NA ELIZABETH ZAYA
19th March 2013
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema kuna umuhinu wa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi wa ngazi ya juu kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Sitta aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mafunzo ya viongozi waandamizi, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Alisema viongozi wengi hutumia muda mwingi katika kufanya mambo mengine tofauti na majukumu yao, hivyo kushindwa kutekeleza wajibu na malengo ya kazi yao.
“Ni mambo ya kizamani kwamba ukiteuliwa kuwa kiongozi basi umekamilika, kiongozi anahitaji kujifunza pia ili ajue wajibu wake na namna ya kutekeleza ipasavyo majukumu yake,” alisema Sitta na kuongeza:
“Viongozi wengi wanasahau kwamba anapoteuliwa majukumu yake makubwa ni kuwahudumia wananchi, lakini kila siku wanatoa majibu eti wako bize, badala ya kuwahudumia wananchi, wanashindia kupekua mafaili kuanzia asubuhi mpaka wanatoka, wanawaambia wananchi njoo kesho kila siku. Huwezi kusema hauna nafasi wakati umeteuliwaili uhudumie wananchi.”
Sita aliongeza kwamba suala jingine linalowasumbua viongozi wengi ni namna ya kutumia muda katika kazi zao.
Alisema kiongozi mzuri ni yule anayejua kutumia muda wake vizuri na kwamba tatizo kubwa linalochangia viongozi washindwe kutekeleza majukumu yao vizuri ni kutokana na kushindwa kutumia muda wao vizuri.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Joseph Semboja, alisema mafunzo hayo mbali na kuwajengea uwezo katika utendaji wao, lakini pia yatawasaidia katika kushindana na wenzao wa Jumuia ya Afrika Mashariki katika masuala ya uongozi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment