Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 7, 2013

Wanasiasa waichambua Serikali ya JK 2012


Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuunga mkono wakazi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam. Kulia ni Katibu wa Kampeni na Uchaguzi NCCR, Faustine Sungura. Picha na Michael Jamson 
Na Waandishi Wetu  (email the author)

Posted  Jumatatu,Januari7  2013
KWA UFUPI
“Matukio ya kukojolewa kwa kitabu kitakatifu (Quran), kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa na kuongezeka kwa vuguvugu za kidini, ni baadhi ya mambo ambayo nayaona kuwa hayakushughulikiwa ipasavyo na hili ni doa kubwa kwa utawala wa Rais Kikwete,” alisema Profesa Lipumba.
WANASIASA wametoa tathmini ya utendaji wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa mwaka 2012, huku wakibainisha upungufu katika maeneo kadhaa ambayo wameishauri iongeze nguvu kuyatekeleza mwaka huu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema pamoja na Rais Kikwete kujisifu kwamba Serikali yake imefanikiwa mambo mengi, kuna maeneo mengi ya msingi ambayo hayakufanikiwa.
Katika salamu zake za mwaka mpya Desemba 31, 2012, Rais Kikwete alifafanua mambo mbalimbali ambayo Serikali yake ilifanikiwa kuyatekeleza mwaka uliopita kwenye sekta za elimu, afya, kilimo, nishati na gesi, miundombinu na barabara, huku akikiri pia changamoto katika maeneo kadhaa.
“Mwaka tunaoumaliza leo ulikuwa wenye mambo mengi mazuri na mafanikio makubwa, lakini ulikuwa na changamoto zake. Baadhi zilikuwa ngumu na zipo zilizokuwa za kusikitisha na kuhuzunisha,” alisema Rais Kikwete.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kwamba baadhi ya maeneo Rais aliyoshindwa kuyafanikisha ni utekelezaji wa Kilimo Kwanza... “Nenda kamuulize mzazi wako, najua ni mkulima kule kijijini.
Akuelezee kama anajua chochote kuhusu Kilimo Kwanza. Wanayosema viongozi wa Serikali ni siasa tu hakuna mikakati ya kiutendaji,” alisema Dk Slaa.
“Kutofanikiwa kwa Kilimo Kwanza kunatokana na mikakati isiyo makini. Serikali iliagiza matrekta, lakini ikashindwa kuyasimamia na hata kuwajengea uwezo wananchi katika kutekeleza mbinu za mapinduzi hayo.”
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema utendaji wa Serikali mwaka jana 2012 haukuwa wa kuridhisha, ingawa kuna mwonekano wa mafanikio.
“Katika utendaji wake, hakuna alama yoyote iliyoongezeka, ameendelea (Rais) kushikilia alama ileile kama ya miaka ya nyuma. Haimaanishi kwamba amekwenda chini, hapana. Jambo la msingi ni kwamba amekuwa siyo mwepesi kusimamia mambo yake ya msingi.”
Lipumba alitaja baadhi ya mambo aliyosema kuwa yamemtia doa Rais katika utendaji wake mwaka 2012 kuwa ni polisi kuwaandama wananchi na wakati mwingine kujitokeza kwa vifo vilivyohusishwa na utendaji mbaya wa jeshi hilo.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vilitumbukia kwenye kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka ikiwamo kusababisha vifo vya raia, jambo ambalo linakwenda kinyume na misingi ya utawala bora.
Tumeshuhudia matukio ya raia kuuliwa kule Morogoro na tukio la kuuliwa kwa mwandishi wa habari mkoani Iringa. Jambo la kushangaza ni kwamba pamoja na matukio hayo kukithiri na Jeshi la Polisi kuwa na mikono yake, lakini hakuna hatua makini na za wazi zilizochukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu hali ya kiasa na amani ya nchini, Profesa Lipumba aliulaumu utawala wa Rais Kikwete kwa kushindwa kushughulikia kikamilifu vurugu za kidini ambazo zilisababisha baadhi ya maeneo kukumbwa na uharibifu wa mali.
“Matukio ya kukojolewa kwa kitabu kitakatifu (Quran), kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa na kuongezeka kwa vuguvugu za kidini, ni baadhi ya mambo ambayo nayaona kuwa hayakushughulikiwa ipasavyo na hili ni doa kubwa kwa utawala wa Rais Kikwete,” alisema Profesa Lipumba.
Hata hivyo, alipongeza namna Rais Kikwete alivyofaulu kuanzisha mchakato wa uandikwaji wa Katiba Mpya akisema kuwa hiyo ni hatua kubwa ambayo inapaswa kupongezwa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema migogoro mingi inayotokea nchini inasababishwa na baadhi ya viongozi wa Serikali iliyopo madarakani kupoteza mwelekeo.
“Uongozi serikalini una matatizo kwa kuwa umeshindwa kuchukua uamuzi sahihi na wakati sahihi, badala yake hukumbuka kufanya hivyo wakati tayari damu za Watanzania zimeshamwagika. Wabunge, wakuu wa mikoa na mawaziri badala ya kutatua migogoro inayolikabili taifa, wao wamegeuka kuwa walalamikaji tu,” alisema Mbatia.
Akizungumzia migogoro ya kidini alisema: “Nadhani kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu migogoro ya kidini kwa kuwa hata uteuzi wa viongozi hivi sasa unahojiwa katika misingi ya dini.”
“Tunamwomba Rais Kikwete tushirikiane kwa pamoja kumaliza suala hili, tukae meza moja sisi kama wanasiasa, viongozi wa dini na wadau mbalimbali kujadili migogoro hii kwa kuwa tunapokwenda si kuzuri.”
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, alitaka usigeuzwe kama amri ya Mungu, kwamba ni lazima Katiba hiyo ipatikane mwaka 2014.
“Tunataka Katiba itakayoweka masilahi ya Watanzania pamoja, hii siyo amri ya Mungu kwamba lazima iwe imepatikana mwaka 2014, Kenya walitumia zaidi ya miaka mitano kuandika Katiba yao, sasa wapo katika mchakato wa kuifanyia marekebisho,” alisema Mbatia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP Augustine Mrema alisema pamoja na mambo mengi Serikali iliyoyafanya, mwaka jana, ilishindwa kuchukua hatua kadhaa kumaliza kero za wananchi.
Alitaja moja ya kero hiyo kuwa ni kunuifaka na rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao akigusia suala la kupatikana kwa gesi asilia huko Mtwara na jinsi wananchi wa huko wanavyozuia lisijengwe bomba kuisafirisha hadi Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democracy (ADC), Saidi Miraji alisema katika kipindi cha mwaka jana mawaziri wake walishindwa kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao.
Alisema hujuma za wizi Tanesco na hila zilizofanywa kulifilisi lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRL), ni miongoni mwa mambo ambayo yameonyesha ubabaishaji wa baadhi ya viongozi wa Serikali.
“Watu wameuziana nyumba za reli kwa bei ya kutupa (bei ndogo), baadhi ya nyumba katika stesheni za reli zimehujumiwa kwa kuvunjwa na kung’olewa madirisha na mbaya zaidi hivi karibuni Serikali imetangaza kulifufua shirika hilo wakati wao wenyewe ndiyo walichangia kuliua. Naibu Mkurugenzi wa Uenezi wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Shaaban Kirita alishangaa uharaka wa Serikali kuondoa mawimbi ya analojia kwenda dijitali akisema huu ni mzigo mwingine kwa wananchi.
“Ving’amuzi ni njia ya kutaka wananchi wasijue kinachoendelea katika Serikali yao, kwani hivi sasa walio wengi hawana tena fursa ya mawasiliano. Hawaoni taarifa ya habari wala kujua kinachoendelea,” alidai.
Habari hii imeandikwa na Leon Bahati Joseph Zablon, Aidan Mhando na Fidelis Butahe.
Chanzo: Mwananchi

No comments :

Post a Comment