Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, March 24, 2013

Bora kero za Muungano kuliko za SMZ

Salim Said Salim,
MARA nyingi tunawasikia watu wa Zanzibar wakiwemo viongozi wa siasa na dini wakizungumzia kile wanachokiita kero za Muungano.
Lakini ukichunguza utaona zipo kero nyingi ambazo sio za Muungano zinazowanyima watu wa Unguja na Pemba haki, demokrasia ya kweli, utawala wa haki na sheria.
Kwa jinsi hali ilivyo, mtu hata akiwa hapendi kusema hivyo, atakuwa hakosei akisema upo ubaguzi Zanzibar na kwa bahati mbaya serikali haionekani kuchukua hatua za kuuondoa.
Ubaguzi huu unapata mashiko kutokana uwepo na mfumo wa kuwa na raia wa daraja la kwanza na daraja la pili.
Vile vile lipo kundi kubwa la watu unaoweza ukasema maisha yao, kwa kiwango fulani, yanalingana na yale ya wakimbizi.
Tofauti iliyopo kati ya wakimbizi tunaowajua kuwepo katika nchi mbalimbali ni kuwa hawa ni watu waliokimbia nchi zao na kwenda nyingine kwa sababu mbalimbali kutafuta usalama wakati hawa wa Zanzibar wao wapo kwao, lakini wanaishi kama wakimbizi.
Kwanza nitazungumzia hiki nilichokiita raia nambari moja na nambari mbili ambacho nataka kusisitiza kuwa kipo wazi na kwa bahati mbaya kinaonekana zaidi mahakamani, pahala ambapo mtu hutarajia kuona utawala wa haki na sheria unachukua mkondo wake.
Ni kawaida kuona katika mahakama za Zanzibar hakimu akitoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa ni kupata wadhamini ambao ni wafanyakazi wa serikali.
Kutolewa kwa sharti hili kunasababisha mtu mwengine, awe mfanyabiashara, mkulima, mvuvi au mweye kufanya shughuli zake binafsi zinazomuendeshea maisha yake kutokuwa na haki ya kumdhamini mshitakiwa.
Hapana kielelezo chochote unachoweza kukitoa kwa mwenendo huu unaoonekana kuwa wa kawaida isipokuwa ni kuwabagua raia.
Hapa umma unaelezwa kuwa kwa mtazamo wa mahakama wapo watu ambao ni safi na wanaoaminika na wengine wasioaminika.
Hawa wanaoaminika ni watumishi wa umma ambao wenyewe siku hizi wanapenda kuitwa wafanyakazi wa serikali.
Suala hili limelalamikiwa sana na wanasheria na wananchi kama ni kero kubwa. Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu alikiri katika kipindi kimoja cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Zanzibar, akilalamikia kero hii.
Jaji Mkuu aliahidi kwamba yeye na “wenzake” (hakuwataja watu hao ni nani) walikuwa wakutane na kulitafakari suala hili. Sasa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu atoe kauli ile na hakuna taarifa yoyote ya kufanyika huo mkutano au suala hili kuonesha dalili za kurekebishwa.
Kwa kweli hali hii haitoi sura nzuri kwa serikali inayojiita kuwa ya demokrasia na inayoheshimu utawala bora wa haki na sheria.
Sasa nije katika hili suala la wakimbizi waliopo ndani ya nchi yao ya visiwa vya Unguja na Pemba na vingine vidogo kama Tumbatu, Kojani na Kisiwa Panza.
Hawa “wakimbizi wa nyumbani kwao” ni maelfu ya watu, wanaume na wanawake, ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakinyimwa vitambulisho vya Mzanzibari na haki ya kupiga kura katika chaguzi za Zanzibar.
Watu hawa wapo tu, wanaishi na kufanya kazi, lakini hawana haki ya kushiriki katika uamuzi wa kuchagua viongozi wa nchi yao. Hii sio haki na wala sio utawala bora, na kisingizio chochote kile hakiwezi kuhalalisha kuwepo kwa uovu huu.
Tatizo kubwa wanalokabili hawa “wakimbizi” wanaozidi 30,000 ambao bado hawajatambulika rasmi na Umoja wa Mataifa, ijapokuwa taasisi za kutetea haki za binadamu na sheria za ndani na nje zinalalamika, ni hawa masheha (wawakilishi wa serikali katika sehemu wanazoishi) wanaodai kuwa hawawatambui kuwepo kwao.
Lakini masheha hao hao ambao hawajui uwepo wa watu hawa katika maeneo yao, wanawataka watu hawa wahesabiwe katika zoezi la sensa. Sijui vipi utamhesabu mtu ambaye hayupo!
Ama kweli hawakukosea wale waliosema mambo ambayo huyaoni kufanyika kwengine duniani utayashuhudia Zanzibar.
Lakini ukweli wa mambo ni kuwa wengi wa hawa waliobaguliwa na kufanywa wakimbizi wamezaliwa wao na wazee wao katika maeneo hayo wakati hao masheha ni watu wa kuhamia sehemu hizo walizopewa usheha.
Hapana haja ya kuzunguka mbuyu. Ukweli ni kuwa yote haya yanafanyika kwa sababu za kisiasa zilizopitwa na wakati za kutaka kuwanyima haki ya kupiga kura kwa kisingizio kuwa sio wakazi wa maeneo hayo na kwahivyo hawastahiki kuandikishwa kupiga kura katika sehemu hizo.
Moja ya njia ya kutekeleza mpango huo ni kuwanyima vitambulisho vya Mzanzibari na wakati huo huo kuwapa watu ambao hawastahiki.
Tujaalie kuwa kweli watu hao hawaishi sehemu hizo, lakini hapana ubishi kuwa wanaishi katika ardhi au bahari ambayo inayoitwa Unguja na Pemba. Baadhi yao hupewa hati za usafiri Zanzibar, leseni za biashara na bili za umeme wanazolipa ni za nyumba zilizopo Visiwani. Ni kichekesho.
Sasa kama watu hawa kutokana na kudaiwa sio wakazi wa sehemu waliodai, lakini wanaishi sehemu nyingine ya visiwa vya Unguja na Pemba (sio mbinguni) kwanini wasipewe angalau haki ya kushiriki katika uchaguzi wa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)?
Tunaambiwa lakini hili hatuoni kuzingatiwa, kuwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi eneo lote la Unguja na Pemba ni jimbo moja la uchaguzi wa rais wa Zanzibar na kwahivyo wapi mtu anaishi ndani ya visiwa hivi halina uzito wowote.
Hivi karibuni tumeelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi, Mohamed Juma Ame, kuwa anavyo vitambulisho 25,673 vinavyotakiwa kuharibiwa baada ya wahusika kushindwa kuvichukua mwaka 2010 katika Kisiwa cha Pemba.
Ninaamini ukweli wa suala hili haujaelezwa na lipo lililojificha au linalofichwa kwa sababu wengi wa watu wenye asili ya Pemba ndio wanaolalamika kukosa vitambulisho. Ninaamini kwa dhati kama utafanyika uchunguzi huru ukweli uliosababisha hali hii kuwepo utajulikana.
Hapo ndipo ukweli utadhihiri na uongo kujitenga. Vinginevyo, maelezo mengine yoyote yale yatakuwa na mushkeli. Tuache kudanganyana.
Kinachonishangaza ni kwamba panapotolewa taarifa za aina hii za watu kutokwenda kuchukua vitambulisho vyao, waandishi wa habari ambao wanajulikana kwamba watauliza maswali yatayotaka ufafanuzi, kuweka mambo hadharani au kuhoji mwenendo wa utoaji wa vitambulisho, huwa hawaalikwi kama vile mikutano ya kutoa taarifa hizo ni siri.
Hata sheria yenyewe ya vitambulisho vya Mzanzibari sio ya haki na unaweza bila ya kutia chumvi kuwa ni batili na si ya kidemokrasia.
Nasema hivi kwa sababu sheria hii inaeleza kuwa kwa Mzanzibari kutokuwa na kitambulisho ni kosa la jinai.
Sawa sheria imeamua kutamka hivyo. Lakini kinachoshangaza ni kuwa haisemi mtu anayemnyima Mzanzibari haki yake ya kupata kitambulisho naye atakuwa ametenda kosa la jinai. Tujiulize kwanini sheria haikumbana mtu anayemuwekea vikwazo mtu anayestahiki kupata kitambulisho?
Kama sheria ingekuwa inabana pande zote mbili hivyo ninaamini masheha wengi wangekuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuwazuia watu wenye haki ya kupata vitambulisho kutopewa. Hivyo tunataka kuambiwa hili halijaonekana? Siamini, lakini ninahisi upungufu huu umefanywa kwa makusudi na walioiandika sheria hiyo ndio wanajua zaidi undani wake.
Katika suala hili pia kipo kichekesho kingine au kile unachoweza kukieleza kama mchezo wa kuigiza.
Miezi michache iliyopita, nilishangaa nilipomsikia Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, akitoa taarifa ya kuwataka watu waliopewa vitambulisho vya Mzanzibari wakati hawakustahili kuwa navyo wavirejeshe.
Makubwa haya. Kwanza watu hawa wanaoombwa kuvirejesha hivyo vitambulisho walivipataje na nani aliwapa na ipo tabu gani kuwakamata watu hao waliovunja sheria? Kwa nini hao waliovunja sheria kwa kutoa vitambulisho kwa watu wasiostahiki wasiwajibishwe?
Hapa hapana hatua zozote zile za kisheria zitakazochukuliwa kwa sababu inaonekana upo mkono wa kisiasa ndani yake. Tusidanganyane, sote ni watu wazima na wengine tunaelewa mambo kuliko hao wanaotaka kutudanganya. Wanaotaka kudanganya wafanye hivyo kwa ukuta na sio kwa Wazanzibari na Watanzania kwa jumla.
Wakati umefika sasa kwa viongozi wa serikali, jamii na wanasiasa wa Zanzibar kuelewa zama za kudanganyana kama wanavyofanyiwa watoto wadogo na baadhi ya wazazi kwa kuwapa pipi pale wanapotaka kuwakimbia nyumbani zimepita na hazirudi tena.
Wanaoota, iwe mchana au usiku, kwamba zama zile zitarudi wajue hilo ni lile ambalo Waswahili walilieleza kama “Yaguju”. Wasiojua maana ya msemo huu wawaulize wazee na wataelezwa kwa undani maana yake.
Kwa ufupi mtu anapokwambia “Yaguju” huwa anakutaka uwache kuishi maisha ya Ali Nacha. Kama pia hujui hekaya ya Ali Nacha, basi wewe sio Mzanzibari na pia hustahili kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari!
Tuache kutamani maisha ya ndoto na tuukubali ukweli wa maisha tuliyokuwa nayo hivi sasa na tuwe waungwana, watu wenye wema na ihsani na watiifu kwa mfumo wa utawala wa kidemokrasia, haki na sheria.
Sio vyema na ni hatari kufumbia macho maandishi yaliyopo ukutani kwa muda mrefu kwani anayefanya hivyo hatimaye hujikuta huo ukuta ambao hataki kusoma maandishi yake unamuangukia.
Kwa kawaida katika dunia ya leo mtu anapoangukiwa na ukuta kwa sababu alizojitakia, umma humuangalia na wengine huwa hawana huruma na husema “aliyataka” au “astahili yamfike”.
Tujirekebishe leo kabla wakati haujachukua nafasi yake ya kuturekebisha kwa tuliyoyafanya siku za nyuma na haya tunayoyatenda hivi sasa kwa mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu.
Tuhakikishe watu wote wa Unguja na Pemba ni sawa na wanatendewa haki na hatuna Wazanzibari ambao wanakuwa kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Naomba kila mmoja wetu popote pale alipo, achukue juhudi za kujifunza haraka na tusingoje ulimwengu wetu huu usiokuwa na huruma wala muhali kuja kutufunza huku shingo zetu zikiwa upande na kuona kama vile tunaonewa.
Kumbukeni ndugu zangu mambo kangaja, huenda yakaja.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments :

Post a Comment