Na Miza Kona-Maelezo Zanzibar 21-03-2013
OFISI ya Idara ya Utamaduni ya Kikundi cha Sanaa Taarab iliyopo Ngome Kongwe, Mjini Zanzibar, imeteketea kwa moto na kuharibu vitu vyote vilivyokuwemo ndani ya ofisi hiyo…
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika eneo la tukio, Katibu wa kikundi hicho Daud Shadhil AbdulMalik amesema moto huo ulitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 10.15 za alfajiri na kusababisha hasara kubwa.
“Vitu vyote vimeteketea kwa moto hakuna kilichobakia wala hakuna kinachofaa ” alisema Katibu huyo kwa huzuni.
Alivitaja vitu vilivyoungua kuwa ni pamoja na fedha taslim shilingi milioni mbili na laki tano, majenereta mawili makubwa pamoja na vifaa vyote vya muziki vinavyotumiwa na kikundi hicho.
“Kuna baadhi ya vifaa vilikuwa zaidi ya seti moja na vyengine vililetwa kwa ajili ya kuongezea uwezo, tunaviita vitu vya moto na baridi hivyo vyote pia vimeteketea”, alisikitika bwana Daud.
Aidha alisema kuwa chanzo cha moto na thamani ya vitu hivyo bado havijajulikana lakini vinakisiwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 70 na aliiomba Wizara husika kuwapatia ofisi na vifaa vyengine ili waweze kufanya kazi zao kama kawaida.
Hata hivyo ameishukuru Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kufika kwa wakati sehemu ya tukio na kufanikiwa kuuzima moto huo.
Kikundi cha sanaa Taarab kina ofisi zake eneo la Ngome Kongwe ikiwa pamoja na ghala na sehemu ya kuhifadhia kumbukumbu.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments :
Post a Comment