongozi wa
serikali na hata baadhi ya watu binafsi wanojitokeza kutoa maelezo,
misimamo au maoni yao kuhusu kadhia hii.
Tatu, mpaka sasa serikali haijaonesha dhamira ya dhati ya kulipatia
ufumbuzi suala hili na kuamua kulipuuza kitu ambacho ni hatari kwani
kwa hali jinsi ilivyo amani inaweza kuvurugika wakati wowote kama hali
itaendelea kuwa kama ilivyo sasa.
Nne, sisi tuna uelewa mkubwa wa misimamo na hisia za WanaMtwara juu ya
suala la gesi kwani tunaishi nao na tunaona na kusikia hisia zao
wanazozidhihirisha kwa vinywa vyao endapo wataendelea kupuuzwa. Hata
hayo maandamano ya tarehe 27 si mwanzo wa malalamiko ila ni kilele tu
cha kile ambacho kimekuwa kikaendelea chini kwa chini tangu pale
ambapo wananchi walihakikishiwa kuwa sasa gesi inasafirishwa na
kupelekwa Dar es Salaam. Kwa hiyo tunaona wazi kuwa kwa namna serikali
yetu ilivyo haitaweza kukabiliana na hali hiyo pale machafuko
yatakapoanza.
7. Tatizo la Gesi Mtwara
Kimsingi, tatizo la gesi Mtwara ni fupi kueleweka na liko wazi.
Serikali ndio kiini cha tatizo hili na sio wananchi wa Mtwara.
Serikali imekuja na mpango wa kuisafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda
Dar es Salaam. Imetangaza na kuzindua mradi wa bomba la gesi
litakalojengwa kwa miezi kumi na nane (18) kutoka Mtwara mpaka Dar es
salaam. Wananchi wa Mtwara wanapinga mradi huo na wazo au uamuzi mzima
wa kuisafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na kuipeleka sehemu yeyote
ile Tanzania na Dar es Salaam ikiwepo bila Mtwara kunufaika kwanza na
gesi hiyo asilia. Kwa msingi huu wanachotaka wao ni kwamba kituo cha
kuchakata gesi hiyo asilia kijengwe Mtwara badala ya Kinyerezi jijini
Dar es Salaam. Msingi wa dai hili ni kwamba wananchi wa Mtwara
wanaamini kuwa kituo hicho cha kuchakata gesi asilia kama kitajengwa
Mtwara kitatoa fursa kubwa ya kushawishi wawekezaji ambao wataweza
kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi ya gesi asilia na hivyo
kuchochea maendeleo ya
Mtwara kwa ujumla. Kwa hiyo kama gesi hii itaanza kufanyiwa kazi
mkoani Mtwara kwanza kwa namna hii, hapo wananchi wataridhia baadaye
gesi hiyo kusafirishwa katika mikoa mingine ya nchi ikiwa imechakatwa
kwa ajili ya matumizi ya Kitaifa ambayo WanaMtwara hawayapingi.
Kwa hiyo hii ndio HOJA ya msingi ya wananchi wa Mtwara na kwamba kwa
hoja hii, ni wazi kwamba wananchi wa Mtwara si wabinasfi na wala sio
wachoyo na hawapingi watu wengine katika maeneo mengine ya nchi
kunufaika na gesi hii. Pia kwa hoja hii wananchi wa Mtwara hawapingi
tu kusafirishwa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kwa UJINGA.
Huu sio ujinga bali wananchi wamesimamisha HOJA ambayo inatakiwa
kufanyiwa kazi kwa uzito uleule wa namna HOJA ilivyosimama.
8. Majibu ya Serikali kwa madai ya WanaMtwara na Athari zake
9. Majibu ya Serikali
Kwa mujibu wa WanaMtwara, mpaka sasa serikali haijatoa jibu la msingi
wala ufafanuzi unaoeleweka dhidi ya HOJA ya WanaMtwara kuhusu gesi
kuanzia katika mkoa, wizara yenye dhamana na masuala ya gesi na hata
mheshimiwa raisi.
Mkuu wa mkoa yeye hakutaka kuwa na maneno mengi bali aliongea kwa
ufupi tu na kurudiarudia kauli yake. “Alisema kuwa watu wa Mtwara ni
wapuuzi kwa madai yao hayo”. Akaendelea tena kidogo kwamba “tena
amewasamehe kuwaita wapuuzi walistahili kuitwa wahaini”. Kwa hiyo HOJA
madhubuti iliyotolewa na wananchi wa Mtwara ilijibiwa kirahisi tu
kiasi hicho kwa kejeli na jeuri lakini hatimaye kejeli na jeuri hizo
za mkuu wa mkoa wa Mtwara hazikujaribu hata chembe kujibu HOJA nzito
ya wananchi. Yeye akawa amemaliza kazi na kuwaachia wakubwa wake.
Waziri wa Nishati na madini naye akaja na mlolongo mrefu wa maelezo
yasiyoshikana na hata kuelewaka kwa mnasaba wa HOJA ya wananchi wa
Mtwara. Kasema Dar es salaam kuna viwanda vingi kuliko Mtwara.
Matumizi ya gesi Mtwara ni madogo kuliko Dar es Salaam. Gesi
imegunduliwa mbali na Mtwara kwa hiyo wananchi wa Mtwara hawapaswi
kulalamika na mengine mengi mfano wa hayo. Kimsingi na Mheshimiwa
waziri nae akapita njia ileile ya mkuu wa mkoa na hatimaye na yeye
hakujibu HOJA ya wananchi kama ilivyosimama.
Mheshimiwa raisi naye akatoa maelezo yake katika hotuba yake ya mwisho
wa mwezi wa kumi na mbili mwaka jana (2012). Kubwa alilolifanya ni
kusisitiza tu kwamba suala la kutosafirishwa gesi kwenda Dar es Salaam
HALIKUBALIKI. Naye katika maelezo yake aligusagusa tu vitu
fulanifulani kama vile umuhimu wa Dar es Salaam kwa kuwa inachangia
sehemu kubwa ya pato la taifa (asiliamia 80) na kwamba viwanda vingi
vipo Dar es salaam.
Pia alisisitiza kuwa sera ya rasilimali iko wazi kwamba lasirimali
zote ni mali ya taifa. Maelezo yake yote ilikuwa ya kujaribu
kuhalalisha mpango wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es
Salaam na hatimaye hakuweza kutoa majibu ya HOJA ya wananchi Mtwara.
Kwa hiyo mpaka sasa tangu alipoanza kuongea mkuu wa mkoa wa Mtwara,
waziri wa Nishati na madini na Mheshimiwa raisi wananchi wa Mtwara
hawajapata jibu la msingi kwa HOJA yao nzito juu ya Gesi.
10. Athari za Majibu ya Serikali
Kimsingi, wananchi wa Mtwara baada ya kuchambua Majibu ya Viongozi wa
serikari hawajaona maelezo yanayojibu HOJA yao. Kwa sababu zifuatazo:
Kwanza, majibu yote tangu ya mkuu wa mkoa, waziri na raisi yanajaribu
kueleza vitu vinginine na sio hoja yenyewe ya wananchi wa Mtwara.
Majibu yote yanajikita katika kuelezea upingaji wa kusafirisha gesi
kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam lakini sababu ya wananchi wa Mtwara
kupinga kusafirishwa gesi haiguswi.
Wananchi wanataka kituo cha kuchakata gesi asilia na ujenzi wa mtambo
wa kufua umeme wa MEGAWATT 300 kijengwe Mtwara na sio Kinyerezi Dar es
salaam kwa sababu kikijengwa Mtwara kitachochea maendeleo. Kwa upande
mwingine, kwa kuwa wananchi wanaamini kuwa gesi ghafi hiyo
ikisafirishwa kwenda Dar es Salaam wao hawatanufaika (kwa msingi ule
wa kujengwa kituo cha kuchata gesi Mtwara), serikali ilitakiwa ijikite
katika kuwaonesha wananchi kinaga ubaga namna gesi hiyo
itakavyoendelea kuchochea maendeleo ya Mtwara hata kama ikisafirishwa
kwenda Dar es Salaam na sio kusema sema tu kwamba wananchi watanufaika
bila kuweka wazi watanufaikaje. Kwa Majibu haya, wananchi wa Mtwara
wanaona kuwa serikali yao haikujipanga kuona Mtwara wananufaika na
gesi na ndio maana wanaikwepa HOJA yao.
Pili, serikali pamoja na kushindwa kutoa majibu ya msingi katika hoja
ya wanaMtwara, imekuwa ikitumia muda mwingi kuwaeleza wananchi wa
maeneo mengine ya nchi kupitia vyombo vya habari kama vile, vipindi
vya televisheni, magazeti na hotuba na kuwaacha wahusika wenyewe ambao
ni wakazi wa Mtwara. Rais, na sio Waziri wa Nishati na madini,
alitakiwa aje azungumze na wananchi ili wananchi wajibiwe HOJA yao
kama ilivyo.
Tatu, serikali imetoa shutuma zisizo za kweli kwa wananchi wa Mtwara.
Hata kama serikali haipendezwi na madai ya WanaMtwara bado ilipaswa
ieleze kile wanachokidai na sio kuwabambikia hoja tofauti. Serikali
imesema wananchi wa Mtwara WANAPINGA gesi kusafirishwa kwenda Dar es
Salaam na kuishia hapo. Kufanya hivyo kumeongeza chuki kwa wananchi wa
Mtwara na wanaona kuwa serikali inatafuta uhalali wa kupitisha jambo
lake. Inajenga mazingira ya wananchi wa Mtwara waonekane wabinafsi,
wachoyo na hatimaye waiunge mkono katika kupuuza dai la wananchi wa
Mtwara. Lakini kinyume chake hata wananchi wa maeneo mengine wameona
dosari hiyo ya serikali na wao kupitia majukwaa mbalimbali ya vyombo
vya habari wanajaribu kuwaelewesha watanzania wengine kuhusu HOJA ya
msingi ya wananchi wa Mtwara. Kwa hali hii serikali tunaiona inapoteza
heshma yake na uaminifu si tu kwa wananchi wa Mtwara bali kwa kila
Mtazania makini anayeitakia heri nchi yake.
Nne, serikali imekosea kuona kuwa msingi wa madai ya WanaMtwara ni
uchochezi wa wanasiasa. Serikali inapaswa kufahamu kuwa wanasiasa ni
wadandiaji wazuri wa hoja mbalimbali za kijamii baada ya kuibuka
kwake. Kilichoanza hapa ni manung’uniko ya wananchi juu ya
kusafirishwa kwa gesi na baada ya wanasiasa kuona kuwa hakuna
anayewasemea wananchi ndio wakapenya hapo na kuwahamasisha juu ya
namna ya kupaza sauti zao lakini tatizo lilikuwepo hata kama tungekuwa
tunaongozwa na chama kimoja. Kwa hiyo hili ni dai la WANANCHI WA
MTWARA sio dai la wanasiasa.
Kwa hiyo kwa ujumla majibu ya serikali kwa wananchi yamezidi kuongeza
tatizo na wananchi wa Mtwara wameona kuwa serikali yao imeamua
kuwapuuza. Na kwa sababu serikali imeshindwa kutoa majibu sahihi kwa
HOJA ya wananchi ya Mtwara, kwa kufanya hivyo imehalalisha kila fikra
itakayokuja katika kichwa cha Mwananchi wa Mtwara kuhusu hatua za
serikali kusafirisha gesi iwe sahihi. Na fikra kubwa waliyonayo
wananchi wa Mtwara kwa sasa ni kwamba serikali imeamua kuwadhuluma
neema iliyopatikana katika maeneo yao na inawapelekea walewale
wachache wakanufaike na neema hiyo. Na kilele cha mtazamo huu ni ile
kauli mbio yao ya GESI KWANZA UHAI BAADAYE. Yaani kwao wao ni bora
kufa kuliko kuona gesi inasafirishwa kwenda Dar es salaam katika namna
ambayo wao hawakubaliani nayo. Wanaona baada ya hapo wataendelea
kunyanyaswa na mwisho watajinyonga kwa udhalili kwa hiyo wanaona ni
bora wafe na GESI.
Kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuszi bwana James Mbatia mjini
Mtwar hivi karibuni pamoja na kuwekewa magogo naibu waziri wa Nishati
na madini Bwana Simbachawene kule Msimbati ni ishara tu ya madhara ya
serikali kupuuzia madai ya WanaMtwara.
11. Ukweli kuhusu Tatizo la Gesi Mtwara
Kwa uzoefu tulio nao kwa wananchi wa Mtwara tangu ukoloni hawajawahi
kufaidi matunda ya maendeleo ya kijamii na wamebaki kuwa duni
ukilinganisha na mikoa mengine. Serikali za kikoloni (ya Wajerumani na
ya Waingereza) zilitumia nguvu kazi ya wananchi wa Mtwara pamoja na
rasilimali zao kwa ajili ya kuendeleza maeneo mengine ya Tanzania na
kuwaacha watu wa mikoa ya kusini wakiwa hoi kwa umasikini wa kutupwa.
Baada ya Uhuru, serikali pia imefuata nyayo zilezile za kulipuuza eneo
hili la kusini mwa Tanzania na kulifanya liwe msindikizaji wa
maendeleo kwa mikoa mingine.
Katika sura hii, tafsiri ya haraka waliyokuwa nayo wananchi wa Mtwara
kuhusu hatua ya serikali kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam bila
kujali madai ya wananchi wa Mtwara ni kuwa huu ni muendelezo uleule wa
kubeza maendeleo ya mikoa ya kusini. Kwao wao hapa hawaoni jipya ila
wao ndio wameamua kuja na staili mpya ya kudai maendeleo yao na
KUPINGA HUJUMA ya kimaendeleo ambayo wamekuwa wakifanyiwa kipindi
kirefu sasa. Wananchi wa Mtwara wanamlolongo ufuatao wa Mashaka na
MATATIZO waliyoyapata katika historia ya maisha yao tangu ukoloni:
o Katika kipindi cha ukoloni wa wajerumani (1885-1917), wananchi wa
mikoa ya kusini walitumika kama nguvu kazi ya kuendeleza maeneo
mengine yenye migodi na mashamba. Wengi walinyang’anywa ardhi zao na
kulazimishwa kuacha familia zao na kwenda Kufanya kazi kwa nguvu
katika maeneo mengine. Katika sura hii, mikoa ya kusini iliachwa bila
kuendelezwa ili iwe kitovu cha kutoa wafanyakazi (manamba) wa kutumika
katika mashamba ya wakoloni katika maeneo mengine ya nchi. Ushiriki wa
watu wa Mtwara katika vita ya majimaji ilikuwa ni kielelezo cha
kupinga dhulma dhidi yao.
o Katika utawala wa waingereza, mwendo ulikuwa ni uleule ambapo
waingireza Walipewa jukumu la kuitawala Tanganyika wakati huo na
League of Nations kwa hiyo hakukuwa na mkakati wowote wa kuendeleza
mikoa ya kusini kwa uchumi. Mikoa ya kusini ilitengwa na kubaguliwa
kiuchumi. Mwandishi wa Kifaranza Libenow (1971) katika kitabu chake
Colonial Rule and Political Development in Tanzania: The Case of
Makonde ukurasa wa 11 anaandika kwamba waingereza waliita Mtwara kuwa
ni “Cinderella Region of a Cenderalla Territory” yaani eneo
lililotengwa/kubaguliwa la ukanda uliotengwa/kubaguliwa. Waingereza
waliweka msimamo kuwa Mtwara na kusini kwa ujumla si sehemu ya
kuendelezwa kiuchumi na walifuata nyao zilezile za wajerumani.
o Baada ya Uhuru, wananchi wa Mtwara na kusini kwa ujumla wakapata
bahati mbaya nyingine kwani ndoto zao za kudhani kuwa wataendelezwa
kiuchumi Ndani ya Tanzania huru ziliota mbawa. Serikali ya Tanganyika
na baadaye Tanzania ilifuata nyayo zilezile za wakoloni wa kijerumani
na waingereza. Kwanza, mikoa ya kusini ikatengwa tena kwa shughuli
nyingine ya uslama wa nchi. Kipindi hiki Mikoa ya kusini ikawa ni
uwanja wa mapambano ya kuzikomboa nchi za kusini mwa Afrika ili wapate
Uhuru. Miundombinu ikazidi kuwa mibovu na hakukuwa na maendeleo yeyote
ya maana. Kwa ujumla wananchi wanalalamika juu ya haya:
o Mtwara ina Bandari yenye kina kirefu katika Afrika ya mashariki
yote lakini mpaka sasa mipango ya kuiendeleza imekuwa ni
kizungurumkuti. Wananchi wana taarifa kuwa mipango ya kuiendeleza
Bandari ya Mtwara imepindishwa na kupelekwa Bagamoyo.
o Wananchi wanakumbuka kwa uchungu zao lao la biashara la muhogo
ambalo serikali ya Tanzania huru imeliacha linakufa kuwa zao la
biashara. Wakulima wengi wanalima mihogo mingi na wanaishia kuitupa tu
baada ya kuoza maana si tu kwamba haina soko bali hata teknolojia ya
kulitunza kwa muda mrefu hawana. Mashamba wanayo na wanalima kwa bidii
wanavuna mihogo mingi lakini wa kumuuzia tayari serikali ilishampoteza
na haina mpango wa kulifufua zao hili kama zao la biashara.
o Wananchi wa Mtwara na kusini kwa ujumla wana kilio cha muda mrefu
cha zao la korosho na mpaka sasa serikali inababaisha tu haina mpango
wowote wa kuboresha soko la zao hili. Wananchi sasa wanapomaliza
kuvuna korosho zao wanaambulia vikaratasi tu na kutakiwa wasubiri pesa
zao kwa muda mrefu bila kuzipata. Ingawa ni jambo liliowazi kuwa zao
la korosho linachangia kiasi kikubwa tu cha fedha katika serikali. Kwa
mfano, kuna takwimu zinaonesha kuwa Katika Mwaka wa Uchumi unaoishia
Novemba 2012, Korosho imeliingizia Taifa jumla ya dola za Kimarekani
151 milioni sawa na shingi trillion mia mbili arobaini na moja na
million mia sita (TZsh241,600,000,000). Katika mwaka 2011 zao hili
liliingiza dola 130 milioni sawa na trilioni mia mbili na nane
(208,000,000,000) wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni tu sawa na
shingi trillion themanini na nne na milioni mia nane
(84,800,000,000).
o Wananchi wa Mtwara na kusini kwa ujumla wanazidi kulia tu na
kusuasua kwa ujenzi wa Barabara ya Mtwara-Lindi-Dar es Salaam.
Wanazidi kuumia wanapoona ile mikoa inoyoheshimiwa na serikali ikiwa
na Barabara nzuri zinazopitika tena ujenzi wake umekamilika kwa muda
mfupi sana. Miaka minane ya Mh. Rais Kikwete zile kilomita 60 za
barabara kutoka Ndundu mpaka Somanga hazijaisha lakini gesi anataka
kuiwekea bomba na mradi ukamilike kwa miezi 18.
o Wananchi wameshuudia reli ya kusini iking’olewa bila sababu za
msingi na huku ikijulikana kuwa reli ni moja ya miundombinu muhimu
katika kuchochea uchumi na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Reli
haikung’olewa katika mikoa ambayo serikali inaiheshimu.
o Wananchi wa Mtwara wameshuhudi mashine ya maji kitangali Newala
ikiondolewa na kupelekwa Dodoma ambayo ilikuwa msaada kutoka Finland.
o Wananchi wa Mtwara wameshuhudia kiwanda cha samaki Mtwara
kikiondolewa na kupelekwa Dar es Salaam.
o Wananchi wa Mtwara wameshuhudia taa za mwanga mkali za uwanja wa
ndege Mtwara ziking’olewa na kupelekwa Arusha.
o Wananchi wa Mtwara wameshuhudia mkataba wa kutumika bandari ya
Mtwara na Malawi kibiashara ukipindishwa na kupelekwa Bagamoyo.
o Wananchi wa Mtwara wamekaa na giza kwa muda mrefu na giza hilo
limechangia kutokuwepo kwa kichocheo cha uchumi kwa kukosekana umeme
wenye uhakika. Ni hivi karibuni tu baada ya kugunduliwa gesi na
kumekuwepo na nishati ya umeme ambao hautoshi kwa maana ya kumfanya
mjasriamali mwenye mtaji kuweza kuwekeza Mtwara katika sekta ya
viwanda.
Mwenyezi Mungu anasema:-
“Kwa hakika MwenyeziMungu anaamrisha uadilifu,na kufanya ihsani,na
kuwapa jamaa(na wengineo),na anakataza uchafu na uovu,na
dhuluma.Anakunasihini ili mpate kufahamu(mfuate)”(Qur’an 16:90)
Amesema Mtume(s.a.w) “Mwenye kuuona uovu mmoja wenu basi na auondoshe
kwa mkono wake ,kama akishindwa basi atumie ulimi wake kushajiisha
uovu uondoke na akishindwa basi achukie moyoni mwake na huko kuchukia
ni udhaifu wa imani”(Bukhari na Muslim)
Wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa muda mrefu wamekuwa wakichukia tu
mioyoni mwao maovu na madhila yote waliyokuwa wakifanyiwa na serikali
lakini sasa imefika wakati tuseme na tudhihirishe maovu hayo waziwazi
ili asaa viongozi wajirekebishe na wawafanye uadilifu kwa watu wao
kama si hivyo hatua inayofuata kwa mujibu wa hadithi ni kutumia mkono
kuondosha uovu.
Kwa hiyo, huu ndio mlolongo wa madhila ambayo wamekumbana nayo
wananchi wa Mtwara. Wao wanaamini kwamba kutoendelezwa kwa maneo yao
ni matokeo tu ya kiubaguzi kwa kuwa serikali tangu ile ya kikoloni
mpaka hii ya leo inaliona eneo hili kama ni eneo ambalo si muhimu na
hivyo ni haki yao kubaki nyuma. Katikati ya mashaka hayo Mwenyezi
Mungu amejaalia kuwepo kwa gesi asilia. Kwa Ugunduzi huu wa gesi watu
wa Mtwara waliamini kuwa sasa hivi serikali itaona aibu na kuwa
waadilifu na kwamba itatumia gesi hii kama kichocheo kilicholetwa na
Mwenyezi Mungu ili kukuza maendeleo ya Mkoa wa Mtwara na Lindi.
Walikuwa na matumaini hayo kupitia kauli na ahadi za viongozi
mbalimbali akiwemo rais mstaafu wa awamu ya tatu na hata Mh.Rais
Kikwete mwenyewe kwamba ukombozi wa kiuchumi sasa umefika kwa mkoa wa
Mtwara pia Ilani ya chama cha mapinduzi(2010) katika ibara ya 63(h) na
(k) ilianisha miradi ya kinyerezi(240MW) na mradi wa Mnazi bay(300MW)
kama miradi miwili tofauti inayojitegemea. Mwenyezi Mungu nasema:
“Na timizeni ahadi mnazozitoa kwa jina la MwenyeziMungu
mnapoahidi;wala msivunje hizo ahadi baada ya kuzithubutisha,hali
mmekwisha mfanya MwenyeziMungu kuwa shahidi wenu.Hakika MwenyeziMungu
anayajua yote mnayoyayafanya”(Qur’an 16:91)
Sasa ghafla, wanakutana na mpango wa kustukiza wa serikali kutaka
kusafirisha gesi hiyo kwenda Dar es Salaam bila kueleza kwa nini kituo
cha kufulia umeme unaotokana na gesi asilia inakopatikana gesi hiyo
kisijengwe Mtwara?. Wanapojaribu kuihoji serikali wanaambulia matusi,
kejeli na kupuuzwa kutoka kwa viongozi wao waliowategemea kuwatetea.
Kwao wanaona ni hujuma tu wanataka kufanyiwa kama walivyofanyiwa huko
nyuma na ndio maana wameamua KUFA na GESI indepo na mara hii serikali
itawapuuza. Serikali imefikia upeo wa juu wa kuwapuuza wana Mtwara na
WanaMtwara nao wamefikia upeo wa juu wa uvumilivu na ndio maana
wanasema GESI KWANZA UHAI BAADAYE. Haya ndio mazingira halisi ambayo
ndiyo KIINI cha mgogoro wa gesi Mtwara. Sio wanasiasa bali ni historia
ya kudharauliwa ndio yaliyoibua mgogoro huu wa gesi kama tulivyoeleza
hapo juu. WanaMtwara wana mfano wa gesi ya Songosongo inayopelekwa Dar
es Salaam. Zipo taarifa zinazoelezea kwamba kodi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Kilwa asilimi 0.3 (0.3%) ilikuwa inalipwa Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ni baada ya juhudi
za mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati ndio kodi
ikaanza kulipwa Kilwa.
25. Maoni na Msimamo wa Shura ya Maimam Mtwara
5.1 Msimamo wa Shura
Shura ya Maimam Mtwara imesikitishwa na kuwepo kwa mgogoro kati wa
wananchi wa Mtwara na serikali katika sula la gesi. Msimamo wetu
kuhusu Kadhia hii ya gesi ni kwamba serikali imeshindwa kutekeleza
wajibu wake kuhusu suala la gesi kwa wananchi wa Mtwara katika maeneo
yafuatayo:
o Kwanza, serikali imekosea kufikiria kujenga kituo cha kufulia umeme
unaotokana na gesi asilia Kinyerezi Dar es Salaam badala ya Mtwara.
Uamuzi huu haujazingatia historia ya wananchi wa Mtwara
iliyowatumbukiza katika umasikini wa kutupwa. Kwa mantiki hiyo,
serikali hajaweza kujenga hoja ambayo itawafanya wananchi wa Mtwara
waridhike na mradi huo wa serikali.
o Pili, serikali haijatoa elimu na maelezo ya kutosha kuhusu Matumizi
ya gesi hiyo iliyogunduliwa Mtwara ili WanaMtwara wapate fursa ya
kuhoji kama mradi huo utakuwa na manufaa kwao au la. Wakati umepita wa
kuwachukua wabunge tu na kuwalipa posho lukuki halafu kuwataka
wapitishe mradi. Katika mazingira haya wabunge hukosa ujasiri wa
kukosoa mradi. Kwa hiyo serikali ilitakiwa kushuka chini kwa wananchi
wenyewe kwa jambo zito kama hili.
o Tatu, serikali imeshindwa kutumia busara na hekima katika
kushughulikia madai ya WanaMtwara kuhusu gesi. Badala yake, imetumia
lugha chafu ambayo imejenga chuki kubwa miongoni mwa wananchi kwa
serikali na Viongozi wake.
o Nne,serikali imeendeleza hali ileile ya kudharau mambo ya mikoa ya
kusini. Majibu ya serikali kwa wananchi wa Mtwara yamekuwa rahisi mno
tofauti na hoja waliyoitoa wananchi. Mpaka sasa serikali imeshindwa
kuona kuwa jambo hili ni zito na hatima yake sasa hivi limefikia hatua
mbaya ambayo serikali haiwezi kuitatua.
o Tano, serikali imeendeleza utaratibu uleule wa kutumia propaganda
katika masuala mazito kama hili la gesi. Imetoa kauli za uwongo kama
kusema kwamba wananchi wa Msimbati wanapatiwa umeme bure, wamejengewa
barabara mzuri ambazo hata Mwananchi wa kawaida anapata picha mbaya
juu ya serikali yake na kupoteza Imani ya serikali.
o Sita,Shirika la Maendeleo ya Petroli(TPDC) wanasema moja ya
mafanikio yao ni kuishauri serikali juu ya mradi wa kujenga bomba la
gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dares-Salaam,haya yalielezwa
katika warsha ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia kwa
kamati ya ushauri ya mkoa wa Mtwara(Rejea kitini ya warsha hiyo tarehe
20 Julai,2012-Mtwara).Hii nayo ni hujuma kubwa kwa wananchi wa mkoa wa
Mtwara.
Kwa hiyo, hizi ndizo nukta muhimu ambazo serikali imefanya sivyo kwa
wananchi wa Mtwara na kwa lugha nyepesi ni kwamba misingi ya uadilifu,
uwazi na utawala bora katika kusimamia rasilimali za nchi kwa maslahi
ya wananchi haijazingatiwa.
32. Maoni ya Shura kwa Serikali
Baada ya kutafakari kwa kina namna mgogoro huu ulivyochukua sura mpya,
shura inaishauri serikali kama ifuatavyo:
o Kwanza, serikali iachane na mpango wa kusafirisha gesi kwenda Dar
es Salaam kwa sababu inaonesha dhahiri kwamba katika hili ilikurupuka
na haikujipanga na badala yake itumie muda wa kutosha kutafakari madai
ya wananchi na kuona namna iliyo bora ya kuvuna gesi ya Mtwara.
o Pili, serikali iache kupuuzia mgogoro huu na badala yake iratibu
namna itakavyokutana na wananchi wa Mtwara ili isikilize hoja za
wananchi na kuzijibu kwa kutoa maelezo ya kina.
o Tatu, ingawa kuna usemi kuwa mkubwa hakosei lakini serikali haina
budi kurudi nyuma na kuona kuwa katika hili la gesi ya Mtwara
haijatenda vema. Ikubali udhaifu huo na izingatie maoni ya wananchi
kwa sababu wao ndio walinzi namba moja wa rasilimali za taifa.
o Nne, serikali ijue kwamba haina namna nyingine ya kuendelea na
mradi huu kinyume na kutumia nguvu za kijeshi kwani wananchi
wamedhamiria kufa kwa ajili ya gesi. Kwa hiyo tafsiri rahisi ya hatua
yeyote ile ya kuendelea na mradi huu ni kwamba serikali imeamua
kumwaga damu za wananchi wa Mtwara. Sasa serikali ipime yenyewe kati
ya manufaa yatakayopatikana kwa kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam
na roho za wananchi zitakazopotea kwa kupinga mradi huo kipi ni cha
heri?.
o Tano, Mkuu wa mkoa Mh.Joseph Simbakalia na Mh.waziri wa nishati na
madini Pro Dr Sospeter Muhongo wawaombe radhi wananchi wa Mtwara kwa
maneno yao ya kejeli kwa kuwaita wahaini wananchi wa mkoa wa Mtwara
wanaopinga gesi kusafirishwa katika bomba hadi Dares-Salaam.
Mwisho kabisa serikali haina budi kubadilika kimawazo na kuona kuwa
mikoa ya kusini ina haki ya kuendelezwa kiuchumi. Serikali iachane na
kasumba ya KILA KITU Dar es Salaam. Umefika wakati sasa wa kuendeleza
mikoa mingine ili mrundikano wa watu Dar es Salaam upungue na usawa wa
maendeleo upatikane kati ya mikoa mbalimbali ya nchi yetu. Hii hali ya
kupendelea maeneo Fulani tu na kulazimisha kuwa kila jambo liende huku
na maeneo mengine ni ya kuendeleza maneo ya wenzao ndio itaifanya nchi
hii siku moja IPASUKE vipande vipande wakati kila watu watataka wabaki
na mikoa yao.
TAMKO – SHURA YA MAIMAM INAUNGANA NA WANANCHI WA MIKOA YA KUSINI
KUITAKA SERIKALI ISITISHE MPANGO WA KUSAFIRISHA GESI ASILIAYA MTWARA
KUPELEKWA DARES-SALAAM NA BADALA YAKE MTAMBO WA KUFUA UMEME WA
MEGAWATT 300 UJENGWE MTWARA KAMA ULIVYOKUSUDIWA AWALI KABLA YA USHAURI
MBAYA WA TPDC KWA SERIKALI. NA KWA KUWA TUNAAMINI KUWA SERIKALI YETU
NI SIKIVU ITATUSIKILIZA WANANCHI WA MIKOA HII YA KUSINI kama
ilivyowasikiliza wananchi wote wa Tanzania tulipoitaka serikali kuwa
na mjadala kuhusu kuandikwa kwa KATIBA MPYA ingawa msimamo wa serikali
mwanzo ulisema katiba iliyopo inakidhi haja za wakati huu.
Ee ALLAH shuhudia kuwa tumefikisha na tumetekeleza wajibu wetu.
Chanzo: Wanabidii Forum
No comments :
Post a Comment