Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameuagiza uongozi wa Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko kuimarisha kitengo cha utafiti katika Wizara hiyo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara Zanzibar.
Dk. Shein ametoa agizo hilo jana wakati akihitimisha mkutano wa kutathmini utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013.
“lazima tuimarishe kitengo cha utafiti katika wizara kwa kufanya mambo ya msingi ya kitafiti ili kitengo kiwe na uwezo wa kushauri na kutoa suluhisho la kasi ndogo ya ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara hapa Zanzibar”alisisitiza
Alieleza kuwa miongoni mwa tafiti hizo zielekezwe katika kuangalia namna ya kuongeza thamani ya mazao kama mwani na karafuu ikiwemo kuanzisha viwanda vitakavyoweza kuzalisha bidhaa nyingine kutokana na mazao hayo.
Sambamba na agizo hilo Dk. Shein ameitaka wizara hiyo kuhakikisha kuwa mkakati wa mageuzi wa Shirika la Biashara (ZSTC) unatekelezwa kwa kasi ili shirika hilo liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“harakisheni utekelezaji wa mpango wa mageuzi katika shirika ili lijijengee uwezo wa kutekeleza majukumu yake katika mazingira ya ushindani kwa ufanisi” alisema Dk Shein.
“harakisheni utekelezaji wa mpango wa mageuzi katika shirika ili lijijengee uwezo wa kutekeleza majukumu yake katika mazingira ya ushindani kwa ufanisi” alisema Dk Shein.
Katika maelezo yake kwa viongozi na watendaji wa wizara hiyo Dk. Shein alilitaka shirika la ZSTC kutekeleza haraka agizo lake la ujenzi wa vituo vya kuuzia karafuu vyenye ubora ikiwa ni mojawapo ya hatua za kuweka mazingira mazuri ya biashara na kuwaondolea usumbufu wakulima wa zao hilo wakati wa mauzo.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kwa kujenga ushirikiano wa karibu na jumuiya ya wafanyabishara hatua ambayo imesaidia sio tu kuwepo kwa chakula chingi nchini lakini pia utulivu wa bei wa bidhaa za chakula kwa kipindi kirefu.
“Naupongeza uongozi wa wizara kwa utaratibu wenu wa kushauriana mara kwa mara na wafanyabiashara utaratibu ambao umesaidia kuwepo na utulivu wa bei ya vyakula kwa muda mrefu sasa” alisema.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Wizara yake Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Mazrui alieleza kuwa dalili za kuimarika kwa sekta ya viwanda Zanzibar zimeanza kuonekana kutokana na matarajio ya kukamilika miradi kadhaa mipya na kuongezeka kwa uwekezaji kwa miradi iliyopo sasa.
Alisema kuwa kwa sasa mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa ni asilimia 12 tu kwa mwaka huku mchango wa sekta ya usarifu wa bidhaa ukiendelea kuwa chini ya asilimia 5.
Waziri alivitaja viwanda vilivyoongeza uzalishaji kufuatia uwekezaji na ukarabati ni kuwa ni Zanzibar Milling Corporation na Zanzibar Bottlers. Viwanda vipya ni cha maji cha Safari Co. Ltd, Pemba Pride, The Perfect Coffee Co. Ltd na Kiwanda cha Maziwa cha Azam huko Fumba.
Akizungumzia tatizo la bei ya mwani kwa wakulima nchini Waziri Mazrui alisema njia pekee ya kuwakoa wakulima hao na kadhia hiyo ya bei isiyostahiki ni kuanzisha kiwanda kitakachotumia malighafi hiyo humu nchini badala ya kutegemea kuuza mwani nchi za nje.
Kuhusu hali ya chakula nchini alieleza kuwa ni nzuri ambapo kati ya Julai 2012 na Machi 2013 wastani wa tani 356,046 za bidhaa muhimu za mchele, sukari na unga wa ngao zilikuwepo Zanzibar kwa matumizi ya ndani ikiwa ni zaidi ya mahitaji.
“mwenendo wa bei za bidhaa hizo kwa soko la ndani uliendelea pia kuwa wa utulivu kutokana na hatua za kisera zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kutuliza makali ya maisha ya wananchi wake ” alieleza.
Chanzo: Zanzinews
No comments :
Post a Comment