Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, April 10, 2013

Ngumi chupuchupu CCM


NA MWANDISHI WETU

10th April 2013

Mwenyekiti wa UVCCM, Hamisi Juma Sadifa.
Siasa za vijana ni moto. Hivyo ndivyo ilijidhihirisha jana katika Ofisi Ndogo ya Makao ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Lumumba, jijini Dar es Salaam ambako baadhi ya makada wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM), waliitwa kuhojiwa.

Hali ilikuwa tete baada ya kuwasili kwa Mwenyekiti wa UVCCM, Hamisi Juma Sadifa, kuitikia wito wa Kamati ya Maadili ya chama hicho, lakini kabla  hata ya kufika kikaoni, alijikuta akiporomoshewa matusi na kada mmoja wa makao makuu (jina tunahifadhi), kwa kuwa hatukumpata kuzungumzia hali hii jana, ambaye alitaka kumchapa makonde.

Akisimulia mkasa huo, Sadifa aliiambia NIPASHE jana kuwa alikutwa na masahibu hayo baada ya kufika Lumumba na kukutana na baadhi ya wana-UVCCM watatu, akawasalimia, lakini mmojawao alikataa kuitikia salamu wala mkono, lakini akaanza kumporomoshea matusi.
“Mimi niliwasalimia kwa pamoja na kuwapa mkono, lakini nilipofika kwa …. Akakataa kupokea mkono wangu na kujitambulisha kwa jina lake kuwa mimi ni….,” alisema Sadifa.

Kutokana na hali hiyo, Sadifa aliamua kumpuuza na kuondoka zake kuelekea ghorofani, lakini akiwa kwenye ngazi, ghafla kada huyo alimfuata nyuma huku akiporomoshea matusi na kutaka kumshambulia.

Sadifa alisema kuwa baada ya kuona hali imekuwa tete, aliamua kukimbilia kwenye ofisi ya Katibu wa Halmashauri Kuu wa Itikadi na Uendezi, kujinusuru.

Kada huyo aliongeza kupandisha mori huku akimsaka Sadifa, lakini alikamatwa na watu wanne (majina tunayo), ili asimdhuru, lakini alivua koti lake ili aendelee kutekeleza azma yake ya kumpiga Sadifa.

“Mimi simfahamu huyu bwana, ndiyo kwanza nimemuona leo (jana) lakini ninaweza kumtambua kwa sura,” alisema Sadifa.

Sadifa alisema ameamua kufuatilia suala hilo, na tayari amekwisha kumwandikia malalamiko Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ili achukue hatua juu ya suala hilo ambalo alisema ni la aibu kwa Chama.
Sadifa na wenzake wanne, Makamu wake, Mboni Mhita; wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia vijana, Deogratias Ndejembi, Jonas Nkya na Jerry Silaa, ambaye pia ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, walikuwa wameitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya chama hicho kwa tuhuma za kushinda nafasi zao kwa njia za rushwa.

Kikao hicho kiliongozwa na maofisa wanne kutoka Idara ya Maadili ya CCM Makao Makuu wakiongozwa na mmoja wa watendaji wakuu wa idara hiyo, katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Barabara ya Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Malalamiko dhidi ya viongozi hao yanadaiwa kuwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili na vijana wanne wa UVCCM, ambao ni Salum Hapi, Paul Makonda, Egler Mwamoto na Edwin Kunambi.

Inadaiwa kuwa wanalalamika kuwa makada wenzao wa UVCCM, aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa; Mjumbe wa Baraza Kuu, Hussein Bashe; Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella, waliandaa mtandao wa kuwawezesha Sadifa na Mboni, kushinda nafasi zao.
Pia wanadaiwa kuwa katika kuandaa mtandao huo kwa kutumia nafasi zao na fedha, waliwawezesha kushinda katika nyadhifa hizo.

Malalamiko mengine ni kuwa Sadifa, Mboni na Nkya, wana umri mkubwa kuliko unaoruhusiwa na kanuni za UVCCM kuwa viongozi.

Habari kutoka ndani ya kikao cha jana zinasema kuwa tuhuma hizo zilipanguliwa zote na walalamikiwa kutaka waliowasilisha malalamiko yao kutoa ushahidi, lakini pia kama ni suala la kuandaa mtandao watu wa kushtaki wanaotuhumiwa na siyo wao.

Taarifa za ndani zinasema kuwa katika tuhuma zote, hakukuwa na ushahidi wowote ulioambatanishwa, isipokuwa madai kwamba kuna picha alipigwa mtu mmoja akiwa na Sh. 500,000 ambazo zinadaiwa ni rushwa.

Hata hivyo, walalamikiwa walipouliza ni kwa nini suala hilo halikuripotiwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), walielezwa kuwa mambo ya Chama yana taratibu zake.

Habari zaidi zinasema kuwa chanzo cha kuanza kuchimbana ndani ya UVCCM ni maamuzi ya Sadifa kutumia madaraka yake kufanya mabadiliko ya mtendaji wa Idara ya Oganaizesheni ya UVCCM, hatua ambayo inadaiwa kukera kada mmoja wa umoja huo ambaye ameapa kuwa atahakikisha Mwenyekiti wake anang’oka katika nafasi hiyo.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment