Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, March 20, 2013

Vitega uchumi CCM vinapogeuzwa ‘shamba la bibi’

NA SABATO KASIKA
20th March 2013
Katibu wa Uchumi na Fedha wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Zakia Meghji
Chama cha Mapinduzi (CCM), kina vitega uchumi vingi ambavyo vimesambaa katika mikoa mbalimbali nchini, madhumuni ya kuanzishwa kwa vitega uchumi hivyo ni kukisaidia chama hicho kujiendesha ingawa imekuwa kinyume chake.
Lakini nia na malengo ya kuanzishwa kwa miradi hiyo hayajafikiwa kutokana na fedha za miradi hiyo kuishia mifukoni mwa watu waliopewa dhamana ya kuisimamia kama CCM wenyewe wanavyosema.
Ndiyo maana hivi karibuni Katibu wa Uchumi  na Fedha wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Zakia Meghji amekuja na mkakati unaolenga kudhibiti mali za chama kwa kupitia upya mikataba yote ya vitega uchumi vya chama hicho.
Chama hicho kinasema kuwa kimeamua kuchukua hatua hizo baada ya kubaini kuwa vitega uchumi vyake vimegeuzwa na baadhi ya wanachama kama ‘Shamba la Bibi’ ambalo mazao yake yanavunwa na kila mtu kwa manufaa yake.
Maana ya ‘shamba la bibi’ ni kwamba hakuna usimamizi wa kutosha katika jambo fulani hali inayowafanya wahusika wafanye kila wanachotaka na kwa wakati wanaoona unafaa.
Wahusika waliopewa dhamana ya kusimamia jambo fulani hawana hofu ya kuwajibishwa kwa kuwa wanajua hakuna mtu wa kuwasimamia hivyo kama ni fedha wanazokusanya wanazitumbukiza kwenye mifuko yao.
Mkakati huo mpya kama utafanikiwa, basi utakuwa umewaumiza baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao wamekuwa wakitegemea vitego uchumi vya CCM kujinufaisha, kwa madai kwamba hawapati ruzuku ya chama.
Meghji anasema pamoja na kwamba Chama cha Mapinduzi kina vitega uchumi vingi, bahati mbaya kimekuwa kikiambulia mapato kidogo na kwamba hali inayoonyesha kuna baadhi ya wanachama wanaonufaika zaidi.
Anaitaja baadhi ya mali hizo za chama ambazo ni vitega uchumi kuwa ni mashamba,viwanja, majengo, maegesho ya magari na vingine vingi karibu kila kona ya nchi ambavyo anaamini mikataba yake ikipitiwa upya inaweza kuimarisha uchumi wa chama.
Anasema vitega uchumi hivyo vimekodishwa kwa fedha kidogo isiyolingana na thamani yake huku baadhi ya mikataba iliyoingiwa ikiwa imepitwa na wakati.
Anasema kutokana na idadi ya vyanzo vya mapato vinavyomilikiwa na chama hicho kilipaswa kuwa kinakusanya zaidi ya Sh. bilioni 52 kwa mwaka lakini wamekuwa wakikusanya kiasi kidogo ambacho hakiendani na vyanzo husika.
Katibu huyo wa Uchumi na Fedha wa CCM amesema maeneo yatakayobainika kuwa na wizi watendaji wake watawajibishwa kwa mujibu wa taratibu za Chama kupitia mikoa na wilaya zao na kuwa uchache huo wa mapato kwa kiasi kikubwa umechangia na mfumo wa uendeshaji wa chama ambao kwa sasa unapaswa kubadilishwa.
Wakati Meghji akiendelea na mkakati huo, ofisi nyingi za CCM zina miradi ya uegeshaji wa magari, ambapo inadaiwa kuwa fedha zinazopatikana zimekuwa vikitumiwa an viongozi wa ofisi husika.
Kama kweli ndivyo ilivyo, basi mkakati wa kigogo huyo utakuwa mateso kwa baadhi ya viongozi hao, kwa sababu watakosa ulaji ambao wamezoea kuupata kila siku bila chama kunufaika.
Wapo wale ambao wameanza kubeza hatua hiyo wakidai kuwa yeye siyo mtu kwanza kupitia upya mikataba hiyo na kwamba atafika mahali atashindwa kuendelea na mkakati wake huo.
Wanadai kuwa wapo viongozi ambao wamefurukuta kufanya hivyo lakini wanajikuta wakikwama, hivyo wanaamini kwamba mkakati wa Meghji ni sawa na nguvu ya soda ambayo haiwezi kufanikiwa hata kidogo.
Wanatolea mfano kwa aliyewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa kupitia mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madadiba, aliyejaribu kuibua miradi mbalimbali katika ofisi chama lakini akakutana na upinzani mkali.
Hivyo wanadai kuwa wana uhakika hata mwana mama huyo atajikuta akiachana na mkakati huo kwasababu waliomtangulia walishindwa kufanikiwa kutokana na mazingira halisi yalivyo ndani ya chama.
Madabida ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kauli yake wakati huo alisema alikuwa na nia nzuri iliyolenga kuibua miradi ya kukinufaisha chama, lakini akawekewa kauzibe.
Baadhi ya viongozi wa chama na hasa ngazi za matawi na kata wamekuwa wakidai kuwa ruzuku inayotolewa na serikali, fungu kubwa limekuwa likiishia wilayani wakati wao wanaambulia kidogo.
Viongozi hao wanadai kuwa wanachama wanapatikana kwenye ngazi ya mashina, matawi na kata ambako chama kingeelekeza fedha nyingi za ruzuku, lakini badala yake zinaishia wilayani ambako hakuna wanachama.
Kutokana na ngazi hizo kukosa ruzuku, chama kimekuwa kikitumia fedha za miradi hiyo kuendesha shughuli zake huku kiasi kingine kikitumiwa na viongozi, kwa vile hawalipwi mshahara.
Kwa mazingira kama ipo haja kwa Meghji kuliona hilo na kutafuta uwezekano wa kuwasaidia wakati akiwa na mkakati wa kudhibiti mali za chama kwa kupitia upya mikataba yote ya vitega uchumi vya chama hicho tawala.
Nasema hivyo kwa sababu inawezekana viongozi hao wanatumia fedha za miradi kwa manufaa yao, kutokana na ukweli kwama hawapati chochote kutoka juu ingawa ndiyo wenye kazi kubwa ya kusaka wanachama wapya.
Ikumbukwe kwamba kuwaacha viongozi wa ngazi za chini bila kitu kuchangia kuwepo kwa ufisadi kwenye miradi ya chama, hivyo upitiaji upya wa mikataba hiyo uende sambamba na kubuni namna ya kuwasaidia.
Hivyo ni vyema hiyo ruzuku ya chama ikashushwa hadi kwenye ngazi hizo za chini, kwani CCM kama vilivyo vya vingine vya siasa kinapata ruzuku kutoka serikalini, hivyo hakina budi kuepuke ufisadi kwa kuwasaidia viongozi wa chini.
Inawezekana mazingira kama hayo yakawa ndiyo yamesababisha.
Kwa mazingira hayo ni vyema mkakati huo wa mama Meghji ukalenga kufufua mradi mkubwa wa CCM wa Shirika la Uchumi na Kilimo Tanzania (SUKITA) uliofilisiwa na wajanja wachache ndani ya chama hicho.
SUKITA ilichangia kukiingizia chama hicho fedha, lakini sasa haupo tena baada ya kutafunwa huku kukiwa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
Aidha, wakati huu ambao mama Meghji anaendesha mkakati huo wa kupitia upya mikataba ni vema pia akatafuta pia chanzo cha kufa kwa miradi mingi ya chama hicho ukiwemo huo wa SUKITA na kuitafutia ufumbuzi pale inawezekana.
Kama alivyosema ni kweli kwamba chama hicho kinamiliki miradi mingi kama aliyoitaja ingawa hakugusia viwanja vya michezo vikiwemo vya CCM Kirumba jijini Mwanza, Samora, mjini Iringa, Sokoine jijini Mbeya na vingine vingi nchini.
Ni uhakika akifanikiwa katika mkakati huo atakuwa amefanikiwa pia kupunguza ama kumaliza kabisa rushwa na ufisadi kwenye miradi ya chama ambayo imechangia kukifanya chama kikose fedha za kutosha.
Hivi karibuni Baraza la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi (CCM), liliazimia kutumia vitega uchumi vya chama hicho kujiongezea mapato ili kuachana na utegemezi wa ruzuku na kupokea fedha chafu kutoka kwa wahisani na marafiki zao.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Kisumo alisema lengo ni kuongeza mapato ya CCM katika kukabiliana na vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa nchini.
“Siasa bila pesa mapambano hayawezekani… tumezoea kuona misaada ya wazi kama kwa akina Sabodo na wanapeleka Chadema waziwazi, na wengine wanaleta kwetu kwa siri, lakini ndani yake kuna pesa chafu,” alisema kada huyo mkongwe wa CCM.
Alisema utegemezi wa ruzuku unayumbisha chama hicho na kubainisha kwamba, wana dhamira ya kuingia ubia na kuanzisha makampuni huru yatakayoongeza mapato ya chama hicho.
“Huu ni mpango mpya tumeiga kutoka kwa wenzetu Msumbiji, Afrika Kusini na Namibia, tumeona vyama vyao vimefanikiwa kwa kuingia ubia na makampuni kupitia vitega uchumi vyao.
“Tutakuwa na kampuni huru zilizopo kisheria, tutaingia nao ubia, lakini chama kinahitaji fedha safi, hii maana yake si kila fedha zinazokuja kutoka kwa marafiki na wahisani wetu ni chafu,” alisema.
“Tunasema fedha chafu iwapo nyuma yake kuna shinikizo au sharti la kumfanyia upendeleo kwenye jambo fulani, hizo ni fedha chafu… tuliwahi kushindwa wakati ule, lakini sasa tumejipanga kushinda kwenye mfumo huu, ninalosisitiza hapa ni fedha safi kutoka vyanzo huru,” alisisitiza.
Alisema baraza limeagizwa na Halmashauri Kuu (NEC) kuweka utaratibu mpya wa kuimarisha mali za chama zenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 57 zinazohitaji usimamizi bora ili kuongeza mapato.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment